Samatta ataka Kapombe akumbukwe zawadi Stars

Tuesday March 26 2019

 

Dar es Salaam. Nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta ametoa ushauri kwa Shirikisho la Soka nchini (TFF) kumpa kiasi cha fedha beki Shomari Kapombe aliyeumia mguu akiwa kwenye kambi ya timu hiyo ikijiandaa na Lesotho.

Hadi sasa Kapombe hayuko fiti japokuwa ameanza mazoezi mepesi na timu yake ya Simba inayojiandaa na mechi ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya TP Mazembe ambapo mechi ya kwanza itachezwa nyumbani Aprili, 6 mwaka huu.

Wachezaji wa Stars wameahidiwa zawadi ya viwanja na Rais wa Jamhuri ya Muungano Tanzania, John Pombe Magufuli pamoja na Sh 10 milioni kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda.

Ahadi hizo ni baada ya Stars kuifunga Uganda mabao 3-0 na kufuzu fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) zitakazoanza Juni 21 hadi Julai 19, Misri.

Katika akaunti yake ya Twiter, Samatta ameandika hivi, "Shomari Kapombe, kama kaptain ningeomba TFF imuangalie katika zawadi ambazo wachezaji watapata, ikishindikana basi ningeomba wachezaji wote tumchangie kidogo kidogo na endapo vyote visipowezekana kabisa basi katika zawadi ahadi ya Mh Paul Mkaonda, nitagawana nae nusu kwa nusu,"

Umauzi huo umeungwa mkono na baba yake Mzee Ally Pazi Samatta; "Samatta anafuata akili zangu, anachokifanya ni sahihi kabisa, ikumbukwe kwamba mafanikio yanachangiwa na baraka za watu wengine ikiwemo kuwasaidia."

Advertisement

Kamati ya Saidia Stars ishinde chini ya Makonda ilielezea juu ya hilo kwamba; "Tuliangalia mechi ya mwisho wachezaji waliocheza ndiyo waliopewa zawadi hiyo, ila suala la Kapombe litafanyiwa utaratibu."

Kuhusu wachezaji tisa wa zamani ambao waliipeleka Stars kwenye fainali za AFCON mwaka 1980, ujumbe wao wameupata na utafanyiwa kazi.

Juzi Jumatatu baada ya Rais John Pombe Magufuli aliwaalika wachezaji wa Stars pamoja na benchi la ufundi Ikulu ambapo kwenye msafara huo mchezaji mwenzao, Peter Tino alikuwemo na kupewa Sh5 milioni na Rais, wachezaji wengine tisa walilalamika kutoalikwa ikiwemo kusaidiwa kama ilivyofanywa kwa mwenzao.

Advertisement