Samatta aongezewa adhabu na baba yake

Muktasari:

Mbwana Samatta amejikuta akiadhibiwa na baba yake mzazi baada ya kupaisha penalti Taifa Stars ikiibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Cape Verde jana Jumapili Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

BABA mzazi wa Mwanasoka wa kimataifa anayekipiga Genk ya Ubelgiji, Mbwana Samatta amekuja na adhabu kali dhidi ya mwanaye huyu pindi inapotokea anakosa penalti.
Mzee huyu anayejulikana kwa jina la Ally Samatta Pazi, amesema tatizo la mwanaye kukosa penalti halijaanza leo na awali alikuwa anawalipisha shilingi 5,000 lakini kwa sasa itakuwa 10,000.
Mzee huyo anaeleza kwamba adhabu hiyo sio kwa Mbwana pekee bali hata kwa kaka yake Mohamed Samatta anayekipiga Mbeya City,akikosea atatakiwa kulipa pesa hiyo.
"Nimewafundisha wakiwa wadogo, najua ubora wao na mapungufu na ndio maana niliwawekea adhabu itakayokuwa inawafanya wawe makini zaidi wanapofikia hatua ya kupiga penalti.
"Nimemshangaa sana Samatta kupiga penalti ovyo dhidi ya Cape Verde anamuona kipa anaruka ruka yeye anaenda kupiga juu, nilijisikia kuchukia kupita kiasi mpaka nikawa naona presha inapanda,"anasema.