Samatta ang’oa mashabiki 25,000

Sunday September 27 2020
samatta pic

KITENDO cha Aston Villa kumpa mkono wa kwakheri nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta kimeonekana kuwatibua mashabiki wengi wa soka la Tanzania ambao wameamua hasira zao kuzimalizia kwenye mtandao wa kijamii wa Instagram wa klabu hiyo.

Aston Villa inayoshiriki Ligi Kuu England, imepoteza zaidi ya wafuasi 25K (25,000) ndani ya saa 24 katika ukurasa wao wa mtandao wa Kijamii baada ya kumpa mkono wa kwaheri ambaye ameichezea klabu hiyo kwa miezi minane.

Awali Aston Villa ilijizolea zaidi ya wafuasi 300K (300,000) kutoka ukanda huu wa Afrika Mashariki kwenye ukurasa wao huo baada ya kumsajili mshambuliaji huyo wakati wa dirisha la usajili la Januari mwaka huu akitokea KRC Genk ya Ubelgiji.

Ukurasa wao kabla ya Samatta kuondoka ulikuwa na zaidi ya wafuasi 891K (891,000) lakini baada ya klabu hiyo kutokuwa na mipango tena na mshambuliaji huyo huku saa chache baadaye akitangazwa kutua Fenerbahce, watanzania nao wakaamua kusepa naye.

Takwimu hizo ni ndani ya saa 24 bado namba zao kwenye ukurasa wao wa mtandao wa Kijamii wa Instagram zinaendelea kushuka, wapo wanaotamani kuona timu hiyo ikishuka daraja huku wengine wakiwataka Fenerbahce kuwakaribisha ili kuwa maskani yao mapya.

Ukurasa wa Instagram wa Fenerbahce, umeanza kupokea wafuasi wapy kutoka ukanda huu wa Afrika Mashariki ambao wamekuwa wakichangia kwa lugha ya Kiswahili kila ambapo Samatta amekuwa akipostiwa.

Advertisement
Advertisement