Samatta ampigia simu baba yake kumwambia mazito

 BABA mzazi wa supastaa Mtanzania anayekipiga Genk ya Ubeligiji, Mbwana Samatta ameshukuru dua za Watanzania anazoamini ndizo zinazompaisha kijana wake kupata mafanikio katika kazi yake ya soka.

Mzee huyo anayejulikana kwa jina la Ally Pazi Samatta, alisema mwanae kuchukua kiatu cha mchezaji bora mwafrika, mfungaji bora si jambo dogo bali ni historia ya aina yake ambayo inawafungulia njia wengine.

Mbali na mafaniki hayo, alisema amepata taarifa nyingine mpya kwamba mwanaey anaweza kuibuka Mchezaji Bora wa Ligi Kuu ya Ubeligiji nje na kiatu cha ufungaji bora na cha Mwafrika bora ndani ya nchini hiyo.

Alisema juzi Ijumaa Samatta alimpigia simu, akimweleza namna ambavyo anahitaji kuipeperusha vyema bendera ya Tanzania na kuhakikisha haishii kucheza Genk bali kutaka kuendelea kupasua anga zaidi ya Ulaya.

“Aliniambia jinsi ambavyo anatamani kuipeperusha bendera ya Tanzania mbele ya wazungu na hilo nimeliona likitimia, jambo la pili ni mawakala ambao wanamfuata kumuuliza alizaliwa wapi na amewezaje kuwa na mafanikio makubwa kama hayo kwa mtu mweusi.

“Majibu anayowapa ni kwamba nendeni Tanzania kuna vipaji vikubwa kuliko yeye akiwaambia yeye amepita kibahati na sio fundi kama wanavyodhani, akiwasisitiza wakitaka mafundi watawapata nchini kwake, nimeona ni kitu kikubwa na cha tofauti anachokifanya, alipofikia ameelimika vya kutosha”alisema.

Aliweka wazi mambo matatu, anayomwambia mwanaye kila anapozungumza naye kwamba aiwakilishe Tanzania kwa uhalisia wake, akimtaka awe mfano wa kuigwa kwa nidhamu, utulivu na upendo dhidi ya wengine.

“Tanzania asilimia kubwa ni watu wenye upendo, utulivu na nidhamu, vitu hivyo akiwa navyo na akaipeperusha bendera ya nchi juu, basi naamini atakuwa anayafanya makubwa zaidi ya kuita watalii kuja kwetu kwa kuvutiwa na uwezo wake uwanjani utakaoambatana na tabia njema.

“Nimefurahi sana mpaka nikachinja jogoo kwa furaha, akija nitamchinjia mbuzi ale na wenzake na sio kwamba siwezi kumfanyia makubwa ila nataka aishi maisha ya uhalisia ya Mtanzania ambayo yatamfanya kuwa sawa na wengine sitaki ajione yupo tofauti na wenzake,” alisema.

Pia alisema amepigiwa simu na watu wa Baraza la Michezo Nchini ambao hakutaka kuwaweka wazi wakimpongeza kwa kijana wake kwamba analiwakilisha vyema taifa la Tanzania.

“Asante Watanzania kwa dau zao, namshukuru Mungu kwa kumnyoshea taa yake njema, naamini atafanikiwa kucheza Uingereza anakotaka kwani anajitambua na ni mtu ambaye hataki kuongea ongea hovyo zaidi ya kutenda,”.

Hakuficha kitu kinachomsikitisha kwamba “Nashangaa sana watu wengine wananiuliza kweli huyo ni mwanao, sijui hata wanaonaje na wengine wanaona si Mtanzania, Samatta ni Mtanzania ni zamu ya Tanzania kung’ara kwa mataifa ya Ulaya”alisema.