Samatta ajiweka sokoni Liverpool

Muktasari:

Samatta alicheza kwa kiwango bora mchezo wa awali na pacha wake Paul Onuachu, na alifunga bao kwa kichwa ambalo lililokataliwa kwa kutumia teknolojia ya usaidizi wa matukio uwanjani ‘VAR’. Alisema mchezaji hodari anaonekana katika mechi kubwa kama ya leo, hivyo kitendo cha Genk kuikabili Liverpool ni fursa kwake kujiweka sokoni.

Dar es Salaam. Nahodha wa timu ya taifa ‘Taifa Stars’, Mbwana Samatta amesema mchezo dhidi ya Liverpool utamuweka katika mazingira mazuri kwenye usajili wa majira ya kiangazi.

Leo usiku, Samatta ataiongoza KRC Genk ya Ubelgiji kucheza na Liverpool kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya katika Uwanja wa Anfield mjini Liverpool.

Samatta alisema mchezo huo utamsafishia njia ya kusajiliwa na klabu kubwa barani Ulaya kwa kuwa unahusisha Liverpool ambayo ni timu kubwa. “Tuliteleza mchezo wa kwanza tumefanyia kazi kasoro na vichwani mwetu tumesahau kama tulifungwa, tuna mawazo ya namna gani tunaweza kupata matokeo mazuri,” alisema.

Samatta alicheza kwa kiwango bora mchezo wa awali na pacha wake Paul Onuachu, na alifunga bao kwa kichwa ambalo lililokataliwa kwa kutumia teknolojia ya usaidizi wa matukio uwanjani ‘VAR’. Alisema mchezaji hodari anaonekana katika mechi kubwa kama ya leo, hivyo kitendo cha Genk kuikabili Liverpool ni fursa kwake kujiweka sokoni.

“Napenda kama mshambuliaji kuwa sehemu ya matokeo mazuri ya klabu yangu. Tutacheza katika moja ya viwanja vigumu, lakini tutashikamana kama timu bila ya kuhofia kuwa kwao, nyumbani,” alisema mchezaji huyo ambaye ni nahodha msaidizi wa KRC Genk.

Samatta (26), ndiye mshambuliaji tegemeo wa safu ya ushambuliaji ya KRC Genk ambapo katika michezo 13 ya Ligi Kuu Ubelgiji ameifungia mabao sita.

Katika moja ya mahojiano yake, Kocha wa KRC Genk, Felice Mazzu alisema wanaenda Anfield kwa lengo la kupambana na sio kufungwa kama ilivyokuwa katika mchezo uliopita. Mazzu ametua England akiwa na kikosi cha wachezaji 25 ambao ni Coucke, Vandevoordt, Leysen, De Norre, Borges, Dewaest, Uronen, Maehle, Lucumí, Cuesta, Screciu, Wouters, Heynen, Nygren, Hrosovsky, Piotrowski, Hagi, Berge, Ito, Samatta, Paintsil, Odey, Onuachu, Bongonda na Ndongala.

Msuva, Himid

Saimon Msuva ambaye anacheza soka la kulipwa Morocco katika klabu ya Difaa El Jadida, alisema anamwamini Samatta kutokana na uwezo wake wa kufunga mabao hivyo haitakuwa ajabu kuifunga Liverpool.

Himid Mao ambaye anaichezea Enppi alimtakia kila la heri Samatta katika mchezo wake wa nne msimu huu katika ligi hiyo kubwa zaidi Ulaya kwa ngazi ya klabu. “Kuifunga Liverpool itakuwa ni heshima kwake na kwa Watanzania,” alisema. Katika mchezo uliopita KR Genk ilifungwa mabao 4-1 na Liverpool nyumbani.