Samatta aanza na sare Uturuki

Derby ya Uturuki inayoikutanisha Galatasary na Fenerbahce anayochezea Mtanzania Mbwana Samatta imemalizika kwa sare ya kutokufungana.

 

Samatta aliingia dakika ya 66 akichukua nafasi ya Mame Thiam akiwa na jezi namba 10 mgongoni alionekana kusumbua mabeki wa timu pinzani licha ya kupata mpira mara chache.

 

Straika huyo amejiunga na timu Fenerbahce kwa mkopo wa mwaka wa mmoja akitokea Aston Villa ya Ligi Kuu ya England.

 

Samatta katika dakika alizocheza ameokoa mpira wa adhabu kwa kichwa uliokuwa ukienda langoni kwao na kutoa pasi ya shambulizi ambayo haikuzaa matunda.

 

Mechi hiyo iliyokuwa na ushindani mkubwa ilikuwa na mastaa wakubwa ambapo kwa upande wa Gala alikuwamo Arda Turan, Falcao, Ryan Babel, Younes Belhanda na  Sofiane Feghouli, wakati kwa timu ya Samatta, alikuwapo staa wa zamani wa West Ham na Everton, Mcolombia Enner Valencia na kiungo wa zamani wa Bayern Munich, Mbrazil Luiz Gustavo.