Samatta aaga Genk, anukia Aston Villa

Muktasari:

Tayari Samatta ameshapiga chini ofa za timu Mashariki ya kati ili akamilishe usajili wake wa kutua kunako ligi ya England.

Dodoma. Mshambuliaji KRC Genk, Mbwana Samatta wa KRC Genk anakaribia kutua Aston Villa ya England kwa mujibu wa taarifa kutoka Ubelgiji.

Mtandao wa Hln umeripoti klabu ya Aston Villa wamekaribia kumnasa mshambuliaji huyo nahodha wa Tanzania kwa dau la euro10 Milioni sawa na Paundi 8.54milioni.

Taarifa hizo zinaeleza Samatta amefanya mazoezi ya mwisho Genk kabla ya kuondoka wakati ambao timu hiyo inafahamu nyota wake huyo ataondoka kwenye dirisha dogo la usajili barani Ulaya.

Upande wa Aston Villa unatajwa kuhitaji huduma ya Samatta kutokana na mshambuliaji wake Mbrazil Wesley Moraes kuumia na atakosekana msimu mzima wa ligi.

Kocha wa Aston Villa, Dean Smith ameshabariki usajili wa Samatta kama mchezaji sahihi wa kuziba nafasi ya Moraes ikiwa pamoja na kwenda kuongeza ufanisi wa eneo la ushambuliaji ili kujinusuru kushuka daraja.

Kwa ujumla Samatta akiwa na Genk ameifungia timu hiyo jumla ya mabao 76, asisti 20 kwenye mechi 192 alizoichezea ikiwamo kuisaidia kubeba taji la Ligi Kuu Ubelgiji.