Samatta: Tunahitaji ushindi, lazima tushinde

Muktasari:

Samatta alisema kutokana na matokeo ya kwanza yamewapa morali wachezaji wote kupambana zaidi mchezo wa kesho na kushinda kwa kishondo.

NAHODHA wa  timu ya Taifa ya Tanzania'Taifa Stars', Mbwana Samatta amesema yeye na wachezaji wenzake wana morali kubwa kuelekea mchezo wa dhidi ya Burundi na anaamini watapata ushindi kwani watakuwa na sapoti kubwa ya Watanzania.
Taifa Stars itakuwa mwenyeji wa Burundi kesho Jumapili kwenye Uwanja wa Taifa ukiwa ni mchezo wa marudiano wa kuwania kufuzu Fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika Qatar mwaka 2022.
Samatta alisema kutokana na matokeo ya kwanza yamewapa morali wachezaji wote kupambana zaidi mchezo wa kesho na kushinda kwa kishondo.
"Kila mchezaji yuko tayari, morali iko juu sana kutokana na matokeo ya mechi ya kwanza na tunatarajia matokeo ya Jumapili  yatakuwa mazuri kwa sababu tunacheza nyumbani na tuna uhakika Watanzania wengi watajitokeza kutusapoti.
"Nguvu ambayo tutaionyesha pamoja kuanzia wachezaji, benchi la ufundi na mashabiki  na imani  matokeo yatakwa mazuri"alisema Samatta.
Hata hivyo Samatta amewataka Watanzania kuweka ushabiki wa klabu na mambo mengine pembeni na kila mmoja kuisapoti timu ya Taifa kwani timu hiyo ni ya kila Mtanzania.
"Wanaoweza  kuja uwanjani Jumapili  wafike  kwa wingi ili kuisapoti  timu yao na wasioweza  basi wakunjue moyo kwani hii ni timu ya Watanzania wote. Tuachane na ushabiki usio na faida kwani linapokuja suala la timu ya Taifa  ni suala la Kitaifa kila Mtanzania anawajibika linamuhusu moja kwa moja.