Samatta, Olunga ni mshikemshike leo Afcon

Thursday June 27 2019

 

Cairo, Misri. Mshambuliaji Mbwana Samatta wa Tanzania na Michael Olunga wa Kenya wataonyesha ubabe wakati miamba ya Afrika Mashariki watakapoisimamisha Misri kwa dakika 90 kwenye Uwanja wa 30 Juni, Cairo.

Timu hizo zinaingia katika mchezo huo wakiwa na kumbukumbu ya kufungwa katika mechi za kwanza kwa Tanzania chapwa 2-0 na Senegal kama ilivyokuwa kwa Kenya kwa Algeria.

Mechi hiyo itakuwa ni vita binafsi ya washambuliaji bora zaidi Afrika Mashariki kwa sasa Samatta na Olunga wanaotaka kuandika majina yao katika orodha ya wafungaji katika mashindano hayo.

Nyota hao wawili pamoja mshambuliaji wa Uganda, Emmanuel Okwi ndiyo wafumania nyavu hatari zaidi katika ukanda huu.

Nahodha wa Taifa Stars, Samatta anaamini mchezo huu ni lazima washinde.

“Mchezo wa kwanza tulikuwa na wasiwasi, tulishindwa kumiliki mpira tulikuwa kwenye wakati mgumu,” alisema na kuongeza kuwa. “Tumeyafanyia kazi matatizo hayo na tupo tayari kucheza dhidi ya Kenya,” alisema Samatta.

Advertisement

Olunga alisema anategemea mechi yenye ushindani mkubwa kwa sababu tunajua vizuri, lakini naamini Harambee Stars itapata ushindi.

“Tunahitaji pointi tatu,” alisema Olunga na kuongeza. “Najua itakuwa mechi ngumu, tunajua vizuri. Tutajaribu kurebisha makosa yetu ya mchezo wa kwanza.”

Mshambuliaji huyo alikuwa kama Samatta baada ya kukosa ushirikiano katika mchezo uliopita, lakini hajamlaumu yeyote kwa kukosa pasi katika mchezo huo.

“Ukiwa mshambuliaji unataka kufunga. Siwezi kumlaumu yeyote kwa jinsi tulivyocheza mechi ya kwanza. Tulipotezwa kila eneo ni matumaini yangu tutabadilika katika mchezo ujao.

Kenya wataendelea kumkosa beki wake Joash Onyango wakati Taifa Stars wanategemea kuanza na Farid Musa ambaye katika mchezo uliopita dhidi ya Senegal alionyesha kiwango cha juu baada ya kuingia mwishoni mwa kipindi cha kwanza.

Advertisement