Samatta, Msuva waifanya kitu mbaya Cape Verde

Muktasari:

Ushindi huo unaifanya Tanzania kuwa katika nafasi ya pili katika Kundi L na kufufua matumaini yake ya kusaka kufuzu kwa AFCON2019, Cameroon

Dar es Salaam. Mabao ya nahodha, Mbwana Samatta na Saimon Msuva yamefufua matumaini ya Taifa Stars kufuzu kwa fainali za Mataifa ya Afrika mwakani baada kuichapa Cape Verde 2-0 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Mshambuliaji Difaa Jadidi, Msuva alifunga bao la kwanza kwa Stars akimalizia vizuri krosi ndogo ya Samatta aliyewatoka mabeki wanne wa Cape Verde na kupiga krosi iliyomkuta mfungaji.

Samatta alifanya kile walichosubiri mashabiki wa Tanzania katika kipindi cha pili kwa kufunga bao la pili kwa shuti kali akiwa ndani ya 18, baada ya kupokea pasi ya Mudhathir Yahya.

Ushindi huo unaifanya Taifa Stars kupanda hadi nafasi ya pili ikiwa na pointi 5, wakati Uganda wakiongoza Kundi L kwa pointi 7, wakati Cape Verde ya tatu na pointi 4 na Lethoso ya mwisho ikiwa na pointi 2.

Katika mchezo huo kocha wa Stars, Emmanuel Amunike aliingia kwa mfumo wa 3-5-2, huku alifanya mabadiliko katika safu ya ulinzi na kiungo na kile kikosi kilichocheza jijini Praia wiki iliyopita na kuchapwa 3-0.

Katika mchezo wa kwanza mabeki walianza Agrey Morris, Abdi Banda na David Mwantika, Hassan Kessy na Gadiel Michael.

Lakini katika mchezo huu Amunike alibadili na kuwaanzisha Banda, Morris, Kelvin Yondani, Gadiel Michael na Shomari Kapombe.

Huku katika upande wa kiungo akimuongeza Erasto Nyoni akisaidiana na Himid Mao na Mudathir Yahya huku katika mchezo wa kwanza dhidi ya Cape Verde akiwaanzisha Mao na Mudathir.

Mabadiliko haya yalionyesha tija katika kikosi cha Stars ambapo dakika 21 Mudathir alipiga mpira mrefu ulioingia ndani ya eneo la 18, kukutana na Msuva, beki wa Cape Verde alimfanyia makosa na refa Souleiman Djama aliweka penalti.

Hata hivyo nafasi hiyo ilishindwa kutumiwa vizuri na nahodha wa Stars, Samatta kupiga penalti aina ya panenka iliyogonga mwamba.

Baada ya kukosa penalti hiyo Samatta alibadilika na dakika 29, alipokea pasi ya Erasto Nyoni na mshambuliaji huyo wa Genk aliwazidi kasi mabeki wa Cape Verde na kuingia ndani ya 18 kisha kupiga pasi na kumaliziwa vizuri na Msuva na kuifanya Stars kupata bao la kuongoza.

Licha ya Stars kuwa mbele kwa bao moja, Cape Verde ilikuwa wakionekana kusuka mipango dhabiti ya kusawazisha baada ya kufika mara kwa mara langoni mwa Stars, hata hivyo umakini wa Yondani na Morris ulioneka kuwa makini katika kuokoa.

Dakika 38, Stars ilifanya shambulizi la kushtukiza baada ya Kapombe kupiga krosi ndefu na kukutana na Samatta ambapo alikimbia na kupiga pasi fupi ndani ya dimba hata hivyo beki ya Cape Verde ilikuwa makini katika kuokoa.

Dakika 40 Cape Verde ilipata nafasi ambapo mshambuliaji Semedo Jorge alipiga shuti lilipoanguliwa na Manula na kuwa kona isiyokuwa na faida.

Kipindi cha pili Stars ilianza kwa kasi na kuongeza mashambulizi, ambapo dakika 52, John Bocco aliingia kuchukua nafasi ya Abdi Banda.

Mabadiliko hayo yalionyesha kabisa benchi la ufundi la Stars lilikuwa linataka mabao zaidi katika mchezo huo.

Dakika 57, Samatta alifungia bao la pili Stars baada ya kucheza pasi za haraka na Mudathir Yahya ambapo pasi ya mwisho Samatta aliipiga kwa Mudathir, lakini alirudishiwa tena na Samatta alipiga shuti moja kwa moja akiwa ndani ya boksi na kutinga wavuni.

 

Stars ilifanya mabadiliko dakika 58 na kumtia Mudathir Yahya na kuingia Feisal Salum kwenda kuongeza nguvu katika nafasi ya kiungo.

Mabadiliko katika safu ya kiungo kwa Stars kulionyesha tija kwani Feisal alikuwa na kazi ya kusambaza mipira huku Mao na Nyoni wakikaba kwa umakini.

Dakika 70, Stars lilifanya shambulio lingine baada ya Kapombe kupiga krosi ambayo mshambuliaji John Bocco alipiga kichwa, lakini kilipaa juu ya lango la Cape Verde.

Cape Verde bado waionekana kutafuta bao baada ya kufanya mabadiliko 78, kwa kumtoa Ricardo Gomes na kumuingiza mshambuliaji Ramos Heldon.