Samatta Msuva kuibeba timu Serengeti Boys, Liunda ataja yatakayojiri

Muktasari:

  • Timu zitakazoshiriki ni wenyeji Tanzania, Nigeria, Guinea, Morocco, Cameroon, Uganda, Angola na Senegal. Nusu ya timu hizo zitacheza Fainali za Kombe la Dunia kwa vijana wa U-17 zitakazofanyika baadaye Oktoba nchini Peru

Dar es Salaam. Siku 26 zimesalia kuanza kwa fainali za Mataifa ya Afrika kwa vijana (Afcon) ambazo zitafanyika kwa mara ya kwanza nchini.

Tayari fainali hizo zimetengewa kitita cha Sh 3.8 bilion kwa ajili ya kuyafanikisha.

Timu zitakazoshiriki ni wenyeji Tanzania, Nigeria, Guinea, Morocco, Cameroon, Uganda, Angola na Senegal. Nusu ya timu hizo zitacheza Fainali za Kombe la Dunia kwa vijana wa U-17 zitakazofanyika baadaye Oktoba nchini Peru.

Spoti Mikiki ilifanya mahojiano na Mtendaji Mkuu wa Kamati ya Maandalizi, mwamuzi wa zamani wa kimataifa ambaye kwa sasa ni Mkufunzi wa Waamuzi wa CAF, Leslie Liunda.

Swali: Tumeshasikia gharama za maandalizi hadi mashindano yanafikia Sh3.8bil, kikubwa ni suala la viwanja, hili limekaaje?

Liunda: Mashindano yatachezwa katika viwanja viwili tofauti, Uwanja wa Taifa na Azam Complex) pale Chamazi.

Uzuri tuko kwenye hatua nzuri ya ukarabati wake, kwa viwango ambavyo CAF imetaka.

Kwenye Uwanja wa Taifa, ukarabati unafanyika pale kwenye Jukwaa Kuu (VIP), vyumbani, vyoo na baadhi ya vyumba kuwekewa samani.

Uwanja wa Chamazi, ubao wa matokeo ulikuwa na hitilafu kidogo unabadilishwa, jukwaa kuu pia litapanuliwa zaidi, lakini pia chumba cha kupimia doping (matumizi ya dawa za kusisimua misuli) kitaandaliwa.

Swali: Hili la chumba cha doping CAF walitoa maelekezo gani?

Liunda: CAF walipokuja hawakusema chochote kuhusu chumba cha doping pale Chamazi, lakini daktari wetu, Marealle alipokiona alisema ni kidogo, hivyo tunafikiria tuwe na hema jingine kwa nje kwa ajili ya doping sanjari na chumba hicho.

Swali: Uwanja wa Taifa unafungwa baada ya mechi ya Taifa Stars Machi 24, vipi Uwanja wa Azam?

Liunda: Uwanja wa Azam utafungwa wiki tatu kabla ya kuanza fainali hizo, Aprili 14 wakati ule wa Taifa utatumika kwa mechi ya Taifa Stars na Uganda pekee kisha utafungwa hadi fainali hizo.

Swali: Mmejiandaa vipi kwa viwanja vya mazoezi?

Liunda: Tumetenga viwanja vitano kwa ajili ya mazoezi ya timu shiriki kwenye fainali hizi.

Uwanja wa JK Youth Park, Uhuru, Gymkhana, Uwanja wa Chamazi (upo pembeni ya uwanja wa mkubwa wa Chamazi) na uwanja wa shule ya kimataifa ya Hopac.

Swali: Nini kimekwamisha Uwanja wa Uhuru usitumike na una sifa zote?

Liunda: Awali ulikuwa kwenye orodha ya viwanja vitakavyotumika kwa ajili ya mechi lakini kuna hitilafu ambazo imelazimika kuondolewa.

Unajua CAF walipokagua waliridhia utumike, lakini wakashauri majukwaa yote yawekewe viti kama ilivyo kwa Uwanja wa Taifa.

Bahati mbaya hilo likawa changamoto. Hatuna fedha kwa ajili ya kufunga viti. Kiasi kilichopo ni kwa ajili ya ukarabati baada ya Taifa, fedha iliyobaki haikuwa ikitosheleza, hivyo tukaamua kukarabati kapeti la uwanja kwa kubadilisha na kuweka nyasi nyingine bandia.

 

Kama ni hivyo, kwanini mnaukarabati?

Liunda: Tumeuingiza kwenye prgramu. Umeingia kwenye orodha ya viwanja ambayo vitatumika kwa ajili ya mazoezi. Viwanja vya nyasi bandia sasa vya mazoezi vitakuwa viwili, ule wa JK Youth Park na Uwanja wa Uhuru.

Viwanja vya nyasi za asili kwa ajili ya mazoezi vitakuwa Gymkhana, Hopac na Chamazi ambao upo pembezoni ya uwanja mkubwa wa Azam Complex.

Swali: Kuna taarifa baadhi ya barabara zitafungwa, hili lina ukweli kiasi gani?

Liunda: CAF walihitaji kujua usalama wa eneo la viwanja yanakofanyika mashindano lakini utaratibu huo utategemea na mapendekezo ya maofisa wa CAF. (Awali Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo, Yusuph Singo aliiambia Spoti Mikiki baadhi ya barabara za kuingia na kutoka uwanja wa Taifa zitabadilishwa matumizi.

Swali: Baada ya ukarabati, maofisa wa CAF watafika lini kuona kinachoendelea ili kujiridhisha zaidi?

Liunda: Maofisa wa CAF watakuja Aprili Mosi. Miongoni mwa mambo watakayohitaji kujua usalama wa eneo hili hivyo watapata taarifa kutoka kwa IGP Sirro (Simon, Mkuu wa Jeshi la Polisi) na Mkuu wa Mkoa (Paul Makonda) ambaye ndiye mwenyekiti kamati ya miundo mbinu.

Swali: Chamazi kuna eneo lina shida kupitika, na siku ndio zinamalizika, imekaaje hii?

Liunda: Tulikuwa na changamoto ya kipande cha barabara kuingia Chamazi kuwa kibovu, lakini RC Makonda tumezungumza naye anasema liko chini yake na si jambo la kuumiza kichwa chake.

Tulikuwa na hofu ya barabara ya Kilwa kipindi cha mashindano ingekuwa kwenye ratiba ya ujenzi wa barabara ya Mwendo kasi, lakini Waziri Mkuu (Kassim Majaliwa) ametuhakikishia ujenzi utaanza baada ya mashindano.

Swali: Kuhusu hoteli zitakazofikia timu, mmejipanga vipi?

Liunda: Hili tumejipanga vizuri na kila timu zina maelekezo yake. Serengeti Boys na Morocco zitakuwa Ledger Plaza Bahari Beach, Nigeria na Senegal zimapengiwa Sea Scape.

Timu za Angola na Cameroon zenyewe zitakuwa Holiday Inn na Uganda na Guinea zimepangiwa kukaa Hoteli ya Peacock.

Swali: Waamuzi na wenyewe watakaa humo humo au kuna utaratibu wao?

Liunda: Hapana, hawawezi kukaa pamoja...waamuzi watakuwa Tiffany Diamond na viongozi watafikia Sea Cliff, tunatarajia kuwa na wageni 72 kutoka CAF ambao ni viongozi na wafanyakazi na waamuzi 24.

Swali: Kila mmoja ana taarifa za wapi watafikia?

Liunda: Timu zote zinafahamu hoteli watakazofikia na zinaweza kutuma watu wake kwa ajili ya kuangalia mazingira.

Swali: Kuna taarifa za wachezaji wetu maarufu kutumika kwenye hamasa ya vijana?

Liunda: Tuko katika mchakato wa kuwaita nyota wa Tanzania, wanaocheza soka la kulipwa nje ya nchi akiwamo Mbwana Samatta na Saimon Msuva. Unajua vijana wakiwaona watahamasika, na sisi tutawatumia kama kuwatia motisha.             

Swali: Mna taarifa CAF wanaleta wachezaji gani maarufu? 

Liunda: Siwezi kusema moja kwa moja lakini ninachofahamu watu wengi maarufu wa nje ya nchi wataalikwa na CAF ambayo yenyewe ndiyo itatueleza ni nani na nani watakuja, ila watakuwepo ingawa upande wetu tunafikiria kuwaita hao nyota wetu ambao wanacheza nje, tutaangalia Ligi zao kule, kama zitakuwa zimesimama tutawaomba waje, uwepo wao utawajengea hamasa vijana wetu.

Swali: Kiujumla, maandalizi ya Serengeti Boys yakoje?

Liunda: Maandalizi ya Serengeti Boys yako katika kiwango bora na haijawahi kutokea timu ikaandaliwa kama ilivyo kwa Serengeti Boys hii, licha ya kwamba hivi karibuni ilipoteza mechi zake mbili kwenye mashindano ya UEFA Assist.

Wengi tuliona ilifungwa na Guinea 1-0, ikashinda 3-2 na Australia na kufungwa 5-0 na wenyeji Uturuki.

Swali: Unadhani mashindano yale yameisaidia timu kwa kiasi gani?

Liunda: Tuliyatumia mashindano yale kwa ajili ya mazoezi, tumefungwa naweza kusema kwa sababu ya hali ya hewa ya kule kwa mchezaji aliyezaliwa na kukulia Dar es Salaam hawezi kustahimili baridi kali iliyopo kule, japo vijana walipambana na mechi ya pili kushinda.

Swali: Timu nne zitacheza Fainali za Kombe la Dunia kule Peru, Serengeti Boys inatakiwa kushinda mechi ngapi walau kujipa matumaini?

Liunda: Tunahitaji kushinda mechi mbili pekee kwenye Afcon ili kufuzu Fainali za Kombe la Dunia, hii ni nafasi adimu katika historia ya soka letu, Watanzania tuisapoti timu yetu ya Serengeti Boys ili ifike hatua hiyo.

Swali: Nafahamu yako mengi unataka kuzungumza, lakini kwa kumalizia, nini unataka kuwaambia Watanzania?

Liunda: Ninachowaomba Watanzania ni kujitokeza kwa wingi kuisapoti Serengeti Boys katika michezo yake yote itakayocheza kwenye Afcon ili iweze kufanya vizuri kwani shabiki ni mchezaji wa 12. Tuwape nguvu.