Samatta, Msuva kuibeba Stars

Muktasari:

Kiungo wa zamani wa Azam Himidi Mao anayecheza Petrojet ya Misri amefunga mabao mawili.

Oliver Albert,Mwananchi

Dar es Salaam. Wakati timu ya Taifa, ‘Taifa Stars’ ikijiandaa kuvaana na Uganda ‘The Cranes’, wachezaji wanaocheza soka ya nje ya nchi wana nafasi kubwa ya kuibeba katika mchezo huo wa Jumapili.

Timu hizo zitacheza mchezo wa kuwania kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na utachezeshwa na mwamuzi Eric Canstane kutoka Gabon.

Taifa Stars inatakiwa kushinda ili kujiweka katika mazingira mazuri ya kufuzu Fainali za Afcon huku ikiiombea Lesotho ifungwe au kutoka sare na Cape Verde.

Wachezaji wote 10 wanaocheza soka la kulipwa nje walioitwa na kocha Emmanuel Amunike wako kambini kujiandaa na mchezo huo.

Nahodha Mbwana Samatta na Simon Msuva wanapewa nafasi kubwa ya kuibeba Taifa Stars katika mchezo huo baada ya kuonyesha viwango bora katika ligi wanazocheza ugenini.

Samatta anayecheza KRC Genk ya Ubelgiji amefunga jumla ya mabao 29 katika mashindano yote Ulaya.

Mshambuliaji huyo amefunga mabao 20 katika Ligi Kuu Ubelgiji na tisa kwenye mashindano ya Europa.

Kwa upande wake Msuva amefunga mabao manane katika Ligi Kuu ya Morocco akitamba na klabu ya Difaa el Jadida.

Pia wachezaji hao ndio wameibeba Taifa Stars katika mechi za kufuzu Afcon katika hatua ya makundi, Samatta akifunga mabao mawili na Msuva moja na kuipa timu hiyo pointi tano ikiwa nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Kundi L wakati Uganda inaongoza kwa pointi 13, Lesotho pointi tano na Cape Verde nne.

Samatta alifunga mabao hayo katika mchezo ambao Taifa Stars iliifunga Lesotho bao 1-0 uliofanyika Juni 11,2017 Dar es Salaam kabla ya kufunga walipoichapa Cape Verde mabao 2-0 Oktoba 16, mwaka jana. Bao jingine lilifungwa na Msuva.

Mastaa wengine wanaotarajiwa kuibeba Taifa Satrs ni Shiza Kichuya anayecheza ENPPI ya Misri ingawa hajafunga bao kwa kuwa ana muda mfupi tangu alipojiunga na klabu hiyo.

Kiungo wa zamani wa Azam Himidi Mao anayecheza Petrojet ya Misri amefunga mabao mawili.

Thomas Ulimwengu aliyejiunga na JS Saoura ya Algeria ni mchezaji muhimu katika kikosi cha Taifa Stars kutokana na uzoefu wake katika mashindano ya kimataifa.Ulimwengu amewahi kucheza TP Mazembe ya DR Congo na El Hilal ya Sudan.

Pia yumo Farid Mussa anayecheza kikosi B katika CD Tenerife Hispania na Shabani Chilunda wa CD Izarra ya nchini humo.

Nyota wengine wanaotarajia kuongoza mashambulizi ya Taifa Stars ni Rashid Mandawa (BDF XI), Hassani Kessy (Nkana) na Yahya Zayd (Ismailia).

Uganda inawategemea Farouk Miya anayecheza Gonca ya Croatia na mwenye mabao mawili, Emmanuel Okwi (Simba) na Henry Kaddu wa KCCA. Pia ina kiungo mshambuliaji nyota chipukizi Allan Okello wa KCCA ambaye ana kiwango bora.

Amunike alisema anatarajia wachezaji wanaocheza soka la kulipwa nje ya nchi watakuwa chachu ya kuipa Taifa Stars matokeo mazuri Jumapili.

Mchezaji wa zamani wa Yanga, Sekilojo Chambua alisema wachezaji wanaocheza soka la kulipwa nje ya nchi wana mchango mkubwa Taifa Stars na anaamini wataibeba timu hiyo.

“Angalia Samatta na Msuva wameibeba timu hadi kufikia hatua hii. Hata mechi ya Jumapili naamini watafanya vizuri wakishirikiana na wachezaji wengine,”alisema Chambua, kiungo wa zamani wa kimataifa wa Taifa Stars.