Salim Aiyee Mama alifariki namuona - 2

Muktasari:

Simulizi yake ikakatishwa na kubadilisha mazingira ya stori mpaka alipotulia na kumudu kuendelea kuelezea mapito ya maisha yake.

KATIKA sehemu ya kwanza, straika wa KMC, Salim Aiyee, alisimulia jinsi alivyoshinda na njaa wakati akisaka kutoka katika soka. Endelea naye alivyomshuhudia mama yake mzazi akikata roho wakati akiwa mtoto mdogo.

“Nilipoingia ndani nikawakuta watu wanamfunika nikaita ‘mamaaa, mamaaa’ baadaye wakaniambia nikacheze, nikaja nikagundua kafariki dunia baada ya kumzika, hiki kitu kinaniuma mpaka kesho, natamani angekuwepo,” anasema.

Wakati anaendelea kusimulia alinyamaza kimya takribani dakika tano, huku uso wake ukiwa umejaa machozi, kwikwi zikisikika kisha akaanza kutetemeka kama mtu aliyeshikwa na baridi kali, kisha akaomba apewe maji ya kunywa.

Simulizi yake ikakatishwa na kubadilisha mazingira ya stori mpaka alipotulia na kumudu kuendelea kuelezea mapito ya maisha yake.

Anasema neno mama tangu 1998 kwake ni kama lilikoma zaidi ya mdomo wake kutamka mjomba, bibi, shangazi, baba na kaka, huku akidai akisikia wenzake wanalitamka kwa wazazi wao alikuwa anasikia roho inamuuma.

“Kuna wakati najitahidi kuonyesha tabasamu ambalo halipo moyoni, asikuambie mtu hakuna kama mama, kuna wakati mwingine na natamani ningemwambia baadhi ya vitu, kuna wakati natamani aone ninachofanya na nimpe chochote kitu ila ndio hivyo.

“Natamani kuita mama ila sina mama mkubwa wala mdogo, neno mama ndio najua umuhimu wake kwa sasa ila sina nafasi tena ya kulitamka, ingawa nawaita majirani na ndugu wa pembeni,” anasema.

BIBI YAKE AMTOA MACHOZI

Anasimulia akiwa mdogo alikuwa mtundu, ilikuwa akipigana na watoto wenzake, walikuwa wanakwenda kusemelea kwa mama zao, jambo ambalo bibi yake aliyemtaja kwa jina la Asha alikuwa hapendi kuliona.

“Mama zao walikuwa wakija nyumbani kunipiga, bibi alikuwa analia sana kisha ananikalisha chini ananiuliza wewe ukipigwa utakuwa unaenda kusemelea kwa nani wakati hauna mama?” Yalikuwa ni kati ya maswali ambayo yalinumiza sana.

“Dada angu na mdogo wangu wa mwisho walifariki dunia na kwa sasa tumebakia mimi na kaka niliyemfuata, yote ni maisha ninamshukuru Mungu.

“Nilikuwa najibu sina kwa kwenda kusemelea bibi, baadaye ilinifanya niwe mnyonge kujiona sina kimbilio halafu nikaona namuumiza sana bibi yangu, hivyo nilijikuta utundu ukiniisha na nilikuwa najiona thamani yangu ndogo kuliko wengine.”

ANA BABA YAKE

Pamoja na kwamba alikosa malezi ya mama yake aliyefariki dunia akiwa mdogo, anakiri baba yake mzazi yupo “Baba yangu kwa sasa yupo Mbeya, tulizaliwa wanne, dada yangu, kaka yangu mimi na mdogo wangu.

“Dada na kaka walizaliwa mkoani Mbeya, baadae baba akahamia kikazi Dar es Salaam, hivyo mama akawa amerudi Mheza ambako ndiko nikaja kuzaliwa mimi na mdogo wangu, akawa anakuja kututembelea tu na tukawa tumezoea kukaa Tanga, ila nawasiliana naye, ananishauri mambo mbalimbali.

“Hata kipaji cha soka nilichukua kwa baba yangu Aiyee ambaye alikuwa anacheza nafasi ninayocheza mimi ingawa yeye aliishia madaraja ya chini kwa maana hakuwahi kucheza Ligi Kuu,” anasema.

PESA YAKE NDEFU KUSHIKA

Aiyee alianza kuonja mkwanja mrefu, aliposajiliwa na Mwadui FC 2014/15, chini ya Kocha Jamhuri Kihwelo ‘Julio’, anaweka wazi dau alilopewa ni Sh1.5 milioni ambayo alinunua pikipiki na nyingine tofali.

“Nimecheza Mwadui FC, misimu mitano kwa kiasi kikubwa ndipo nilipoanzia kupatia mafanikio ya kimaisha, nimejenga na kunua kiwanja Muheza na sasa nataka kununua kingine Dar es Salaam.

“Pesa kubwa zaidi ambayo nimeipata kwenye soka ni hii ya timu yangu mpya ya KMC, bado nitaifanyia malengo ya maana pia nimekuwa nikisaidia ndugu zangu akiwemo bibi yangu Asha,” anasema.

ANAVYOONA NAFASI YAKE KMC

Hajajikweza kuona anaweza akajihakikishia namba kwenye kikosi cha kwanza, kinachonolewa na Kocha Mganda Jakson Mayanja, amekiri atakuwa na kazi ngumu kuhakikisha anaendeleza moto wake wa kufunga mabao.

Aiyee alikuwa ni miongoni mwa washambuliaji ambao walikuwa wanapigiwa hesabu ya kunyakua kiatu msimu ulioisha kabla ya Meddie Kagere wa Simba, kuwa kinara kwa kuzifuma nyavu mara 22.

ANAOGOPA SOKA LA ULAYA KISA NDEGE

Kama kuna vitu anaviogopa Aiyee ni kupanda ndege, anasimulia alikuwa haoni tabu na alikuwa anatamani kabla ya kupanda akiwa na KMC wakati wanakwenda kucheza na AS Kigali, Kombe la Shirikisho Afrika.

“Kitendo cha kupanda ndege tu, nilijikuta ndoto zangu za kutamani kucheza Ulaya kama zinayeyuka, niliomba Mungu kupita kiasi, nilikuwa nahisi nakufa, sijui kama ipo siku nitazoea,” anasema.

Alipoulizwa atafanye akijumuishwa kwenye kikosi cha Stars ikisafiri na ndege kwenda kucheza mbali? Alijibu huku akiwa amebanwa na kicheko “Hiyo siwezi kuogopa sana kwa sababu nakuwa najua ni safari ya mara moja moja sana.

“Kiukweli natamani kufika mbali lakini nikifikiria kuhusu kupanda ndege, najikuta nakosa pozi kabisa, yaani nakuwa nahisi kama kifo kipo mkononi, amani inakuwa haipo kabisa,” anasema.

JERRY TEGETE SABABU YA KUPENDA SOKA

Amemtaja mshambuliaji wa zamani wa Yanga, Jerry Tegete ndiye sababu ya yeye kucheza nafasi hiyo na kupenda soka, kitu kikubwa kilichokuwa kinamvutia namna alikuwa hodari wa kufunga.

“Nilikuwa naenda kuangalia mpira vibandani, nikirudi nachapwa na mjomba ambaye alijua nitapotea kimaisha, mchezaji ambaye alikuwa ananiamisha nitakuja kufika mbali ni Tegete.

“Mjomba yangu Athuman kwa sasa ndio ameanza kuamini kwamba nilikuwa namanisha kuja kuwa mfungaji ingawa bado ananitaka niwe makini nisiumie, nakumbuka wakati nipo Mwadui FC nimwambia Tegete namna nilivyokuwa namfuatilia alinipa moyo na nitafanya vitu zaidi yake,” anasema.

Ukiachana na Tegete ambaye alikuwa anamvutia, wachezaji wa Tanzania anaowapenda kwa sasa ni Mbwana Samatta anayetamani kufikia ama kupita mafanikio yake ingawa mtihani mkubwa upo kwenye kupanda ndege.

“Samatta ndiye mpango mzima ni mfano wa kuigwa katoka Lyon, kaenda Simba, TP Mazembe, Genk na sasa anaendelea kupasua anga, anachofanya ni kitu kikubwa, shida nikiwaza ndege akili inaniruka,” anasema.

NJE AMKUBALI RONALDO

Ukiacha wachezaji wa Tanzania, majuu anamkubali Cristiano Ronaldo anayekipiga klabu ya Juventus, aliyedai historia ya maisha yake, juhudi zinazompa mafanikio na kujitambua vitu alivyodai ndivyo vinavyomvutia.

“Unajua hata mtoto wake naona atakuja kuwa staa mkubwa anaonekana namna anavyomjengea misingi ya kuwa mchezaji mwenye vitu mguuni, yaani ni staa ambaye nampenda sana,” anasema.

CHAKULA ANACHOPENDA

Kwenye upande wa msosi humwambii kitu juu ya wali na kuku wa kienyeji ingawa anadai akiwa Dar es Salaam, anapenda kutumia samaki “Napenda sana kula wali kuku nikiwa Tanga, ila huku Dar natumia samaki,” anasema.