Salah atupia moja, aumia Liverpool hofu

Muktasari:

Salah tangu alipoumizwa bega na beki wa Real Madrid, Ramos bado hajapona vizuri na amekuwa akicheza huku akuwa amefunga bandeji bega lake

Cairo, Misri. Mshambuliaji Mohamed Salah alifunga bao kwa mpira wa kona uliokwenda moja kwa moja wavuni kabla ya kutolewa kwa kuumia Misri ikishinda mabao 4-1 dhidi ya eSwatini katika mchezo wa kusaka kufuzu kwa fainali za Mataifa ya Afrika 2019.
Mshambuliaji huyo wa Liverpool alifungia Misri bao la nne kwa mguu wa kushoto baada ya kupiga kona upande wa kulia na kuwafanya kwenda mapumziko wakiwa mbele kwa mabao 4-0.
Salah (26) bado hajafunga bao lolote katika mechi nne zilizopita za Liverpool, alitolewa uwanjani akiwa chini ya uangalizi wa madaktari baada ya kudondoka.
Mabao mengine ya Misri yalifungwa na Ahmed Elmohamady, Amr Warda na Mohamed 'Trezeguet' Hassan.
Wageni eSwatini ilipata bao la kufutia machozi kupitia Sibonginkhosi Gamedze zikiwa zimebaki dakika tano kabla ya mchezo kumalizika.
Matokeo hayo yanaifanya Misri kuongoza Kundi J sawa na Tunisia itakayocheza leo na Niger.
Kipigo hicho cha eSwatini ambayo zamani ilitambulika kama Swaziland inashika mkia ikiwa imecheza mechi tatu bila ya kushinda.
Matokeo ya mechi za jana za AFCON2019
Kundi B: Cameroon 1-0 Malawi
Kundi C: Gabon 3-0 Sudan Kusinu
Kundi D: Togo 1-1 Gambia
Kundi H: Guinea 2-0 Rwanda, Ivory Coast 4-0 Central African Republic
Kundi I: Angola 4-1 Mauritania
Kundi J: Misri 4-1 eSwatini
Kundi L: Cape Verde 3-0 Tanzania