Salah ashikilia matumaini ya Misri Afcon

Muktasari:

Salah ameichezea timu ya Taifa ya Misri jumla ya mechi 67 huku akiifungia mabao 41 na amepiga jumla ya pasi 22 za mwisho.

Nyota wa Liverpool, Mohamed Salah ataongoza kikosi cha wachezaji 19 wa Misri kilichoitwa kwa ajili ya mechi mbili za kuwania kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) mwakani kilichotangazwa jana na kocha  Hossam El-Badry.

Kocha El-Badry ameonekana kutoa kipaumbele kikubwa kwa wachezaji wanaocheza ligi ya nyumbani ambao amewaita 14 huku watano tu wanaocheza soka la kulipwa nje ya nchi hiyo wakipewa fursa ya kuunda kikosi hicho ambacho kitacheza dhidi ya Togo kati ya Novemba 9 hadi 17 mwaka huu.

Kiungo wa Arsenal, Mohamed Elneny ni staa mwingine ambaye kocha El-Badry amemjumuisha katika kikosi chake ambacho pia kitakuwa na winga wa Aston Villa, Mahmoud Hassan 'Trezeguet'.

Ukiondoa hao, wengine walioitwa kikosini ni beki Ahmed Hegazi ambaye hivi karibuni amesajiliwa na Ittihad Jeddah ya Saudi Arabia akitokea West Bromwich Albion ya England pamoja na mshambuliaji wa Olympiacos ya Ugiriki, Ahmed Hassan Kouka.

Timu ya Pyramids imeongoza kwa kutoa idadi kubwa ya wachezaji katika kikosi hicho ambapo jumla ya wachezaji nane wameitwa na kocha El-Badry wakitokea katika timu hiyo lakini pia klabu nyingine ambazo zimetoa wachezaji wake ni Zamalek, Al Ahly, ENPPI, El Gouna, Arab Contractors, Tala’a El Gaish  na Smouha.

Kikosi hicho cha wachezaji 19 wa Misri kinaundwa na El-Mahdy Soliman, Ramadan Sobhi, Abdallah El-Said, Ali Gabr, Ahmed Hegazi (Ittihad Jeddah), Ahmed Ayman Mansour, Mohamed Hamdy, Mohamed Farouk, Ahmed Tawfik (Pyramids FC), Mohamed Bassam (Tala’a El-Gaish),

Wengine ni Mohamed Salah (Liverpool) Mohamed Sherif (ENPPI), Mohamed Elneny (Arsenal), Hossam Hassan, Ahmed Aboul-Fotouh (Smouha), Ahmed Kouka (Olympiacos), Taher Mohamed (Arab Contractors), Akram Tawfik (El-Gouna) na Mahmoud Hassan 'Trezeguet' (Aston Villa).

Misri inashika nafasi ya tatu katika kundi G la kuwania kufuzu Fainali za Afcon 2021 ikiwa na pointi zake mbili ilizopata baada ya kucheza mechi mbili ikiwa nyuma ya Comoro inayoongoza na pointi zake nne, Kenya ikiwa nafasi ya pili na pointi mbili huku Togo ikishika mkia na pointi moja.