Sala ndio basi tena!

Muktasari:

Uhamisho wa staa huyo kutoka Nantes kwenda Cardiff ulitangazwa siku mbili kabla ya kupotea kwa ndege hiyo na Cardiff ilikuwa imekubali kulipa dau la Pauni 15 milioni ambayo ni rekodi ya uhamisho klabu hiyo kwa ajili ya kumnasa Sala ili aongeze makali katika safu yao ya ushambuliaji ambayo inasuasua kwa sasa.

LONDON, ENGLAND

SASA ni rasmi. Staa wa Argentina, Emiliano Sala ambaye alikuwa njiani kuhamia Klabu ya Cardiff City akitokea Nantes ya Ufaransa imethibitishwa amefariki dunia na juzi Alhamisi mwili wake uliopolewa kutoka katika ndege ndogo iliyoanguka katika Pwani za England.

Sala, 28, pamoja na rubani David Ibbotson walipotea na ndege hiyo tangu Jumatatu Januari 21 baada ya ndege yao kupoteza mwelekeo na kutoonekana katika rada na kwa muda mrefu ilikuwa haijulikani walipo.

Jumapili asubuhi ndege yao hatimaye ilionekana chini ya maji na Jumatano mwili ulionekana ukiwa umenasa katika ndege hiyo na baada ya uchunguzi juzi polisi usiku waliachia taarifa iliyoweka wazi mwili huo ni wa mwanasoka Emiliano Sala.

“Mwili ambao umeletwa Portland, Alhamisi Februari 7, 2019 umegundulika kuwa wa Mwanasoka wa kulipwa, Emiliano Sala. Familia za Mr Sala na rubani David Ibbotson zimeshapewa taarifa hizi na wataendelea kupewa sapoti na watu wetu. Fikra zetu zipo na wao katika nyakati hizi ngumu.” Ilisema taarifa hiyo ya polisi.

Uhamisho wa staa huyo kutoka Nantes kwenda Cardiff ulitangazwa siku mbili kabla ya kupotea kwa ndege hiyo na Cardiff ilikuwa imekubali kulipa dau la Pauni 15 milioni ambayo ni rekodi ya uhamisho klabu hiyo kwa ajili ya kumnasa Sala ili aongeze makali katika safu yao ya ushambuliaji ambayo inasuasua kwa sasa.

Staa huyo alipimwa afya katika mji wa Cardiff lakini akarudi Ufaransa kwa ajili ya kuwaaga wachezaji wenzake pamoja na wafanyakazi wa klabu yake ya Nantes ambao aliishi nao vema lakini wakati akirejea Cardiff kwa ajili ya kuanza maisha mapya ndege yake ilipotea.

Sala alitazamiwa kuichezea Cardiff mechi ya kwanza katikati ya wiki iliyopita katika pambano la ugenini dhidi ya Arsenal kabla ya kutazamiwa kucheza mechi ya kwanza nyumbani wikiendi iliyopita katika pambano dhidi ya Bournemouth.

Mechi zote hizo zilitumika katika kumkumbuka staa huyo lakini familia yake iligoma klabu zisivae vitambaa vyeusi kwa sababu kulikuwa hakuna taarifa rasmi kama staa huyo alikuwa amepoteza maisha yake. Lakini sasa timu zote zinatazamiwa kuvaa vitambaa vyeusi kabla ya mechi hiyo kwa vile taarifa ya msiba wake imethibitishwa rasmi.

Klabu ya Cardiff iliungana na mastaa mbalimbali kuandika taarifa ya maombelezo katika kurasa zake za mitandao ya kijamii ikisema “Tunatoa pole zetu kwa familia ya Emiliano. Yeye na David wataendelea kubakia katika mawazo yetu kwa maisha yetu yote.”

Dada yake Emiliano, Romina ambaye pamoja na Mama yake na kaka yake walisafiri kutoka Argentina mpaka Wales mara baada ya kupotea kwa ndege hiyo aliandika katika ukurasa wake wa Instagram na kuweka picha ya Sala akisema “Moyo wako katika moyo wangu utang’aa kwa maisha yote. Nakupenda sana Tito.”

Baadhi ya mastaa ambao walituma salamu zao za rambirambi mitandaoni ni pamoja na Mesut Ozil, Wayne Rooney, Jerome Boateng, Harry Maguire, Sergio Kun Aguero, Glen Johnson, Alexandre Lacazette, Benjamin Mendy, Kylian Mbappe, Sol Bamba wa Cardiff ambaye angecheza naye sambamba kama angefika salama, Riyad Mahrez na wengineo wengi.

Klabu mbalimbali pia ziliandika pole kwa msiba wa Sala. Klabu kama Barcelona, Tottenham, Independiente, na nyinginezo nazo ziliomboleza msiba wa staa huyo ambaye alikuwa anafungua ukurasa mpya wa maisha kwa kucheza Ligi Kuu England.