Sakata la Rio: Uhusika wa Keino, wawavuruga wadau wa riadha

Muktasari:

Keino, ambaye kwa sasa ni mjumbe wa heshima wa kamati ya kimataifa ya olimpiki (IOC), ameombwa kurejea nchini mara moja na kuripoti katika ofisi ya DCI, huku Wario ambaye yupo nchini Austria naye akitakiwa kufanya hivyo.

Nairobi, Kenya. Kufuatia uamuzi wa kumtaja aliyekuwa Mwenyekiti wa kamati ya Olimpiki nchini (NOCK), na mmoja wa magwiji wa Riadha nchini, Dr. Hezekiah Kipchoge Keino na sakata Sakata la Rio, umeibua maoni mchanganyiko miongoni mwa wadau wa michezo nchini, wengi wasiamini kilichotokea.
Kipchoge Keino pamoja na watu wengine sita akiwemo Waziri wa zamani wa michezo, Dr. Hassan Wario, wanatuhumiwa kuhusika katika sakata la Rio, lililohusisha matumizi mabaya ya Ksh55 milioni, zilizotengwa kwa ajili ya timu ya Kenya, kwenye michezo ya Olimpiki, iliyofanyika Jijini Rio de Janeiro, nchini Brazil, mwaka 2016.
Kwa mujibu wa taarifa ya Mkurugenzi wa Mashitaka ya Umma, Noordin Haji, watuhumiwa hao saba, walihusika katika unuzuzi wa tiketi za ndege ambazo hazikutumika, utoaji wa malipo hewa ya zaidi ya Ksh. 15 milioni kama posho, pamoja kuidhinisha malipo kwa watu hewa (zaidi ya Ksh. 6 milioni).
Baada ya Jaji Douglas Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) pamoja na ile ya Mkuu wa Upelelezi (DCI), kumtaka Keino pamoja na Wario ambaye kwa sasa ni Balozi wa Kenya nchini Austria, kujisalimisha kabla ya Alhamisi (kesho), wadau wa michezo wameibuka na kuhoji kukamatwa kwa Keino.
Baada ya Jaji wa Mahakama ya Ufisadi, Douglas Ogoti, kutoa amri ya kuwataka Keino na Wario kujisalimisha katika ofisi ya DCI kabla ya Alhamisi, Wadau wa michezo nchini walijitokeza na kutoa hisia zao kupitia mitandao ya kijamii n vyombo vya habari.
Walioonesha kughadhabishwa na tuhuma dhidi ya Keino ni, Mbunge wa eneo bunge la Soy, Caleb Kositany, ambaye aliwaambia waandishi wa habari katika maeneo ya Bunge kuwa, tuhuma zote dhidi ya Keino lazima yanapaswa kutupiliwa mbali, huku akisema yuko tayari kuendesha Harambee kwa ajili ya kukusanya fedha ambazo Keino anadaiwa kuhusika katika upotevu wake.
“Kama kuna kitu ambacho nina mashaka nayo ni hii ripoti ya Rio, huwezi kumhusisha mzee wetu na heshima zake katika ripoti yako kienyeji. Wakenya tumheshimu huyu Mzee, amefanya kazi kubwa ajili ya taifa letu, niko tayari, kushiriki mchango wa fedha hizo,” alisema Kositany
Mbali na Mbunge huyo, baada ya taarifa hizo kushika kasi kwenye mtandao wa kijamii, wakenya walijitokeza kuhoji uhalali wa ripoti hiyo pamoja na ushiriki wa Keino katika sakata hilo. Wengi walitumia mitandao hiyo, kuonesha hisia zao. Mmoja wao akiwa ni Waziri Mkuu wa zamani, Raila Odinga.