Sakata la Morrison bado linahitaji majibu

Ghafla filamu ya sakata la mchezaji Bernard Morrison limezikwa kimtindo kama ilivyo kawaida yetu. Mchezo umemalizika kirahisi na wala hakuna anayetaka kuuliza kwa undani.

Tuanzie hapa. Wakili Elias Mwanjala ambaye ni mwenyekiti wa Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji wakati akitoa hukumu ya sakata la mchezaji huyo mbali na kubaliki wakidai kuwa Morrison hakuwa na mkataba uliokidhi viwango, kuna mambo ambayo aliyaelekeza kwenye Kamati ya Maadili.

Mambo hayo yalikuwa haya ambayo Kamati ya Maadili chini ya mwenyekiti wake Kichele Waissaka imeyatolea ufafanuzi wiki iliyopita kwa kuchukuliwa hatua mjumbe wa Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji, Zacharia Hans Poppe baada ya kubainika kuongelea sakata hilo akiwa kama mjumbe wa kamati husika.

Pia kamati ya Waissaka ikawachukulia hatua wasemaji wawili - Hassan Bumbuli wa Yanga na Haji Manara wa Simba kwa makosa kama hayo ya Hans Poppe wakidaiwa kuliongelea sakata hilo hali ya kuwa lilikuwa katika ngazi ya hukumu.

Nilikuwa mmoja wa watu waliohudhuria mkutano wa Mwanjala akitoa hukumu ya shauri la Morrison na suala la kwanza kabla ya kesi za Hans Poppe, Bumbuli na Manara alitamka kwamba Morrison pia alikuwa na mashtaka aliyotakiwa kupelekwa katika Kamati ya Maadili ya Waissaka, baada ya kubainika kufanya kosa kwa kuingia mkataba na klabu anayoitumikia sasa ya Simba wakati akiwa ndani ya kesi ya msingi na klabu yake ya Yanga.

Mwanjala alienda mbali zaidi akisema Morrison alipoulizwa suala la kusaini mkataba alikiri kufanya hivyo na kwamba, hapo alifanya kosa kubwa la kutoiheshimu kamati na kwamba, hilo ni kosa la kimaadili na atapelekwa kwenye Kamati ya Maadili chini ya Waissaka kutafutiwa adhabu yake.

Bahati mbaya sana Waissaka alikuja wiki iliyopita, lakini shtaka la Morrison likikosekana katika hukumu zake na kuacha maswali juu ya suala hilo.

Hapa ndipo Mwanjala na Waissaka wanapoonekana kuacha maswali kwa kushindwa kulitolea ufafanuzi shauri husika.

Eneo hilo linapoleta ukakasi wa kwamba ipo michezo inafanyika katika kufukia mambo ya msingi na hali kama hii inazidi kuliletea shida ya kiafya soka letu.

Inakuwa haingii akili kwamba mhusika mkuu, Morrison, shtaka analotakiwa kulijibu na hata kuhukumiwa linakosa hitimisho na wahusika kuamua kukaa kimya.

Hatua mbaya zaidi inayoleta giza zito ni juu ya Kamati ya Maadili kujihami mapema kwamba hawatajibu swali la nje ya hukumu tatu walizotoa siku hiyo - kitu ambacho kinaashiria kuna mengi yamejificha ndani kwa hatua ya kufunika.

Shida kubwa ni kwamba haya yanafanyika mbele ya nyuso za wabobezi wa kisheria walioaminiwa kuongoza kamati hizi nzito za vyombo vya uamuzi wa juu wa soka.

Katika hali ya namna hii inatoa kabisa usafi kwamba, vyombo hivi vinaweza kusimamia haki na usawa kwa ‘kupepesa macho’ katika shauri hili na kutoa hukumu ambazo zinakosa kueleweka kwa watu ambao wanahitaji kuona mambo yalinyooka.

Naona bado mpira wetu utaendelea kupiga hatua, lakini kuna maeneo muhimu tunaanguka kwa kukosa weledi na hasa wasomi ndio wanaotuongoza katika vyombo hivi.

Ni ngumu kuamini Morrison anakosa kukamatwa na makosa ya kimaadili katika shauri hili kutokana na jinsi mwenendo mzima ulivyokuwa katika kesi ya kwanza.

Jambo naloamini ni kwamba sioni mwisho wa sarakasi za namna hii katika soka letu kwisha kwa kuwa wahusika hawatakuwa wanaogopa kabisa kufanya makosa ya namna hii.

Nimalizie kwa kusema kuwa kamati za kina Mwanjala na Waissaka bado imeacha maswali mazito katika sakata hili, na kwa hakika wapenzi na wadau wa soka wangali wanahitaji majibu husika ili kwenda sambamba na maendeleo ya soka la Tanzania. Asanteni.