Saka marufuku kuingia chumba cha wakubwa Arsenal

Muktasari:

Saka amecheza mechi tano kwenye kikosi cha Arsenal msimu huu, ikiwamo mechi tatu za Ligi Kuu England.

London, England. Nyota wa Arsenal, Bukayo Saka bado haruhusiwi kuingia kwenye vyumba vya kubadilishia vya kikosi cha wakubwa cha timu hiyo kwenye uwanja wa mazoezi.

Winga huyo kinda mwenye umri wa miaka 18, bado haruhusiwi kujiunga pamoja na wakubwa kwenye vyumba vya kubadilishia hivyo amekuwa akijiandaa kivyake huko kwenye maeneo mengine ya akademia.

Saka amecheza mechi tano kwenye kikosi cha Arsenal msimu huu, ikiwamo mechi tatu za Ligi Kuu England. Akionyesha kiwango bora na kutabiriwa kuwa staa mkubwa huko Emirates, akiwa amefunga pia kwenye mechi ya Europa League kuichapa Eintracht Frankfurt, akipiga pia asisti mbili, Saka bado anachukuliwa kama mtoto.

Alionyesha kiwango bora kwenye Kombe la Ligi, wakati Arsenal ilipoichapa Nottingham Forest 5-0, huku Saka akipewa nafasi pia kwenye mechi dhidi ya Aston Villa, Manchester United na Bournemouth.

Huko kwenye viwanja vya mazoezi, Arsenal imekuwa ikijiandaa tofauti, ikigawanywa ile timu ya wakubwa, akademia na makinda. Lakini, Saka, ambaye yupo kwenye mwendo mzuri huko kwenye kikosi cha Arsenal bado anaonekana kama mtoto licha ya kupandishwa kuichezea timu ya wakubwa.

Hata hivyo, jambo hilo halimpi shida Saka akisema anajisikia tu vizuri licha ya kuendelea kutumia vyumba vya akademia kwenye kujiandaa na mechi hata kama anafanya mazoezi na kikosi cha wakubwa.