Sajili nne zapiga jeki Express FC

Thursday September 3 2020

By HAMISI NGOWA

KUSAJILIWA kwa mashine wanne wapya za nguvu katika kikosi cha timu ya Express FC inayoshiriki katika Ligi ya Daraja la Kwanza Kaunti ya Mombasa kumeongeza ari kwa timu hiyo kufanya vyema msimu mpya wa Ligi utakapoanza.

Mkufunzi wa Klabu hiyo Emanuel Were anasema baada ya kuandikisha matokeo mabaya katika mechi za ligi msimu uliopita,timu hiyo sasa imeanza kujikusanya nakusajili majembe makali kwa maandalizi ya msimu ujao.

Anasema tayari  amenasa saini za wachezaji  wanne ambao anaimani kubwa wataisaidia katika kuandikisha matokeo bora  wakati ligi itapong’oa nanga baada ya janga la corona kuisha.

Were anasema wachezaji ambao wamekubali kuweka wino vidole vyao ili kutoa huduma zao kwa labu hiyo katika mechi za msimu ujao ni mshambuliaji matata, Zwere Salim kutoka Klabu ya Kishada FC.

Wengine ni Bakari Mambo,Katengo Hamisi na Elijah Aguko wanaotarajiwa kuongeza nguvu katika kikosi cha  kwanza cha timu hiyo wakati msimu utakapoanza.

Kocha huyo anawasifu wachezaji hao akisema wameonyesha makali yao katika baadhi ya mechi za kirafiki walizocheza hivi karibuni na kuwataka  wapinzani wao katika Ligi hiyo kujiandaa kwa kivumbi kikali.

Were anasema kando na vifaa hivyo 4,uongozi wa Klabu hiyo bado uko mbioni kutafuta wachezaji zaidi ili kuiweka Klabu hiyo katika nafasi nzuri ya kumaliza Ligi hiyo katika nafasi bora.

“Tumeanza  kujipanga mapema kwa kufanya usajili wa nguvu tukipania kutesa katika mechi za Ligi msimu ujao ili baada ya msimu kuisha tuweze kupanda ngazi na kushirikishi Ligi ya Mombasa Premier," akasema.

Advertisement