Saida Karoli asubiria huruma ya serikali

Muktasari:

Saida muimbaji mahiri wa muziki wa asili alitamba katika  miaka ya 2000 kupitia vibao vyake kama Chenkula Akatambala, Salome na Ukajuale

MUIMBAJI wa nyimbo za asilI nchini, Saida Karoli amesema anasubiri kwa hamu tamko la Serikali kurejesha shughuli za burudani ili aendeleze mipango yake ya kimuziki.

Saida alitamba na nyimbo nyingi kama Nkyalimuto(Bado mdogo) Orugambo(Neno), Kaisiki (Kasichana) Mwanyita ntakafile(mmeniua sijafa) na nyinginezo.

Akizungumza na Mwanaspoti Saida anasema, anasubiri burudani zirejee ili aweze kujipatia riziki kupitia shoo zake alizokuwa akizifanya kabla ya Serikali kusimamisha shughuli hizo kwa ajili ya kuzuia kuenea kwa virusi vya Corona.

Anasema baada ya Serikali kukaitisha shughuri za michezo na burudani aliamua kwenda nyumbani kwao Kagera kupumzika licha ya makazi yake kuwa Jijini Mwanza.

"Serikali imerejesha michezo bado sisi wa burudani hatujapata ruksa lakini nina imani na sisi siku sio nyingi tutaanza mapambano kama kawaida,” alisema Saida.

Anasema kwa sasa hawezi kufanya chochote kutokana na katazo hilo hivyo ameamua kukaa na familia yake na kuweka sawa akili yake ingawa amekiri kuyumba kwa sasa.   

"Mimi kazi yangu ni muziki sina kazi nyingine zaidi ya muziki, hivyo nina imani shughuli zikirejea nitaanza kupata shoo katika sehemu tofauti tofauti katika kumbi za starehe na hata kwenye maharusi," alisema mwanamuziki huyo.

Saida anasema  alikuwa katika wakati mgumu  baada ya waliokuwa wakimshika mkono marehemu Ruge Mutahaba wa Clouds na Reginald Mengi wa IPP kufariki Dunia.