Saha: Ole kakosea kumtosa Fernandez

Muktasari:

Kilichowafanya Man United kukwama kwenye dili la kumnasa Fernandez ni dau ambalo Sporting walitaka kulipwa, Pauni 70 milioni.

MANCHESTER, ENGLAND.FOWADI wa zamani wa Manchester United, Louis Saha amesema kocha Ole Gunnar Solskjaer amefanya makosa makubwa kwa kushindwa kumsajili kiungo Bruno Fernandes kwenye dirisha hili la majira ya kiangazi.

Fowadi huyo wa zamani wa Ufaransa, Saha alisema kitu ambacho Man United inakikosa kwenye kikosi chao msimu huu ni huduma ya kiungo huyo wa kimataifa wa Ureno, ambaye amekuwa na ubunifu mkubwa ndani ya uwanja.

Kocha Solskjaer alitajwa sana kwenye mpango wa kumsajili kiungo huyo karibu kwenye muda wote wa usajili wa majira ya kiangazi, lakini hadi dirisha linafungwa huko England, dili hilo lilishindwa kukamilika na Fernandez amebaki zake Sporting Lisborn.

"Bruno Fernandes ni mchezaji fundi sana, ambaye hakika angeweza kwenda kuunogesha mpira wa Man United," alisema Saha.

"Zaidi ya hicho, alizaliwa kuwa kiongozi na hicho ndicho kitu ambacho Man United inakosa msimu huu. Ni suala la muda tu, kila kitu kinajionyesha wazi, lakini ukweli Man United imefanya makosa makubwa kwa kushindwa kumsajili Bruno Fernandes au kushindwa kusajili kiungo mwingine mbunifu."

Kilichowafanya Man United kukwama kwenye dili la kumnasa Fernandez ni dau ambalo Sporting walitaka kulipwa, Pauni 70 milioni.

"Ninatia shaka, mchezaji mkubwa hata bei yake inakuwa kubwa, hivyo sio kitu kizuri kushindwa kununuliwa na timu kama Man United," alisema Saha.