Safari ya Simba ilianzia kwa JPM

Muktasari:

Katika hotuba yake kwa Simba, Rais Magufuli aliichana Simba baada ya kuishuhudia ikifungwa 1-0 na Kagera Sugar na kusema kama itaenda kwa mwendo huo haitafika kokote, huku akisisitiza kiu yake ni kuona timu hiyo inabeba taji la Afrika kwa mara ya kwanza.

SIMBA mwenda pole ndiye mla nyama na anayecheka mwishoni ndiye anayecheka sana baada ya Simba kuwaduwaza wengi.

Simba imefuzu hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kuinyoa AS Vita kwa mabao 2-1 na kumaliza ya pili ikiwa na pointi tisa kwenye Kundi D nyuma ya Al Ahly ya Misri yenye pointi 10 baada ya juzi Jumamosi nayo kuisambaratisha JS Saoura 3-0.

Kama hujui tu safari ya Wekundu hao wa Msimbazi ilianzia Mei 19 mwaka jana wakati wakikabidhiwa taji lao la Ubingwa wa Ligi Kuu Bara na Rais John Magufuli kutoa hotuba moja matata ambayo ni kama ilianzisha mwendo wa mafanikio kwa klabu hiyo katika michuano hiyo ya CAF.

Katika hotuba yake kwa Simba, Rais Magufuli aliichana Simba baada ya kuishuhudia ikifungwa 1-0 na Kagera Sugar na kusema kama itaenda kwa mwendo huo haitafika kokote, huku akisisitiza kiu yake ni kuona timu hiyo inabeba taji la Afrika kwa mara ya kwanza.

Kauli ya Rais ni kama iliwachochea Simba ambao waliachana na Kocha Pierre Lechantre na kumpa kazi Patrick Aussems kutoka Ubelgiji ambaye amefanya maajabu katika safari yao ya Ligi ya Mabingwa msimu huu. Kivipi endelea nayo...!

MZUKA MWINGI

Baada ya Shirikisho la soka Afrika (CAF) kubadilisha ratiba ya mashindano hayo kuwa hayataanza tena Februari kama ilivyo katika miaka ya nyuma bali yataanzia Novemba kwa zile timu ambazo zitaanzia katika hatua ya awali.

Novemba 18, mwaka jana Simba ilianza kazi katika Ligi ya Mabingwa katika hatua ya awali ikiwafunga Mbabane Swallows mabao 4-1, katika uwanja wa Taifa mabao ambayo yalifungwa na John Bocco mawili na Meddie Kagere na Clatous Chama.

Baada ya hapo Mnyama mkali mwituni Simba aliendeleza mawindo yake baada ya kwenda kurudiana na Mbabane Swallows na huku huku Eswatin waliuwasha moto wa maana kwa kuwafunga mabao 4-0, wenyeji na kuwandoa kwa jumla ya mabao 8-1.

Mabao ya Simba katika mechi hiyo iliyochezwa Desemba 4, yalifungwa na Chama mawili, huku Kagere na Emmanuel Okwi kila mmoja alifunga bao moja.

Katika mechi hizo za raundi ya awali Simba ilionekana wanaweza kuzuiliwa na timu hiyo kutokana iliweza kuindoa Azam Kombe la Shirikisho Afrika 2017, lakini mambo yalikuwa mepesi kwao. Ikavuka.

MASHETANI WEKUNDU

Baada ya kuvuka kizingiti cha WaeSwatini, Simba ilikutana na Nkana Red Devils ya Zambia na mechi ya kwanza ilichezwa nchini Zambia ambapo Wakundu wa Msimbazi walikubali kulala kwa mabao 2-1 bao lao likifungwa na John Bocco kwa mkwaju wa penalti.

Kutokana na motokeo hayo baadhi ya mashabiki wa soka nchini walibeza kuwa Simba hawataweza kupindua matokeo na mwisho wao wa kucheza mashindano hayo makubwa Afrika kwa ngazi ya klabu utakuwa hapo.

Desemba 24, Simba iliweka historia baada ya kuwafunga mabao 3-1, Nkana na kupindua matokeo ya mechi ya kwanza ambapo Mnyama alifuzu na kwenda kucheza hatua ya makundi, katika mchezo huu mabao ya Simba yalifungwa na Jonas Mkude, Kagere na lile la kuivusha lilifungwa na Chama katika Uwanja wa Taifa.

Rekodi waliyoiweka Simba ni kucheza hatua ya makundi ambayo mara ya mwisho timu kutoka hapa nchini kucheza hatua hiyo ilikuwa Simba mwaka 2003.

KUNDI LA KIFO

Baada ya sherehe na tambo nyingi baada ya timu yao kufuzu katika hatua hiyo ya makundi ambayo ndio yalikuwa malengo yao, CAF walifanya droo ya mashindano hayo na kuipeleka Simba kundi D ambapo iliangukia katika timu ngumu.

Simba iliangukia katika kundi hilo ikipangwa na Al Ahly waliotoka kucheza fainali ya msimu uliopita, AS Vita iliocheza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu uliopita na JS Saoura ambao ilikuwa ni miongoni mwa timu inayofanya vizuri licha ya kuanzishwa mwaka 2008.

Hapo ndio waliibuka mashabiki wengine wakiamini Mnyama safari yake ilikuwa imefikia mwishoni, kwani hataweza kupenya kutoka na hao vigogo ambao atacheza nao.

Kutokana na kundi hilo lilivyokuwa ilifikia Simba itadharauliwa na kuitwa (Underdog) jambo ambalo kwa hesabu za historia za timu ambazo alikuwa nazo katika kundi ilikuwa si vigumu kuamini hilo.

Mnyama Simba alianza harakati zake za kusaka pointi Januari 12, alipocheza na JS Saoura ambao waliweza kuwafunga mabao 3-0, ambayo yalifungwa na Kagere mawili na Okwi ambaye katika mchezo huu alikuwa katika kiwango bora.

AIBU MFULULIZO

Ushindi huo wa kishindo uliwainua mashabiki wa Simba kuona timu yao inaweza kufika mbali katika mashindano hayo ambayo hawakushiriki zaidi ya miaka mitano.

Lakini bwana wee ikakumbana na aibu kubwa ugenini kwani ilikwenda DR Congo katika mji wa Kinshasa ambapo ilikutana na dhahama ya mabao kutoka kwa AS Vita ambao iliwafunga mabao 5-0.

Mechi ya AS Vita na Simba ilichezwa Januari 19 kwa mabao yaliyofungwa na Botuli Bompunga, Juan Makusu aliyefunga mawili, Fabrice Ngoma na Makwekwe Kupa. Kipigo hiko kiliwainua mashabiki ambao wapo tofauti na Simba hasa watani wao wa Jadi Yanga kwa kutoa maneno ya utani haswa katika vijiwe vya soka na kuamini kuwaeleza kuwa timu yao haitaweza kwenda kokote.

Simba ilizidi kuvurugwa baada ya kwenda kuchezea tena kipigo cha maana Misri kutoka kwa Al Ahly ambao iliwalaza kwa mabao 5-0, ambayo ni wazi ilikuwa kama yanafunika matumaini ya timu hiyo kuendelea kucheza hatua inayofuata.

WABADILISHA KIBAO

Wachezaji, benchi la ufundi, viongozi na hata mashabiki wa timu hiyo walikuwa kimywa wakiwaacha mashabiki wa timu pinzani kuendelea kutamba baada ya kula tano kwa mara ya pili mfululizo.

Baada ya vipigo hivyo viwili ugenini vya jumla ya mabao kumi, Simba alirudi nyumbani kucheza na Al Ahly Februari 12, ambapo iliweza kuondoka na ushindi baada ya kuwafunga bao 1-0 ambalo lilifungwa na Kagere ambaye alifikisha jumla ya mabao sita katika mashindano hayo.

Ushindi huo uliufanya Simba kufikisha pointi sita ambazo ziliinua nguvu na morali ya kuamini kuwa wana nafasi ya kusonga mbele katika hatua inayofata na hata pale walipokuwa wanabezwa na mashabiki pinzani na wao walikuwa wanacho cha kuwajibu.