Safari ya Hawa wa Diamond India yaishia Kipawa

Muktasari:

Msanii Hawa Said aliyekuwa aondoke leo kwenda nchini India kwa ajili ya matibabu amejikuta akishindwa kufanya hivyo baada ya kutokuwa na kibali cha daktari.

Dar es Salaam. Msanii Hawa Said maarufu Hawa wa Diamond ameshindwa kusafiri kwenda India kwa matibabu baada ya kurudishwa akiwa ndani ya uwanja wa ndege Julius Nyerere kutotimiza vibali vya kusafiri vya kimatibabu.

Akizungumza na MCL Digital, Meneja wa mwanamuziki Diamond aliyegharamia matibabu hayo, Babu Tale amesema wamezuiliwa wakiwa tayari wameingia ndani ya uwanja wa ndege wa Julius Nyerere na kuanza kukaguliwa nyaraka zao mbalimbali.

Babu Tale amesema nyaraka iliyosababisha kutoruhusiwa kusafiri ni ya kutoka kwa daktari ya kuelezea hali ya mgonjwa ili wahudumu ndani ya ndege wajue watamuhudumiaje katika safari nzima.

"Kuna mgonjwa anaweza akawa katika hali ya kuzimia, kutapika ambapo anatakiwa ahudumiwe kitofauti, hivyo Hawa imeshindikana kwa kuwa hakuna hizo nyaraka inayoonyesha hivyo kutoka kwa daktari na wametuambia turudi mpaka hapo itakapokamilika," amesema Tale.

Hawa, Babu Tale pamoja na mama yake ilikiwa waondoke leo sa 11:00 na ndege ya Shirika la Emirates.

Hawa na mama yake Ndagina Hassan walifika uwanjani hapo tangu saa saba mchana huku Babu Tale yeye aliwasili saa tisa.

MCL Digital iliyokuwa imepiga kambi wakati wote hapo ilifanikiwa kuzungumza na mama wa Hawa aliyeelezea furaha yake ya Hawa kupata msaada wa matibabu hayo.

Wakati Hawa ambaye hakuwa tayari kuzungumza mengi aliwaomba watanzania kumuombea dua katika matibabu hayo.

Awali Babu Tale alisema walitarajia kuwa nchini humo kwa wiki mbili na huenda Hawa akapandikizwa ini kama madaktari watashauri hivyo.

Alisema wamelazimika kumsaidia Hawa baada ya kuona hali yake kwenye vyombo vya habari na kuongeza kwamba watanzania wanapaswa kuwaunga mkono katika hilo kwani msanii huyo bado anahitaji matibabu na huduma nyingine zaidi.

"Kama mlivyoona hali ya Hawa sio ya kusema atapona mara moja anahitaji msaada wa watanzania wengi zaidi, sisi tumeanza basi na wengine wanaweza kujitolea kwa chochote kitu ili aweze kupona," amesema Babu Tale.

Hawa aliyewahi kutamba na wimbo wa 'Nitarejea' aliomshirikisha Diamond, ana zaidi ya mwezi sasa anasumbuliwa na ugonjwa wa kujaa maji tumboni kulikosababishwa na tatizo la ini.

Kutokana na ugonjwa huo ameshalazwa katika hospitali ya Taifa ya muhimbili zaidi ya mara nne na kutolewa maji tumboni ambao kuna wakati alikuwa akitolewa hadi lita nne.