Safari ya Gor Mahia hadi robo fainali

Muktasari:

  • Hii ni baada ya Gor kumaliza nafasi ya pili kwenye kundi D kwa pointi tisa sawia na Zamalek ya Misri waliomaliza na idadi bora ya mabao. Ni pointi tisa ambazo Gor ilizoa nyumbani tu wakipoteza zote nyumbani.

KWA mara ya kwanza chini ya muundo mpya wa Kombe la Shirikisho, mabingwa mara 17 wa Ligi Kuu Kenya, Gor Mahia wamefuzu robo fainali ya mashindano haya na kujihakikisha kitita cha Kshs38 milioni.

Hii ni baada ya Gor kumaliza nafasi ya pili kwenye kundi D kwa pointi tisa sawia na Zamalek ya Misri waliomaliza na idadi bora ya mabao. Ni pointi tisa ambazo Gor ilizoa nyumbani tu wakipoteza zote nyumbani.

Hivi cheki safari yao ilivyoanza.

MWAKA 2018

Baada ya kuwahi ubingwa wa Kenya wa mwaka 2017, Kogalo waliwahi tiketi ya kuwakilisha Kenya kwenye michuano ya klabu bingwa wakipangwa na Leones Vegetarionos ya Equatorial Guinea raundi ya kwanza wakiwaondoa 2-0 kwa mabao ya ugenini na kumenyana na Esperance ya Tunisia raundi ya pili.

Hapa walitoka sare tasa nyumbani na kufungwa bao 1-0 ugenini na kuteremshwa michuano ya Shirikisho.

Kwenye mechi ya kufuzu makundi, walipangwa dhidi ya SuperSport United ya Afrika Kusini wakiilaza 1-0 ugani Machakos kabla ya kupoteza 2-1 mechi ya mkondo wa pili kule Sauzi ila wakafuzu makundi kwa sheria ya mabao ya ugenini (2-2).

Walipangwa kundi D pamoja na Yanga ya Tanzania, Rayon Sports ya Rwanda na USM Alger ya Algeria.

Katika mechi za nyumbani, Gor iliandikisha ushindi wa 4-0 dhidi ya Yanga, 0-0 na USM Alger na kupigwa 2-1 na Rayon Sports mechi ya mwisho ya nyumbani na ni hii iliwaondoa hesabu kwani walisafiri nchini Algeria na kupoteza 2-1 kwa USM huku Rayon Sports ikitoa sare tasa dhidi ya Yanga na kufuzu kama nambari mbili nyuma ya USM.

MWAKA 2018/19

Shirikisho la soka barani (CAF) liliamuru ligi zote za barani ziwe zikianza Julai hadi Mei sawia na mashindano yao hili likibadili kalenda yao pia na michuano ya mwaka huu ilianza Novemba mwaka jana ikitarajiwa kutamatika mwezi Juni.

Ndio hapa Gor, mabingwa wa msimu jana ligi kuu ya KPL, waliwahi nafasi nyingine ya kuwakilisha taifa michuano ya klabu bingwa.

Katika raundi ya kwanza, waliwalaza Nyasa Big Bullets ya Malawi raundi ya kwanza kupitia matuta kabla ya kuondolewa na Lobi Stars ya Nigeria kwa mabao ya ugenini 3-3.

Gor ilikuwa imeandikisha ushindi wa 3-1 nyumbani lakini kichapo cha 2-0 ugenini kiliwateremsha hadi michuano ya mashirikisho walipopangwa dhidi ya New Stars de Douala ya Cameroon wakiwaondoa 2-1, ushindi waliosajili nyumbani na kutoka sare tasa ugenini. Hapa ndipo walifuzu makundi wakijipata na Zamalek, Hussein Dey ya Algeria na Petro Atletico ya Angola.

MAFUNZO

Hapa, walihakikisha wanazoa alama zote tatu nyumbani wakianza na ushindi wa 4-2 baina ya Zamalek mwezi Februari, kisha wakawanyuka Hussein Dey 2-0 hiyo jana Petro 1-0 na kufuzu. Ugenini, walipoteza mechi zote dhidi ya Petro (2-1), Hussein Dey (1-0) na Zamalek (4-0).

“Mwaka jana, tulijifunza kwamba mechi za nyumbani ni muhimu sana kwenye mashindano haya ndiposa mwaka huu tuliamua nyumbani lazima afe mtu kisha tusubiri hesabu itakuaje kwenye kundi,” beki wa Gor Phillemon Otieno alifichua.

“Mfano mwaka jana sare ya USM Alger na kichapo cha Rayon Sports kilituharibia hesabu za kufuzu na umeona mwaka huu jinsi tulijikakamua tukawahi,” akaongeza.

WACHEZAJI NYOTA

Straika matata Jacques Tuyisenge naye alisema siri imekuWa mashabiki wa nyumbani kuwashangilia kila dakika.

“Ukienda mechi za ugenini, unapata tunacheza na timu zenye wafuasi wengi nyumbani, ni kitu ambacho tulisihi mashabiki wetu kujitokeza maana hiyo kelele huwatoa hesabu wapinzani na kutufaidi na tunawashukuru sana mwaka huu, sasa tumefuzu robo fainali tunawaomba wazidi kujitokeza kwa wingi kuliko hata juzi usiku,” Mrwanda huyo, ambaye amefunga mabao manne kwenye michuano hii alisema.

Kando na Tuyisenge, Gor pia itawashukuru mabeki Harun Shakava na Charles Momanyi, Philemon Otieno kisha Mganda Shaffik Batambuze pamoja na kiungo mbunifu Francis Kahata kama waliochangia pakubwa safari hii yao bila kumsahau golikipa mchanga Peter Fredrick Odhiambo.

Kwa kocha Hassan Oktay, anasubiria droo ya hapo kesho tu kupiga hesabu jinsi atafika fainali.

“Kila mchezaji anajituma na tunacheza vizuri, sioni kitakachotuzuia kufika fainali ya michuano hii na sapoti ya kila mtu,” Oktay, 42, alisema.

Kwenye mechi kumi na moja, Oktay ameshinda tano, kupoteza tano na kutoa sare moja.

Safari ya Gor haijaanza mwaka huu bali mwaka jana na kulingana na wadau wengi, wakiendelea hivi kila msimu basi watakuwa mojawapo wa timu bora barani kwani sasa kila Mkenya amefurahia hatua waliyopiga.

“Cha msingi waanze kujifunza kuzoa pointi ugenini na kila kitu kitakua rahisi sana,” mwanahabari wa michezo Stephen Mukangai.