Safari ya Elias Maguli kutua Rwanda imeiva

Muktasari:

  • Maguli ambaye amewahi kuichezea Dhofar SC ya Oman, Ruvu Shooting ya Pwani, Stand United ya Shinyanga na Simba SC ya Dar es Salaam, alijiunga na AS Kigali, Julai 26 kwa kusaini mkataba wa miaka miwili.

STRAIKA wa AS Kigali ya Rwanda, Elias Maguli amedai yuko kwenye mazoezi makali ili kuwa fiti kabla ya kujiunga na wachezaji wenzake kwa ajili ya kujiandaa na msimu mpya wa Ligi Kuu Rwanda.

Maguli ambaye amewahi kuichezea Dhofar SC ya Oman, Ruvu Shooting ya Pwani, Stand United ya Shinyanga na Simba SC ya Dar es Salaam, alijiunga na AS Kigali, Julai 26 kwa kusaini mkataba wa miaka miwili.

“Bado sijatumiwa tiketi ya kwenda Rwanda, lakini nipo kwenye maandalizi binafsi ili niwe fiti kwa ajili ya kuuanza msimu mpya wa ligi. Sijajua lini nitatumiwa lini.

“Maelekezo niliyonayo ligi itaanza mwezi ujao kwa hiyo muda wowote naweza kutumiwa tiketi hiyo,” alisema mshambuliaji huyo ambaye mara ya mwisho kuichezea Taifa Stars ilikuwa kwenye mashindano ya Cosafa. Mazoezi hayo ambayo amekuwa akiyafanya Maguli ni pamoja na kukimbia umbali mrefu ili kusaka pumzi, gym na mazoezi mbalimbali ya ufungaji mabao. Nyota huyo alisema anashauku ya kukutana na kocha wake mpya pamoja na kushirikiana na wachezaji wenzake kwenye kikosi hicho.