Sadio Mane kukosekana mwanzo wa Ligi England

Muktasari:

Liverpool imesharudi katika mazoezi ya msimu mpya na juzi ilicheza pambano jingine la kirafiki dhidi ya Sevilla. Hata hivyo, imeendelea kuwakosa baadhi ya mastaa wake wakubwa kama vile, Roberto Firmino, Alisson na Mohamed Salah.

LIVERPOOL, ENGLAND.MAMBO ni mengi muda ni mchache. Ndivyo ilivyo kwa staa wa Liverpool, Sadio Mane. Anaelekea kukosa mechi tatu za mwanzo za Liverpool mwanzo wa msimu ujao baada ya majukumu ya muda mrefu na Senegal.

Mane aliiongoza Senegal kufika fainali yake ya pili katika historia pale Misri na walipoteza dhidi ya Algeria 1-0 na kutokana na Senegal kufika mbali katika michuano hiyo Mane amejikuta hana muda wa kutosha wa maandalizi na wenzake.

Kwa kuanzia Mane atalikosa pambano la Ngao ya Jamii maarufu kama Community Shield dhidi ya wapinzani wao wa karibu katika soka la Kiingereza kwa sasa Manchester City. Pambano hilo linalokutanisha bingwa wa FA dhidi ya bingwa wa Ligi kuu litachezwa Uwanja wa Wembley Jumapili Agosti 4.

Liverpool itacheza pambano hilo kutokana na kushika nafasi ya pili katika Ligi Kuu ya England msimu uliopita baada ya Manchester City kuzoa mataji yote mawili msimu uliopita. Liverpool itacheza ikiwakilisha upande wa Ligi Kuu.

Baada ya kulikosa pambano hilo, Mane anatazamiwa kulikosa pambano la kwanza la ufunguzi wa Ligi Kuu dhidi ya Norwich iliyopanda daraja msimu huu. Pambano hilo la kwanza litachezwa siku ya Ijumaa Agosti 9 katika Uwanja wa Anfield.

Lakini pia kuna wasiwasi staa huyo wa zamani wa Southampton akalikosa pambano la Super Cup dhidi ya Chelsea Agosti 14. Pambano hilo hukutanisha bingwa wa Ulaya dhidi ya bingwa wa michuano ya Europa kwa ajili ya ufunguzi wa michuano mbalimbali mikubwa ya Ulaya.

Liverpool imesharudi katika mazoezi ya msimu mpya na juzi ilicheza pambano jingine la kirafiki dhidi ya Sevilla. Hata hivyo, imeendelea kuwakosa baadhi ya mastaa wake wakubwa kama vile, Roberto Firmino, Alisson na Mohamed Salah.

Wakati Firmino na Alisson walikuwa katika kikosi cha Brazil kilichofika fainali ya michuano ya Mataifa ya Amerika Kusini, Copa Amerika na kutwaa taji hilo dhidi ya Peru, Salah alikuwepo katika kikosi cha Misri kilichotolewa katika hatua ya mtoano na Afrika Kusini katika michuano ya Mataifa ya Afrika.

Wote hao wapo katika likizo ingawa watarudi mapema kabla ya Mane ambaye alicheza kwa muda mrefu zaidi huku akiendelea kuwa na kikosi cha Senegal wakati Liverpool ikiwa imeshaanza maandalizi ya msimu mpya wa michuano mbalimbali. Kocha wa Liverpool, Jurgen Klopp amethibitisha Mane anatazamiwa kurudi katika kikosi cha Liverpool Agosti 5, hii ikiwa ni siku moja baada ya mechi dhidi ya City lakini pia ikiwa ni chini ya wiki moja kabla ya kucheza pambano la kwanza dhidi ya Norwich.

“Yupo katika hali nzuri. Ni wazi walikuwa na sherehe kwao Senegal na nina furaha kuhusu hilo kwa sababu wameonyesha wanaheshimu michuano na wameona nafasi ya pili ni mafanikio kitu ambacho ni kizuri,” alisema Klopp.

“Kwa sasa yupo likizo, sio likizo ndefu sana. Atarudi Agosti 5 baada ya mechi ya Manchester City. Ina maana atakuwa na wiki mbili. Kuna siku nne au tano za kujiandaa na Norwich. Siku 10 kabla ya Chelsea katika Super Cup,” alisema kocha huyo.

Mane alikuwa na msimu mzuri ulioisha licha ya Liverpool kushindwa kutwaa taji la Ligi Kuu ya England ambapo aliibuka kuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu ya England akifunga mabao 22 sambamba na staa mwenzake wa Liverpool, Salah, na staa wa Arsenal, Pierre-Emerick Aubameyang.

Yeye na Salah pia waliiingia katika orodha ya mastaa wa Afrika waliowahi kutwaa ubingwa wa Ulaya baada ya kuichapa Tottenham bao 2-0 katika pambano la fainali jijini Madrid.