Sabato akiamua Makambo anasubiri

Tuesday December 4 2018

 

By Doris Maliyaga

UNAAMBIWA hivi, mshambuliaji wa Mtibwa Sugar, Kelvin Sabato ‘Kiduku’ ni bonge la mchezaji na kama atafanya mazoezi ya dhati, Taifa Stars hata isingekuwa na shida na mtu wa kufunga mabao.

Sabato ambaye yumo kwenye kikosi cha Taifa Stars cha U-23, sifa yake kubwa ni kupiga mipira iliyokufa kama faulo na penalti huwa hakosei ni bao tu.

Kiwango hicho kimeisaidia Mtibwa Sugar kufika hapo lakini wataalamu wanasema, sehemu anayofanyia kazi ni kama nusu tu kwani ana uwezo mkubwa ambao kama angezingata kwenye matizi, wachezaji wanaong’ara sasa mfano wa kina John Bocco ‘Adebayor’, Meddie Kagere wa Simba, Mrisho Ngassa ‘Anko’ na Mkongo Haritier Makambo wa Yanga wangekuwa wanasubiri.

“Sifichi lakini kama Sabato angekuwa mtu wa kufanya mazoezi ya nguvu, angekuwa mchezaji mkubwa sana na si kwa klabu tu, bali angekuwa msaada mkubwa kwa timu za taifa kama hiyo ya chini ya miaka 23 na Taifa Stars,” alisema Kocha wa Makipa wa Mtibwa Sugar, Patrick Mwangata.

Mwangata ambaye ni mlinda mlango wa zamani wa Simba na Taifa Stars ameongeza ana uhakika na anachokizungumza kwa sababu ana uzoefu mkubwa kwenye soka.

Hata hivyo, Sabato si miongoni mwa wachezaji wa Mtibwa Sugar waliosafiri kwenda Shelisheli kuivaa Northen Dynamo katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.

“Huwa naambiwa kuwa nina uwezo lakini wao ndiyo wanaoniona, kuhusu mazoezi sijui, binafsi naona nafanya kwa bidii tu sijui kinachotokea,” alisema Sabato.

Amesema, watu huwa wanajaji bila kufahamu kwani wakati mwingine kuna matatizo mengi nje ya uwanja yanawasumbua wachezaji kama familia na mengineyo.”

Advertisement