Wanapotea wapi hawa: Sababu za makocha wazawa kushindwa kusonga mbele!

Muktasari:

Timu kongwe Simba na Yanga kwa muda mrefu zimekuwa chini ya makocha wa kigeni, hii inatokana na mambo mengi nyuma yake kwa wazawa katika soka la Bongo na chache kati ya hizo ni pamoja

KUFANYA vizuri kwa timu kunachangiwa na mambo mengi kwenye kikosi husika, mojawapo ni kuwa na kocha sahihi. Ndio maana inawachukua muda mrefu viongozi kupata kocha pamoja na benchi lake la ufundi.

Tumeshuhidia timu mbalimbali zikiyumba, sio kwasababu ya kuwa na uchumi mbaya, bali kutokana na kuwa na kocha ambaye sio sahihi kulingana na mahitaji ili kufikia malengo wanayoyaweka ndani ya msimu husika.

Tanzania ni moja kati ya nchi zenye ligi yenye ushindani mkali na kupendwa na mashabiki hasa Ukanda wa Afrika Mashariki na kuwa kimbilio kwa makocha wa kigeni pamoja na wachezaji ndio maana msimu huu Ligi Kuu ina wachezaji 63 wakigeni.

Timu kongwe Simba na Yanga kwa muda mrefu zimekuwa chini ya makocha wa kigeni, hii inatokana na mambo mengi nyuma yake kwa wazawa katika soka la Bongo na chache kati ya hizo ni pamoja na:

ELIMU / TAALUMA

Jambo limeonekana kuwa kikwazo kikubwa kwa wazawa ni kukosa elimu kulingana na soko la ushindani la kazi ya ukocha na kuwafanya wengi wao kushindwa kukimbizana na mabadiliko ya soka la kisasa na kuwapisha wageni wakiendelea kutesa, alisema Kocha wa Tanzania Prisons, Mohamed Rishard ‘Adolph’.

Adolf ambaye alipata kiuwa mchezaji wa Pan Afrika, Pamba na Taifa Stars aliongeza wazawa wengi hawana kasumba ya kujiendeleza kwenye elimu kitu ambacho ni hatari kwenye mabadiliko ya soka kujua nini kinafanyinka katika nchi zilizoendelea kwenye tasnia hiyo.

KUSHINDWA KUTHAMINIWA

Kocha Kenny Mwaisabula ‘Mzazi’ anasema viongozi wengi wa timu wanawachukulia sivyo makocha wa nyumbani na kushindwa kuwathamini, lakini anapotokea kocha wa nje ya nchi, basi atapewa kila kitu kuanzia usafiri hadi nyumba wakati mzawa hapewi mahitaji hayo.

“Kocha anaweza akaomba mipira 25 lakini mwisho wa siku akapewa mipira mitano na anapofanya vibaya kutokana na uzembe uliosababishwa na wao wenyewe, atafukuzwa na hatimaye kutumia gharama kubwa kumtafuta kocha mwingine ambaye hana utofauti na mzawa.

“Kuna mwaka alikuja kocha kutoka Afrika Kusini ambaye alisoma na Boniface Mkwasa huko Brazil, akastaajabu kukuta Mkwasa hana hata timu ya FDL wakati yeye kwenye ‘performance’ alikuwa chini, hapo ndio utajua kwanini watu wanasema nabii hakubaliki kwao,” alisema Mwaisabula.

UTHUBUTU

Tatizo hili limeonekana sio kwa makocha pekee, bali hata kwa wachezaji wetu, kushindwa kuwa na uthubutu wa kutoka nje ya nchi ili kupata changamoto na kuzidi kujifunza kwa wenzetu hilo kwa Tanzania limekuwa tofauti.

“Angaliwa makocha kutoka Burundi mfano kina, Etienne Ndayiragije wanakuja Tanzania sio kwasababu wa ubora wa ligi pekee, bali wanaongeza wasifu wa kocha na sasa yupo kwenye kikosi cha Timu ya Taifa,” alisema mchambuzi na mchezaji wa soka wa zamani, Ali Mayay.

LUGHA

Japo soka lina lugha yake ambayo hutumika dunia nzima, suala la kujiongeza kwa makocha kujua lugha hasa Kingereza nayo imekuwa sababu mojawapo zinazowafanya kushindwa kuwa na uhakika na kazi yao.

“Ukiacha zile kozi za awali zinazoendeshwa na TFF kwa Lugha ya Kiswahili, kozi nyingi za Caf zinaendeshwa kwa lugha mbili, kama sio kingereza basi Kifaransa, ndio maana kina, Mwinyi Zahera wanakwenda Ufaransa kufuata kozi kwa sababu wana uelewa wa lugha hiyo,” alisema Mayay.

UBUNIFU WA KAZI

Kazi yoyote ili uendelee kubaki kwenye chati inategemea na ubunifu kwa wale wanaoendesha, hivyo kwenye ukocha benchi la ufundi pamoja na kocha nalo linapaswa kuwa hivyo, lakini kwa Tanzania, makocha wetu wameonekana kulikosa hilo.

Mojawapo ya ubunifu wa kocha ni pamoja na kuwasoma wapinzani wake haraka, kubadili mbinu kutokana na mahitaji na uwezo wa mpinzani wake, lakini kuwa na maamuzi ya haraka na sahihi kwa wazawa nalo limeonekana kuwa tatizo kwao.

KUJIAMINI

Makocha wengi wanapoteza mwelekea hasa wanapokosa hamasa kwa mashabiki wao kutokana na shinikizo la kupata matokeo mazuri kwa muda ambao huwa mgumu kwao kwenye mchezo.

Pamoja na kuwa na uwezo na uzoefu, bado wazawa wanakosa kuaminiwa hasa inapotokea nafasi ya kufundisha timu za taifa asilimia kubwa utakuta wanaopewa ni wale wa mataifa ya nje, yaani hata Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF) bado haliwaamini, anasema Kocha, Rashidi Idi ‘Chama’.

USHABIKI

Tatizo lingine ambalo makocha wameeleza ni pamoja na wengi wao kuwa na ushabiki wa timu nyingine ili hali wakiwa wanafundisha timu nyingine, hasa kwa timu kongwe za Simba na Yanga ndizo zimekuwa zikiwaathiri makocha wazawa kutokana na kuonyesha wazi unazi wao.

“Unaweza kukuta timu unayofundisha inacheza na Simba au Yanga halafu wote mnahitaji ushindi, lakini anasahau kufanya kilichomuweka kwenye timu na anageukia mapenzi ya timu hizo kongwe na mwisho wake anapoteza mchezo na uamifu wa kazi pia unapotea kwa mabosi wake,” alisema Chama ambaye amewahi kukipiga Yanga, Pani na Taifa Stars.