Sababu za Eymael kuwatosa Mkwasa, Manyika hizi hapa

Muktasari:

KOCHA wa Yanga, Luc Eymael amemuondoa kikosini msaidizi wake, Boniface Mkwassa na Kocha wa makipa, Peter Manyika wakati wakijiandaa kuikabili Mtibwa jioni hii mjini Morogoro.

Eymael licha ya kutoweka wazi sababu alitamka jana kwamba; “Mimi ni Kocha mwenye weledi. Nimewaacha na kwenda na kocha wa timu ya U-20, Saidi Maulid ‘SMG’.

“Ni vigumu kuzungumzia hilo pamoja na ukweli kuwa kuna makocha hawajasafiri nasi, mechi lazima ichezwe na nina kocha msaidizi ambaye ndiye kocha mkuu wa timu ya U-20, Maulidi. Kazi itafanyika pamoja na kuwa na kikosi finyu chenye majeruhi na wagonjwa,” alisema Eymael, ambaye habari za ndani zinasema amewakataa makocha hao na anataka kuwa na benchi jipya kabisa.

Ukiachana na Mapinduzi Balama ambaye amevunjika mguu, wachezaji wengine, Papy Tshishimbi, Haruna Niyonzima na kipa Farouk Shikhalo ni majeruhi huku Patrick Sibomana akimuuguza mkewe.

Hata hivyo, alisema amemwambia Metacha amfuate Morogoro ili kuongeza nguvu kama tu atakuwa amepata nafuu.

“Metacha ni mgonjwa na hataweza kucheza mechi kutokana na hali yake kwa sasa. Alilazwa na kutolewa, amekuja huku kuongeza morali, ila kipa namba tatu, Ramadhan Kabwili na kipa wa timu ya U-20, Geofrey watakuwepo katika mechi hiyo,” alisema Eymael, ambaye baadhi ya viongozi wa Yanga walidokeza jana kwamba, siku zake klabuni hapo zinahesabika. Hata hivyo, wamefichua kuwa wanasubiri mchezo dhidi ya Mtibwa ipite kwanza.

Kwa mujibu wa Eymael suala la Morrison (Benard) lipo chini ya uongozi wa klabu na si kazi yake zaidi ya kusimamia timu wakati wa mazoezi.

“Morrison ana matatizo na utovu wa nidhamu, sina haja ya kuingia kwa ndani zaidi kwani kila mtu anafahamu alivyofanya, ila katika suala la uchezaji, ni mchezaji mzuri,” alisema.

Hata hivyo, mabosi wa Yanga walipotafutwa jana hawakutaka kuzungumzia lolote kuhusu sakata la makocha hao, lakini Mkwassa mwenyewe alidai amebaki Dar es Salaam kwa sababu ya masuala ya kifamilia.