Sababu ya Zahera kuangua kilio

Muktasari:

Kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera amefunguka na kuelezea sababu ya kuangua kilio jijini Mbeya, ambako aliibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Prisons, mchezo ulipigwa Uwanja wa Sokoine.

KOCHA wa Yanga, Mwinyi Zahera aliangua kilio baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Prisons, jambo lililowaacha njiapanda mashabiki wake kushindwa kuelewa ni machozi ya furaha ama amekumbwa na tatizo linalomnyima raha na kufanya ashindwe kujizuia.
Mwanaspoti Online lilimtafuta kocha Zahera ili kujua alikumbwa na kitu gani kilichompelekea kuangua kilio mbele ya kadamnasi ya watu alikuwa na haya ya kusema.
"Nimejikuta nina uchungu nisioweza kuuzuia, wachezaji wanachokifanya uwanjani ni tofauti na maisha wanayoishi kwa sasa, wanaonyesha uzalendo wa hali ya juu kana kwamba mambo ni mazuri Yanga.
"Ninapokuwa na wachezaji nasimama nafasi ya baba ambaye ana watoto wanaoonyesha juhudi ya kufanya kitu, lakini nakuwa siwezi kuwatimizia mahitaji yao kwa wakati, sio kwamba nakuwa napenda ila sina cha kuwapa.
"Natamani baada ya ushindi niwape kitu cha kuwatia moyo nakuwa sina, lakini nawaona wanapambana kama vile wanapatiwa kila kitu, kiukweli nimejikuta siwezi kustahimili, kuna wakati navaa roho ngumu kuwaelekeza kujituma ili tuweze kuchukua ubingwa, hawachoki kunisikiliza na kuyatendea kazi,"anasema
Yanga imecheza mechi 14 imeshinda mechi 12,sare mbili, jambo linalomfanya kocha Zahera aendelee kuwa mwiba kwa makocha wenzake wa kigeni kama Patrick Aussems wa Simba, ambaye kikosi chake kimecheza michezo 12, kimeshinda nane na sare tatu.