Sababu Samatta kutakiwa Everton hizi hapa

Thursday October 11 2018

 

By Thomas Ng’itu

Dar es Salaam. Kasi ya nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta ya kufunga mabao, ubutu wa safu za ushambuliaji za Everton, Burnley, West Ham United na Brighton & Hove vimeziingiza vitani klabu hizo kuwania saini ya mshambuliaji huyo.

Samatta amekuwa mwiba mkali tangu msimu huu ulipoanza ambapo amefunga mabao 14 katika mechi 16 alizocheza katika timu yake ya KRC Genk ya Ubelgiji kwenye mashindano mbalimbali.

Mshambuliaji huyo amefunga mabao hayo katika mashindano ya Kombe la Europa yaliyopo hatua ya makundi, Ligi Kuu ya Ubelgiji na Kombe la Chama cha Soka Ubelgiji.

Everton inatajwa kumuwania zaidi Samatta ikiamini ataiokoa na ubutu wa safu yake ya ushambuliaji ambayo katika mechi nane ilizocheza hadi sasa imefunga mara 13.

Mtandao wa www.readeverton.com na www.hitc.com imetaja sababu nyingine kubwa inayoishawishi Everton kumnasa Samatta ni kuziba pengo la mshambuliaji Omar Niasse ambaye huenda akatimka.

Brighton & Hove inamuwania Samatta kama mtu anayeweza kuingia katika kikosi moja kwa moja baada ya mshambuliaji Percy Tau aliyesajiliwa kutoka Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini kushindwa kupata namba.

Pia Samatta anaweza kwenda kumaliza ufalme wa nyota wa Mexico, Javier Hernandez 'Chicharito’ West Ham United ambayo ipo kwenye harakati za kumuwania ili kuimarisha safu ya ushambuliaji ambayo imefunga mabao manane.

Kocha na mchambuzi wa soka Dk Mshindo Msolla, alisema Samatta ni mchezaji anayejua wajibu wake na hashangai kuwania na klabu kubwa za Ulaya.

“Nadhani anatimiza wajibu wake hususani kufunga mabao, thamani yake itakuwa kubwa zaidi kama ataendelea kufunga mara kwa mara,” alisema,” alisema Msolla.

Kocha huyo wa zamani wa Taifa Stars, alisema wachezaji wanaocheza ligi ya ndani wanapaswa kuiga mfano bora wa Samatta kwa kujikita katika nidhamu ndani na nje ya uwanja.

Advertisement