Saa tatu za soga na Lady Jay Dee

Muktasari:

Najaribu kumdadisi Jide mambo mengi kuhusu yeye. Kuhusu wanamuziki wa sasa na kuhusu kila kitu kuhusu muziki wa zamani na wa sasa. Jide anaufungua moyo wake katika namna ambavyo hajawahi kuufungua kama nilivyomsikia.

ALIWAHI kuimba Mwanamke anayeitwa Aretha Franklin. Aliimba ‘Rose still a Rose’. Mwanamke ataendelea kubakia kuwa mwanamke. Ataendelea tu. Tabia zao zitabakia kuwa zile zile tu. Ndivyo alivyonigandisha Lady Jay Dee katika baa maarufu ya The Governor’s pale Kinondoni. Tuna tabia ya kukutana na kupiga soga.

Ilikuwa tukutane saa tisa, ikavuka. Ikaja saa kumi, ikavuka. Ikaja saa kumi na moja ikavuka. Saa kumi na mbili akaposti katika mtandao wake wa Instagram kwamba, ananifuata nilipo. Poda ilikuwa imeshamiri katika sura yake, manukato yakinukia katika mwili wake na mbwembwe zake zile zile za tangu akiitwa Binti Machozi.

Saa moja kamili alifanikiwa kufika na ‘uongo wake’ wa hapa na pale kuhusu tatizo la foleni. Mbele yetu tuliweka Mvinyo aina ya KWV na kuanza soga za hapa na pale. Ni hapo ndipo nilipogundua kwamba mdomo wa Jide ni kama wa samaki. Una mengi ya kuongea lakini ‘umejaa maji’.

Najaribu kumdadisi Jide mambo mengi kuhusu yeye. Kuhusu wanamuziki wa sasa na kuhusu kila kitu kuhusu muziki wa zamani na wa sasa. Jide anaufungua moyo wake katika namna ambavyo hajawahi kuufungua kama nilivyomsikia.

Akiwa nje ya mchezo kama mkongwe anayeheshimika, Jide anashuhudia kwa upendo kuibuka kwa rundo la wadogo zake wenye vipaji kama Vanessa Mdee, Nandy, Ruby, Linah na wengineo. Anadai kwamba hana tatizo na vipaji hivi huku akidai ni wadogo zake anaowapenda.

Lakini, hata hivyo anatoa kitu kizito kilichopo moyoni mwake. Najikita zaidi katika kumchokonoa Jide azungumzie hali ilivyo kati ya muziki wa sasa na wa zamani pamoja na hali ilivyo kati ya wasanii wa zamani na wa sasa.

“Edo kuna watu wanasababisha wanamuziki wa sasa wasituheshimu. Sijui kwanini. Wametengeneza daraja kubwa baina yao na sisi kwa sababu ya chuki zao binafsi. Hawa watoto wa sasa wala hawana shida na sisi, lakini kuna watu tu wameamua kutengeneza chuki.” anasema Jide.

“Mimi ni mwanamuziki wa kwanza wa kike kutamba katika muziki wa kizazi kipya, lakini umewahi kusikia hawa wanamuziki wa sasa wananitaja kuwa mimi ni Role Model wao? Hapana. Wameambiwa wasinitaje” anaongeza Jide.

“Kwa wenzetu unaweza kukuta Rihanna amekaa meza moja na Eve na anasema kwamba ‘wewe ni Role Model wangu’. Kila mmoja anafanya kazi zake anapiga pesa zake kwa njia yake. Huku imekuwa tofauti kwa sababu kuna watu hawataki hilo litokee. Siwezi kushindana na mwanamuziki yeyote wa kike kwa sasa. Mimefanya yangu nimemaliza. Hakuna nilichobakisha.”

Tunaendelea kupiga stori na Jide anaufungua zaidi moyo wake kwa kudai kwamba, wanaofanya hilo ni watu wenye roho mbaya ambayo wameshindwa kufuata misingi ya kuheshimiana ambayo wao wenyewe waliiweka wakati walipopokelewa na wanamuziki wa zamani.

“Nikwambie kitu, sisi wakati tunaanza kuimba tuliwasikia kina Marijan Rajabu na heshima zao. Marijan alikuwa mtu wa kwanza kupata tuzo nje ya nchi. Alipata Kenya. Lakini hatukufanywa tusiheshimu alichofanya. Wengine mpaka tuliimba nyimbo zake. Mimi ni mwanamuziki wa kwanza kupata tuzo nje ya nchi, lakini kuna watu wanajaribu kuziba huo ukweli,” anasema Jide.

“Leo wapo watu wanaopata tuzo nje ya nchi lakini wanaonekana kama vile wanafanya kitu kipya. Kisa? Ni chuki ambayo imetengenezwa na baadhi ya watu ili kumfanya Jide na wakongwe wengine wasisikike au wadharaulike,” anaongeza Jide.

Wakati tukizungumza, tunapewa chaguo la kupiga nyimbo ambazo tunataka kupitia simu ya mkononi ya mmiliki wa baa hiyo. Jide anagoma kusikiliza nyimbo zake na badala yake anataka kusikiliza nyimbo za wanamuziki wengine wa sasa.

“Sitaki kusikiliza nyimbo zangu. Weka ‘Kivuruge’ wa Nandy” anasema Jide. Ni hapo ndipo ninapogundua kwamba Jide anapenda zaidi kusikiliza nyimbo za wanamuziki wengi wa sasa na anafurahia muziki kama kawaida.

Anachagua nyimbo za Nandy. Vanessa, Ruby, Maua Samma, Linah na wengineo. Lakini, zaidi anaupenda wimbo wa ‘Mhudumu’ wa Dogo Aslay.

Tunaendelea na maongezi yetu na sasa namchimba zaidi Jide kuhusu mabadiliko ya muziki na pia jinsi ambavyo wanamuziki wengi wa zamani wa zama zake wamechoka na wanashindwa kurudi katika anga za juu.

“Unajua kila kitu kinabadilika. Kwa sasa ni zama za wengine. Tatizo wasanii wengi wa zama zangu hawakujiandaa kisaikolojia na ndio maana baadhi yao wanaishia kula dawa za kulevya. Inabidi ukubali kwamba, Jide wa miaka 10 iliyopita hawezi kuwa Jide wa leo. lazima ukubali.

“Tatizo kubwa ni kwamba kuna wasanii wa zamani wanajaribu kulazimisha waonekane kama ilivyokuwa miaka 10 iliyopita kitu ambacho hakiwezekani. Hata taswira yako binafsi imebadilika vipi kuhusu muziki wako?,” anahoji Jide.

Pamoja na kukiri hilo lakini Jide anaamini kwamba, muziki wa Tanzania unamshangaza kwa namna ambavyo wanamuziki wa zamani hawaheshimiwi na wametengenezewa mazingira ya kutosikika tena baada ya kuondoka kwao.

“Ukienda Marekani mpaka leo Michael Bolton anapiga shoo na anajaza. Anatumia nyimbo zake za zamani. Ipo hivyo hivyo kwa kina Janeth Jackson na wengineo. Lakini, hapa eti mpaka utoe nyimbo ndipo upate shoo au ufanye shoo. Inashangaza sana,” anasema Jide.

Jide anadai kwamba hana tatizo lolote kutengeneza wimbo na mastaa wa kike au wa kiume ambao, wanatamba katika zama hizi. Namuuliza kama anaweza kuimba wimbo mmoja na Vanessa Mdee, ambaye kwa sasa anaweza kuwa mwanamuziki wa kike aliye juu zaidi.

“Sina bifu na Vanessa kabisa. Ni mdogo wangu. Kwanini nisifanye naye wimbo kama ikitokea? Kitu cha msingi ni kufanya kitu kizuri. Usije ukafanya kitu ambacho kitapotea zaidi na kukushusha. Ujue achilia mbali kuimba lakini kuna kazi kubwa katika kuwekeza pesa na kufanyia promosheni wimbo. Unaweza kufanya kazi tatu ambazo kama zote unaweka tu pesa lakini hazilipi inakuangusha zaidi,” anasema Jide.

Jide anakiri kwamba amefanya wimbo mmoja alioshirikishiwa na mwanamuziki maarufu wa kizazi kipya, Harmonize ambaye juzi alitangazwa kuwa katika harakati za kujiondoa katika kundi maarufu la muziki la Wasafi.

“Harmonize alimpigia simu Gadna (mumewe wa zamani) na kumuulizia kama anaweza kufanya kazi na mimi. Gadna akanicheki na nikakubali kwahiyo tumefanya lakini nadhani bado hajauachia,” anasema Jide.

Wakati tukiendelea kupiga soga. Jide anasimama na kuucheza kwa hisia kali wimbo wa ‘Kiokote’ wa Maua Sama. Anaucheza na kuuimba. Lakini, baadaye tunaendelea na soga letu huku akisikitishwa na jinsi ambavyo wasanii wa sasa hawana ushirikiano.

“Zamani wanamuziki walikuwa wanaweza kuja kwangu wote, wakati ule naishi Kinondoni. Angekuja Professa Jay, TID, Mangwear, na wengine wengi. Tungekula na kunywa na kupiga sana stori. Siku hizi sisikii kama wasanii wana tabia hizi. Sijui kama wanafanya hivi,” anaongeza Jide.

Jide pia anashangaa kwamba siku hizi wanamuziki wanalazimishwa kuimba muziki wa aina moja hili watoke au waonekana wamefanya vizuri wakati zamani hali haikuwa hivyo.

“Zamani mimi nilikuwa na muziki wangu, Professa Jay ana muziki wake, Juma Nature anaimba kivyake, TID anaimba kivyake, kila mmoja anaimba kivyake. Lakini, sasa wenye muziki wao wanataka watu wote waimbe muziki wa aina moja,” anaongeza Jide.

Tunamaliza soga letu na kumrudisha Jide nyumbani kwake Kimara usiku wa manane. Bado nina kiu ya kumuuliza maswali mengi kuhusu habari nzito zilizowahi kumtokea katika miaka ya karibuni. Jide anaahidi kwamba muda si mrefu atafunguka. Anaahidi kwamba, akifunguka basi kiandikwe kama kilivyo. Tega sikio.