SPOTI DOKTA : Mwanamichezo anzia hatua hii kujiweka sawa

Muktasari:

Ikumbukwe kuwa kwa sasa maisha ya jamii nyingi duniani yamebadilika kutokana na njia zilizoelekezwa za kujikinga ni pamoja na kukaa ndani tu, jambo ambalo haliepukiki katika maeneo yenye visa vingi vya corona.

Takribani mipaka na nchi 200 duniani bado inakabiliwa na janga la kidunia la ugonjwa wa corona (Covid-19) unaosababishwa na familia ya virusi vya corona ambavyo mpaka sasa havina tiba wala kinga.

Ugonjwa huu umelipuka maeneo mengi ambako umesababisha vifo na visa vingi vya corona ikiwamo Hispania, Italia, China, Marekani na Iran.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya duniani (WHO) na mtandao unaotoa takwimu za kidunia za ugonjwa wa corona ujulikanao kama wolrdometer, inaelezwa mpaka sasa kuna maambukizi yaliyothibitishwa zaidi ya 860,000 na vifo zaidi ya 42,000 duniani kote.

Ugonjwa huu kulipuka kwake kumesababisha pia kuwakumba na kuwasababishia vifo wadau wa michezo ikiwamo hapa Tanzania, Iddy Hashim Mbita ambaye alikuwa mwanachama na kiongozi wa Simba aliyefariki juzi alfajiri katika Hospitali ya Rufaa ya Mloganzila, Dar es Salaam. Wakati nchi ya Senegal imempoteza Papa Diouf aliyewahi kuwa rais wa kwanza mweusi wa klabu ya soka ya Ufaransa ya Marseille ambaye amefariki akiwa na umri wa miaka 68.

Vifo hivi vinatupa onyo la kuchukua tahadhari zaidi za kujikinga kwani ugonjwa huu sio kweli kuwa unaua Wazungu pekee, bali hata Waafrika pia unawapata na kuwaua.

Ikumbukwe kuwa kwa sasa maisha ya jamii nyingi duniani yamebadilika kutokana na njia zilizoelekezwa za kujikinga ni pamoja na kukaa ndani tu, jambo ambalo haliepukiki katika maeneo yenye visa vingi vya corona.

Katika kipindi hiki kuna maelfu ya wanamichezo ambao wapo katika nchi ambazo zina visa vingi na vifo vya corona wakiwa wametengwa au kujitenga au kutotoka nje.

Ni kawaida kwa mwanamichezio ambaye yupo katika mazingira hayo kupata hali isiyo ya kawaida ya kuhisi uchovu au hali ya misuli ya mwili kuuma. Kama itajitokeza hali hii kwa mwanamichezo usistuke kwani hiyo inayokana na viungo vya mwili kuwa na mazoea ya mazoezi ya mara kwa mara na kufanya kazi wakati wa mechi au mashindano.

Ikumbukwe makatazo yote yaliyotolewa ikiwamo ya kubaki ndani au kutengwa kutokana na kuchangamana na washukiwa au wagonjwa wa corona waliothibitishwa yalikuwa ni ya ghafla hivyo mwili ulipewa jukumu jipya ambalo halijauzoea.

Leo tutalitupia macho tatizo la uchovu ambalo kipindi hiki mwanamichezo anaweza kupata hisia za uchovu wa viungo vya mwili kiasi cha kujihisi kuwa ana ugonjwa mkali mwilini.

Jinsi wakukabiliananna uchovu

Uchovu hujulikana kitabibu kama Muscle fatigue au physical fatigue ni hali inayojitokeza mwilini pale misuli ya mwili inapofanyishwa kazi kupita kiwango chake. Lakini pia hili hii inaweza kujitokeza kama mwili haufanyi mazoezi yoyote au kusitishwa ghafla kwa maoezi ya mwili na kukaa tu bila kufanya mazoezi yoyote.

Kujitokeza kwa uchovu unao ambatana na maumivu ni njia mojawapo ya mwili kujihami na kukupa ishara kuwa viungo vya mwili ikiwamo misuli haifanyiwi unyooshaji. Uchovu unasababisha misuli ya mwili kukosa nguvu kama ilivyo kawaida yake. Tatizo hili linaweza kuambatana na maumivu yanayoweza kuwa ya wastani mpaka kuwa makali.

Hisia za uchovu huweza kuhisiwa zaidi katika maeneo ya maungio (joint), mgongoni, kiunoni, mapajani na magotini. Mwathirika anaweza kuhisi pengine ana ugonjwa mkubwa kumbe ni uchovu wa viungo vya mwili. Uchovu unatokana na uwapo vitu vinavyoingilia hatua za utendani yaani kukunjuka na kujikunja kuwezesha matendo mbalimbali ikiwamo kukimbia, kuruka na kutembea.

Tatizo hili linaweza kusababishwa na mishipa ya fahamu kutosisimua vizuri misuli na uwepo wa mrundikano wa mabaki au taka mwili baada ya seli kutumia sukari ya mwili kupita kiwango chake.Uchovu unaotokana na mwili kufanya kazi sana au kusitishwa ghafla kwa ufanyaji kazi wa misuli ni tatizo la muda tu ambalo linaweza kuisha endapo mambo haya yatafanyika. Unapokuwa na uchovu unahitajika kulala masaa 6-8 pasipo usumbufu wowote ili kuepuka kukatika katika kwa usingizi.

Pumzisha mwili katika maeneo yenye hewa safi au maeneo ya wazi kwani mazingira ya hewa chafu yanachangia kuongeza uchovu zaidi. Kula mlo kamili ikiwamo vyakula vyenye protini, mboga za majani na matunda na vyakula vya wanga.

Lishe hii inasaidia kukurudishia nguvu iliyotumika, kurudishia akiba ya nishati katika misuli na kuwezesha ukarabati na uponaji wa vijeraha vya misuli.

Kunywa lita 1.5-3 na fanya mazoezi mepesi na nyoosha viungo kwa dakika 5-10 kabla ya kuanza mambo yoyote ukiwa ndani kwako.

Fanya mazoezi ya viungo ya kunyoosha misuli ya mwili angalau dakika 10-15 huku ukiwa katika mkao sahihi kimwili ili kuondoa uwezekano wa kujijeruhi misuli. Oga kwa maji ya vuguvugu yanayotiririka kwa wingi au oga katika mabafu ya kisasa yenye kutoa mvuke wa joto. Epuka mambo yatakayokupa shinikizo la akili au kukusababishia hisia hasi kwani yatakuongezea uchovu. Jichanganya katika mazingira ya burudani ili kukupa hisia chanya.

Epuka matumizi ya vilevi ikiwamo unywaji pombe kupita kiasi, matumizi ya tumbaku kwani vinachangia kuongeza uchovu wa mwili.

Unapokuwa na uchovu wa mwili usikimbilie kutumia dawa za maumivu pasipo ushauri wa daktari.

Endelea kuzingatia njia za kujikinga na corona

Osha mikono kwa sabuni na maji mengi yanayotiririka mara kwa mara au tumia kitakasa mikono.

Ieleweke pia karibia sabuni nyingi zilivyotengenezwa huwa na kampaundi zenye ukakasi ambazo humyima nafasi kirusi au vimelea wengine kuweza kuishi.

Vitu vingine kama dawa za kuoshea kama vile Detol au spiriti yenye asilimia 60 % ya kilevi huweza kutumika pia kuoshea mikono au maeneo ya mwili ambayo endapo utagusana na mwenye maambukizi.

Inasisitizwa zaidi kuosha mikono kutokana na eneo hili la mwili kuwa na shughuli nyingi ikiwamo kushika shika huku na kule mwilini kama vile puani, machoni na mdomoni.

Tumia vikinga pua, mdomo na uso endapo unahudumia washukiwa wa korona. Tutumie kitambaa au tishu au sehemu ya mbele ya kona ya kiwiko kuzuia vitone vinarushwa na chafya au kikohozi. Vilevile ikashauriwa kukaa mbali na watu ambao wana maambukizi au washukiwa wa ugonjwa huu angalau kwa umbali wa mita moja toka kwa watu hawa.

Umbali huu unakuepusha kuwa katika hatari ya kushikamana na matone yenye maambukizi ambayo yanaweza kurushwa mdomoni au puani.