SPOTI DOKTA : Majeraha ya Ngolo Kante yamekaa hivi

Muktasari:

Majeraha ya misuli ya Adductor hayatabiriki uponaji wake kwani misuli kuwa eneo la ndani kabisa likijumuisha kundi la misuli mikubwa minne iliyojipachika katika kinena sehemu ya mfupa wa kiuno.

Wakati klabu ya Chelsea ikipokea kipigo cha mabao 2-0 na klabu ya Machester United usiku wa Jumatatu ilipata pigo baada ya kiungo wake wa kati Ngolo kante kupata majeraha dakika ya 12 ya mchezo.

Kante alionekana ghafla kukaa chini huku akishikilia mapaja na huku akikunja sura yake hali iliyoashiria nidhahiri alipata majeraha yaliyompa maumivu makali katika kona ya ndani ya paja.

Kiungo huyo mkabaji hakuweza kuendelea na mchezo huo na alitoka nje ya uwanja huku akiwa anachechemea nakusaidiwa kutoka lakini hatua chache alijitegema na kutembea mwenyewe.

Kocha wa klabu hiyo Frank Lampard ameeleza katika vyombo vya habari kuwa kiungo huyo amepata majeraha ya misuli ya paja iliyojichimbia kwenye kinena ambayo hujulikana kitabibu kama Groin.

Misuli iliyojeruhiwa inajulikana kitabibu kama Adductor muscles ni majeraha ambayo huwapata wanasoka kutokana na kutumia zaidi miguu hivyo kulifanya eneo hilo kufanya kazi sana kupita kiasi.

Majeraha ya misuli ya Adductor hayatabiriki uponaji wake kwani misuli kuwa eneo la ndani kabisa likijumuisha kundi la misuli mikubwa minne iliyojipachika katika kinena sehemu ya mfupa wa kiuno.

Vile vile eneo hilo huwa na nyuzi ngumu za ligamenti zinazounganisha mfupa na mfupa na tendoni ambazo ni miishilio ya misuli hiyo inayojipachika katika mfupa wa kiuno.

Endapo itatokea kuwa misuli na nyuzi hizi zimejeruhiwa na kukatika au kuchanika pande mbili huchukua muda mrefu kupona na hukadiriwa na madaktari wa majeraha ya michezo kupona kati ya miezi 3-6.

Alifanyiwa vipimo kadhaa ikiwamo kipimo cha picha ambacho ni muhimu kwa aina hii ya majeraha kijulikanacho kama Magnetic Resonance Imaging (MRI) lakini haikuwekwa bayana ukubwa wa jeraha.

Kipimo hiki cha kisasa kinachotumia mionzi salama hupiga picha za tishu laini na kuleta picha inayotafsiriwa na kompyuta ikiwa ni picha inayoonyesha vizuri kwa kina viungo vya ndani ya mwili.

Katika nchi zilizoendelea MRI hutumiwa zaidi kufanya uchunguzi wa majeraha ya michezo na hivyo kuwawezesha kubaini kiungo cha mwili kilichojeruhiwa na kumpa matibau sahihi mchezaji.

Kwa jicho la kitabibu kwa namna alivyotoka uwanjani kwa mtindo ule huenda ikawa amepata vimchubuko au kuvutika sana kwa misuli hiyo au kuchanika kiasi hivyo kuangukia daraja la pili.

Majeraha haya si habari njema kwa Kante kwani yanachangia kudidimiza kiungo huyo ambaye ni muhimu katika klabu hiyo ambayo keshokutwa ina kibarua kugumu cha ligi EPL dhidi ya Totenham.

Akiwa ni msimu wake wa nne klabuni hapo katika siku za karibuni ameandamwa na majeraha kiasi cha kumfanya msimu huu kuanza kucheza katika mechi 16 tu za ligi kuu kati ya mechi 26.

Lampard anaeleza kuwa kwa mchezaji kama Kante taarifa hizi za majeraha hazimpi chochote zaidi ya kumchanganya tu kwani anafahamu anavyohitajika katika klabu hii.

Kante mwenye miaka 28 ni mmoja wa viungo bora duniani ambaye hutumia sana nguvu na kasi hivyo kumweka katika hatari ya kupata majeraha mbalimbali.

Ubora wake katika sehemu ya kiungo kunamfanya kutumika sana na klabu na timu ya taifa jambo ambalo ni moja ya sababu ya mchezaji huyu kupata majeraha.

Kante ambaye ni mshindi wa kombe la dunia, kombe la ligi kuu mara mbili, kombe la FA na mafanikio katika kombe la ligi la ulaya mambo yote haya yanamfanya kutumika sana katika ngazi zote.

Majeraha hayo haijulikani yatamweka kwa muda gani zaidi ya kuelezwa kuwa ataikosa mechi ya keshokutwa dhidi ya Totenham na mchezo huo na miwili ijayo inayofanyika nyumbani kwao.

Itakumbukwa pia Chelsea wana michezo mingine migumu ikiwamo dhidi ya Buyern Munich UEFA na wa ligi unaofuata ni dhidi ya Liverpool hivyo kumkosa kiungo huyu mkabaji ni pigo kwao.

Alifanyiwa uchunguzi wa kimwili wa kitabibu, na vipimo vingine pamoja na kile kipimo cha picha za skani za MRI ambayo ndiyo ilibaini kupata majeraja ya misuli hiyo ambayo ukubwa wa jeraha si rahisi kubainika na vipimo vingine.

Misuli hii ni tofauti na misuli ile ya nyuma ya paja ijulikanayo kama Hamstring Muscles ambayo ndiyo inaongoza zaidi kujeruhiwa kwa wachezaji wa soka.

Yenyewe Misuli ya Adductor ipo ndani kabisa katikati ikijichimbia katika kiuno sehemu ya chini pembeni kwenye kinene (groin) kazi yake kuupeleka mguu pembeni au mguu upande.

Mtindo wa ukabaji wa viungo wa kati unajulikana sana kwa kutumia mtindo wa kukwea kwa daluga ili kupokonya mpira na huku wakiwa katika kasi na kukumbana kimwili na wapinzani wao.

Hivyo aina ya ukabaji pamoja na nafasi anayochezea ambayo ni kawaida pia kubadilika na kuwa kiungo mshambuliaji katika eneo la kati au pembeni kama winga kunamweka katika hatari ya kujeruhiwa.

Mtakumbuka moja ya mbinu ambayo kocha wa zamani wa Chelsea Maurizio Sarri aliifanya alikuwa akimpanga Kante winga wa kulia zaidi badala ya kumweka kama kiungo wa kati.

Kwa namna moja au nyingine ilikuwa ni mbinu ya kumlinda mchezaji huyu asipate majeraha au kumlinda asijijeruhi tena ilihali muda si mrefu alitoka kupona majeraha ya awali.

Taarifa za jopo la madaktari wa klabu hiyo imaishaweka wazi kuwa majeraha hayo hayataihitaji upasuaji wowote zaidi ya kupewa muda mwingi akipumzuka na kuacha jeraha kuunga lenyewe.

Ingawa wamesema kuwa atakuwa katika uangalizi wa karibu na vile vile vipimo vitaendelea kufanyika kuangalia upigaji hatua wa uponaji wa misuli hiyo.

Tusubiri tuone uponaji wa jeraha hili kwa Kiungo huyo ambaye anatajwa kuhitaji kwa udi na uvumba na kocha wa klabu ya Real Madrid Zenedine Zidane.