SIO ZENGWE: Kwa Morrison tulifikiri kwa kutumia midomo

NILIPOSOMA taarifa za tamko la Yanga kuhusu winga wa Ghana, Berbard Morrison kuwa mkataba wake uliopandishwa katika mtandao wa usajili kimataifa (Transfer Matching System), una makosa, nikaona kabisa kuwa Shirikisho la Soka (TFF) litakuwa likifanya jitihada kutafuta maelezo ya kutosha kukabili yale yaliyotolewa na Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji.

Nilijua kutakuwa na kazi kubwa ya kutafuta maelezo ya kuhalalisha uamuzi wa kamati hiyo na palepale kuhalalisha usajili ya winga huyo katika klabu ya Simba. Ni dhahiri kuwa kwa kanuni tulizozichezea kwa matendo yetu, tukatumia midomo kutetea kilichofanyika, Simba haitaathirika kwa uamuzi wowote utakaobainisha kuwa kile kilichopandishwa TMS si mkataba, yaani hakina pande zilizokubaliana kiasi cha hizo nyaraka kuwa na sifa ya kuwa mkataba.

Kwa kutumia midomo kufikiri, tulirekebisha kanuni ambayo ni ya dunia nzima ya kuipokonya timu pointi pale inapobainika ilimtumia mchezaji ambaye hakustahili (ineligible player). Hoja zetu midomoni ni kwamba ushindi wa mezani hauko duniani kote, lakini kiuhalisia ni kwamba wenzetu wanahakikisha makosa yote yanayoweza kusababisha timu kumchezesha mchezaji ambaye ana kasoro, yanatatuliwa hata kabla ya kushuka uwanjani.

Iwe anasubiri kibali cha kazi, mkataba haujakamilika, hana uhamisho halali kutoka klabu yake ya zamani na mambo mengine yote hutafutiwa ufumbuzi kabla ya kocha kuruhusiwa kumtumia.

Pengine timu ya mwisho Ulaya kupokonywa pointi kwa kuchezesha wachezaji ambao ni ‘ineligible’ ni Sion FC ya Uswisi ambayo mwaka 2011 iliiondoa Celtic ya Scotland kwa jumla ya mabao 3-1 katika michuano ya awali ya Europa League, lakini UEFA ikaipokonya ushindi huo na kuipa Celtic.

Sion ilikuwa imechezesha wachezaji ambao iliwasajili wakati ikitumikia adhabu ya kuzuiwa kusajili iliyopewa na FIFA. Hata hivyo, mahakama ya Uswisi ilihalalisha wachezaji hao kucheza mechi za ligi ya nchi hiyo.

Kwa hiyo, kwa kanuni tulizozibadili kwa kutumia fikra za midomo, hakutakuwa na adhabu yoyote mbaya kwa Morrison au Simba kwa sababu tulishaamua kwenda kinyume na uendeshaji soka duniani. Kwamba Yanga ikibahatika kumtumia Lionel Messi katika mechi yake muhimu ya kuamua bingwa, haitapokonywa pointi itakapobainika kuwa Muargentina huyo alipewa leseni kimakosa, badala yake ataadhibiwa Messi kwa kuwa TFF ndiyo iliyomruhusu!

Messi akiadhibiwa, kuna tatizo gani wakati mechi muhimu imeshaisha na ushindi umepatikana? Kutumia midomo kufikiri!

Kimsingi, naona Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji iliboronga kwa kuchukua uamuzi ule wa kubatilisha mkataba “eti” kwa sababu kulikuwa na kasoro. Kukwepa kuamua hoja ya msingi kuwa kuna mkataba au hakuna, pia ni kufikiri kwa kutumia midomo.

Ni dhahiri kuwa kama ikizingatiwa rejeo au kisheria wanavyosema precedence, uamuzi wa kubatilisha mkataba wa Morrison, Yanga ndio unatakiwa kubatilisha mkataba wake Simba. Kama uamuzi ule ulikuwa makini, kasoro zilizoko katika mkataba wa sasa ni kubwa kuliko zile zilizokuwa katika mkataba wa Yanga.

Kwamba ni mtu mmoja tu amesaini, maana yake hakuna mkataba. Hivyo kamati ileile ikikutana leo sijui kama Hanspope atahusishwa baada ya kosa lile inatazamiwa iseme uamuzi uliochukuliwa na kamati awali, umekuwa ‘precedent’ na hivyo unailazimisha kamati ichukue uamuzi kama huo katika sakata jipya.

Hapo ndipo litakuja suala la adhabu. Yaani TFF ifuate kanuni kuu ya soka duniani kwamba Simba ipokonywe pointi zote ambazo Morrison alihusika?

Na kama ilivyokuwa kwa Sion, makosa hayo yatamaanisha nini kwa Simba na Morrison katika mechi za Ligi ya Mabingwa wa Afrika? Sion iliruhusiwa kutumia wachezaji wale katika ligi ya nyumbani, lakini ikapokonywa ushindi ilipowachezesha michuano ya Ulaya.

Tutumie akili kufikiri badala ya kufanya uamuzi kwanza na baadaye kuanza kutafuta maneno ya kuutetea.