SIO ZENGWE: Kuna tofauti ndogo sana ya klabu kubwa, ndogo

Monday September 14 2020

 

By ANGETILE OSIAH

MSIMU mpya wa soka Tanzania umeanza wiki iliyopita kwa mashabiki kuona matokeo tofauti na jinsi klabu kubwa tatu za Azam, Simba na Yanga zikifanya kazi za ziada kuibuka na ushindi au kulazimisha sare.

Kwa jinsi msimu wa usajili ulivyojaa habari kuhusu aina ya wachezaji walioletwa, ungeweza kudhania kuwa timu nyingine zisubiri vipigo tu au kushindana zenyewe, lakini si dhidi ya vigogo hao.

Kuanzia wachezaji majina kutoka Brazil, Ghana, Msumbiji, Angola, Kenya, Uganda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Burkina Faso, Rwanda na Burundi walitawala vichwa vya habari na magazeti na mijadala ya redioni, katika televisheni na mitandao ya kijamii kiasi kwamba ungeweza kudhania hakuna timu ingeambulia pointi dhidi ya vigogo hao.

Lakini ukiacha timu ya Manispaa ya Kinondoni iliyoibuka na ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Mbeyas City, ushindi mwingine ulikuwa wa jasho wa tofauti ya bao moja, achilia mbali kasoro za uamuzi ambazo zingeweza kusababisha ushindi kuwa wa timu chache katika mechi za fungua dimba.

Ingawa kuna timu zilifanya kazi ya ziada kulinda malango yao zisichakazwe vibaya, lakini ukweli kwamba zilimudu kuzuia nyavu zao zisitikiswe hovyo unatosha kutueleza kuwa pengine tulizidisha sifa dhidi ya wageni na kudharau uwezo wa wazawa.

Na kikubwa zaidi timu kama Prisons, Ihefu, Coastal Union zilifanikiwa kuonyesha udhaifu wa timu kubwa katika ngome zao na katika kutembea pamoja, inapofika wakati zinapokonywa mpira na kukutana na mashambulizi ya kushtukiza.

Advertisement

Mbali na kumudu kutochakazwa, timu hizi ‘ndogo’ zimeonyesha zina wachezaji wazuri waliostahili sifa, pengine kuliko nyota wengi waliosajiliwa kwa mbwembwe na kusababisha watu kutukanana mitandaoni.

Kwa kifupi kuna tofauti ndogo sana kati ya klabu zetu kubwa na hizi nyingine tunazoziita ndogo. Na pengine tofauti hiyo husababishwa na uamuzi mbovu, ambao husababisha mshindi kupatikana, na hata pengine kuzuia kipigo kwa timu zetu kubwa.

Kwa kifupi mechi za raundi ya kwanza na baadhi ya za raundi ya pili zinatufikirisha. Baadhi wanaweza kusema kuwa kwa kuwa ndio mwanzo wa msimu, timu kubwa zimeshindwa kuonyesha uwezo wao au kutumia kale kamsemo kalikoanza kupata umaarufu siku hizi; “timu bado haijakuwa na MUUNGANIKO”.

Yule Mwamnyeto aliyekuwa Coastal Union, hakusifiwa kama anavyosifika sasa wakati uchezaji wake ni uleule. Haujaendelea kwa sababu amejiunga na Yanga. Ni sababu gani zilimfanya asisifike sana kila Coastal Union ilipocheza?

Hali ni kama hiyo kwa wazawa wengine kibao ambao waling’ara na klabu zao msimu uliopita bila ya kupata sifa zinazostahili katika vyombo vya habari.

Kwa hiyo kama Mwamnyeto ni yuleyule na anacheza vilevile hivi sasa akiwa Yanga, maana yake kinachobadilika ni kusifiwa na media tu na si uwezo wake uwanjani. Na hii inanipa mimi majumuisho kuwa hakuna tofauti kati ya hizi timu tunazozisifia hadi kutukanana, na hizi ambazo hata zikicheza bila kiingilio, hatujisumbui kwenda kuziona.

Wakati mwingine matarajio makubwa hujengwa na klabu na mashabiki, wakati katika hali halisi mambo ni ya kawaida sana.

Kuna haja ya kuangalia kwa kina nje ya Simba, Yanga na Azam. Nadhani kuna makubwa zaidi yanayoweza kutupa burudani kubwa iliyofichika na inayoweza kusaidia hata taifa.

Nasema hivi kwa sababu kila kocha mgeni akija kufundisha timu ya taifa, huita wachezaji nje ya klabu hizo kubwa ambao hatujawahi hata kuwafikiria. Na anapowaingiza katika kikosi cha kwanza, macho yote huelekezwa kwake ili timu inaposhindwa tu, lawama zote zihamie kwa kocha kuwa alichezesha wachezaji wasio na uwezo.

Hakuna kocha wa nje ambaye tulimkosoa kwa staili au aina yake ya mchezo, bali kwa uteuzi wa kikosi cha kwanza. Na mara nyingi, hukosolewa pale anapowaacha wale nyota walio katika klabu hizo kwa sababu ndio tunaowaona kila mara na tunapoteza muda mwingi kuwafuatilia.

Kuna haja ya kugeuzia macho kwingine.

 

 

 

Advertisement