SIO ZENGWE: Kama wilayani soka halichezwi, tunategemea nini

Monday October 12 2020

By ANGETILE OSIAH

Nimekuwa nafuatilia habari za michezo magazetini, redioni, katika televisheni na mitandao yetu kupata habari motomto na za kina kuhusu burudani yetu inayotufanya tukose raha pale tunapoikosa.

Kitu kimoja naona hakipumziki wala kuisha ni michuano ya mitaani, maarufu kama ndondo, harage au jina jingine lolote lile linalohalalisha mtu kucheza kwa dakika kadhaa na baadaye kupata ujira wa muda usijue kesho utapata wapi mwingine.

Kwa kawaida michuano hii ya ndondo imekuwepo kwa miaka mingi, zamani ikilenga kukutanisha vijana wa mtaa fulani au eneo fulani.

Ilikuwa ikifanyika wakati ligi zimesimama hivyo kuwapa nafasi kaka zetu waliobahatika kupata timu kubwa, wengine waliokuwa shuleni na vyuoni kuungana na waliobaki mtaani kuunda timu ya mtaa kupambana na mitaa mingine.

Ilikuwa inaunda mchanganyiko bora. Fikiria yule kaka aliyekuwa akicheza Avengers na kupata nafasi ya kusajiliwa na klabu ya Pan African au Tumbaku ya Morogoro, amerudi mtaani kupumzika na kukutana na vijana wengine wawili au watatu waliokuwa timu ya kanda ya sekondari nao wamerudi likizo, changanya na wale waliobakia mtaani na kuendelea na mazoezi.

Ni lazima kunakuwa na uzoefu tofauti na ujuzi unaoufanya mtaa ujione bora kulinganisha na mitaa mingine. Mara nyingine, wale waliosajiliwa Ligi Kuu wakileta rafiki zao wawili au mmoja, timu inakuwa bora zaidi. Na huu ndio ulikuwa utamu wa mashindano hayo ya ndondo.

Advertisement

Ilianza kuharibika pale wale waliokuwa wakitaka ushindi zaidi kuliko burudani, waliotaka kujinufaisha kisiasa na ndondo au waliotaka kugeuza mashindano hayo kuwa tegemeo la maisha, walipoingia. Ndondo ikabaki kuwa si michuano ya kipindi cha likizo tena, bali msimu mzima.

Siku hizi ukichangishwa fedha kwa ajili ya timu ya mtaani, utashangaa unapofika kuangalia mechi huoni kijana hata mmoja unayemjua wa mtaani kwako. Zaidi ya hapo, kila mchezaji katika timu anamuita mwenzake ‘father’ kwa kuwa wamekutana uwanjani na hawatakuwa pamoja mechi ya kesho.

Haya ndiyo mashindano ya ndondo ya sasa. Watu wako bize na mpira lakini hawako bize na maendeleo ya mpira.

Naposikia kila siku kuna mashindano ya ndondo, hata wakati ligi zinaendelea, napata picha kuwa vyama vya soka vya wilaya havifanyi kazi yao ipasavyo.

Maana yake hakuna mashindano ya nguvu ya ngazi ya wilaya. Kanuni zinataka wilaya yenye timu kuanzia 10 iweze kuandaa ligi ya ubingwa wa wilaya. Naamini katika wilaya kuna timu zaidi ya 10 au 20, lakini hazina usajili kwa kuwa hazioni umuhimu wa kusajiliwa.

Zinachofanya ni kusubiri mashindano ya ndondo; kombe la mbuzi, kombe la diwani, kombe la mbunge, kombe la ng’ombe na mengineyo yenye majina kama hayo.

Ukitaka kusikiliza habari za ligi, basi ni kuanzia ligi ya mabingwa wa mikoa kwenda juu. Hawa vijana wanaochipukia wanapata nafasi wapi ya kushindana mashindano rasmi? Hawa wachezaji nyota wa klabu za ligi za juu wanastaafia wapi?

Wangekuwa na mchango mkubwa katika soka kama kungekuwa na ligi za wilaya ambako wangemalizia soka lao kwa kuchanganyika na vijana wanaochipukia na hivyo kuwapa ushauri na uzoefu wao.

Hawa vijana wanaotoka shuleni, wanachukuliwa na klabu zipi kama huku wilayani hakuna ligi rasmi, au ziko ligi za bora liende ili kupata wawakilishi?

Cha ajabu, hata viongozi wa soka wa wilaya ndio wanakuwa mstari wa mbele kuendesha mashindano ya ndondo wakisahau kuwa wana majukumu ya kuendesha ligi katika ngazi zao.

Tunaweza kulilaumu Shirikisho la Soka (TFF) kila tunapopata matokeo mabaya ya timu ya Taifa, lakini tunafanya nini katika ngazi yetu kushiriki kukuza vipaji na kuinua soka?

Ngazi ya wilaya ni sehemu muhimu sana katika maendeleo ya soka. Ndiko chimbuko la vipaji, ndiko mchezaji anatakiwa ajue ABC za mpira kwa kupata mafunzo sahihi kutoka kwa makocha sahihi.

 

Advertisement