SIO ZENGWE: Hii ya kutumia Azam Complex safi sana

KWA wiki za karibuni, mechi za kirafiki kati ya klabu za Ligi Kuu zimekuwa zikichezwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, uliopo pembezoni mwa jiji la Dar es Salaam.

Klabu kubwa za Yanga na Simba zimeamua kutumia uwanja huo kujipima nguvu dhidi ya timu za Zanzibar, hivyo kuweka msisimko wa pekee Mbagala, kwani wakazi wake wamekuwa wakishuhudia mechi za Azam peke inapocheza na timu nyingine—si Simba na Yanga.

Binafsi, hatua hiyo naiona kuwa ni kubwa katika maendeleo ya soka ambayo, si tu inapumzisha viwanja vikubwa viwili—Uwanja wa Benjamin Mkapa na Uwanja wa Uhuru—bali unabadili mazoea na utamaduni usiotakiwa wa mechi kuchezwa viwanja hivyo tu.

Jaribio la kupeleka mchezo kati ya Yanga na Azam, Mbagala lilipingwa vikali na mashabiki na wadau wengine muhimu. Sababu ya wengi kupinga mechi hiyo kuchezwa Mbagala ni udogo wa sehemu za mashabiki.

Kwamba mechi ya Yanga na Azam ni kubwa, hivyo ina mashabiki wengi ambao wangefurika kuitazama, hivyo ni lazima ichezwe Uwanja wa Benjamin Mkapa, ambao una uwezo wa kuchukua watu 60,000 waliokaa.

Hivyo, haki ya Azam kutumia na kunufaika na uwanja wake wa nyumbani, ikaporwa na mchezo ukarudishwa Uwanja wa Mkapa.

Sikuona kama jambo hilo lilijadiliwa kwa marefu na mapana yake na halijaibuliwa kuonyesha lilikuwa muhimu na lilihitaji mjadala mzito kuweka kupata ufumbuzi.

Ingawa ni kweli kwamba idadi ya watu Dar es Salaam inaongezeka. Lakini kabla ya Uwanja wa Mkapa kujengwa tulikuwa tunaangalia mechi Uwanja wa Uhuru, ambao miaka michache iliyopita uliongezewa uwezo wa kuchukua idadi kubwa ya watu. Lakini kabla ya hapo watu 15,000 tulikuwa tunafurika Uhuru kuangalia mechi na baadaye kuondoka zetu.

Kwa wale wengine waliokuwepo Dar es Salaam kitambo, vigogo hivyo tulikuwa tunaviangalia kwenye Uwanja wa Karume, ambao enzi hizo ulikuwa kama wa Azam.

Wakati Azam wameweka viti kwa kutumia vyuma, Uwanja wa Karume ulijengwa viti vya aina hiyohiyo kwa kutumia zege. Lakini uwezo wa idadi ya watu ulikuwa sawa na wa Azam.

Na enzi hizo tuliamini Karume ndio ulikuwa uwanja bora na mara chache tulienda Uwanja wa Uhuru, enzi hizo wa Taifa kushuhudia mechi kubwa.

Ni mazoea ndio yalitufanya tuamini hivyo na kujisikia tuko salama Uwanja wa Karume, achilia mbali ule wa Tandika Mabatini na Mburahati ambako vigogo hivyo pia vilikuwa wakienda.

Hivyo mazoea yanaweza kutuaminisha kuwa Simba na Azam haziwezi kucheza Azam Complex kwa sababu unachukua watu wachache.

Ni mazoea yanaweza kutuminisha leo hii kwamba Simba na Yanga haziwezi kucheza Uwanja wa Uhuru kwani ni mdogo kulinganisha na wa Mkapa, licha ya kwamba miaka michache iliyopita ndio ulioaminika kuwa unafaa kuliko Mbeya, Arusha na Mwanza (Nyamagana) ambako zimewahi kucheza.

Wapo wanaoenda uwanjani kwa sababu ni karibu. Kwamba akitoka kazini, au akimaliza kinywaji na wenzake, atakwenda uwanjani kwa sababu ni karibu, hatasumbuka. Huyu lazima apinge mechi kupelekwa Azam Complex kwa sababu ataona ni mbali, akizingatia foleni.

Lakini kwa kutafakari kwa kina, tunaweza kuachana na mazoea hayo na tukaamini kuwa Uwanja wa Azam unafaa kucheza mechi hizo kubwa kulingana na uwezo wake wa kuchukua mashabiki.

Kulingana na uwezo wake kunamaanisha kufanya maandalizi ya mechi kwa kuzingatia mengi; idadi ya watazamaji, kiingilio, usalama, umbali, matangazo na elimu kwa mashabiki.

Unapoamua kupeleka mechi Uwanja wa Azam, huwezi ukawa na maandalizi kama yanayofanana na yale ya kuchezea Uwanja wa Mkapa, lazima utakwama.

Kama kiingilio cha chini kwa Mkapa ni Sh 5,000 basi Azam kitakuwa tofauti. Kama utataka kiwe sawa, basi mazingira ya uuzwaji tiketi na udhibiti wa waingiaji ni lazima yabadilike.

Kwa hiyo, maendeleo ya mchezo hayaletwi na kuendelea kufanya vitu vilevile kwa njia ileile, bali kubadili mazoea na kukubali mambo mapya.

Hata wawekezaji, wanafurahishwa wanapoona miundombinu wanayowekeza kwa ajili ya soka, inatumiwa kikamilifu na kwa ufanisi.