SIO ZENGWE: Hapa Kocha Etienne Ndayiragije aliyumba

KILA kocha ana utamaduni wake wa kuzungumzia mikakati yake, staili, mfumo na mambo mengine kuhusu timu yake. Lakini kuna mambo ambayo makocha hulingana na kuonekana ndio utamaduni wa walimu wa soka, kama si mafunzo ya maadili.

Nilikuwa nasikiliza mahojiano na Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Etienne Ndayiragije mara baada ya kutangaza kikosi chake kwa ajili ya mechi ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya Burundi iliyofanyika zaidi ya wiki moja iliyopita.

Watangazaji walikuwa wakimhoji kuhusu uteuzi wake na nini anazingatia, lakini wasikilizaji walikuwa na hasira za kutoitwa kwa baadhi ya wachezaji, hasa Kibwana Shomari na Yassin Mustafa wa Yanga.

Imani ya mashabiki ilikuwa kwamba wawili hao wamecheza takriban mechi zote za mwanzoni mwa msimu za Yanga na ukuta wao umeruhusu bao moja tu na hivyo wanadhani walistahili kuitwa.

Ingawa mwanzoni Ndayiragije alikuwa ameweka vigezo anavyotumia kuteua wachezaji kama uwezo binafsi wa mchezaji mwenyewe, mbinu ambayo kocha mwenyewe anataka kuitumia na kuangalia timu gani anaenda kukutana nayo, alienda mbali zaidi kuzungumzia wachezaji hao.

Alisema beki wa pembeni ni lazima awe anahusika katika mabao, yaani kutoa pasi za mwisho na mambo mengine. Kibaya zaidi akazungumzia udhaifu wa Kibwana kwamba katika mechi dhidi ya Coastal Union mashambulizi yalikuwa yanapitia kwake.

Binafsi niliduwaa. Iweje kocha azungumzie udhaifu wa mchezaji ambaye hajamuita katika kikosi chake? Inawezekana kabisa kwamba wapo makocha wamewahi kufanya hivyo, lakini ni wachache sana.

Mara nyingi, makocha hujikita kuelezea uzuri wa wachezaji aliowaita tu kwa sababu ni kundi dogo kulinganisha na lile lililo nje ambalo hajaliita. Kocha akianza kuzungumzia wachezaji ambao hajawaita ni wengi sana na anaweza kuchukua hata mwaka mmoja anatoa maelezo tu ya sababu za kutoita wachezaji fulani.

Ni muhimu sana kocha kujikita katika wachezaji aliowaita kwa sababu ni wachache na ameona kitu fulani anachoweza kukizungumzia. Zaidi ya hapo, ana muda hata wa kurekebisha udhaifu wa yule aliyemuita kwa kuwa anakuwa ameona mengi mazuri.

Licha ya hivyo, mchezaji ambaye hayuko katika kikosi na ameelezewa udhaifu wake, kunaweza kukawepo na mawili. Kwanza kujenga hisia hasi dhidi ya kocha kwa udhaifu ambao pengine haujui, na pili inaweza kuwa changamoto kwake na kufanya jitihada za kujirekebisha.

Lakini udhaifu mwingine hutokana na jinsi timu inavyocheza na inavyojiweka mikakati yake, hivyo mfumo kusababisha aonekane mbovu.

Mchezaji akiwa na udhaifu, kocha anaweza kuzungumza naye pembeni kuliko kuuanika.

Suala la pili ambalo binafsi naona Ndayiragije alipotoka siku ile ni ile kauli yake dhidi ya makocha wengine. Kwamba amezunguka kuangalia mazoezi ya klabu za Ligi Kuu na kukuta Simba pekee ndio inayofanya mazoezi ya kufunga mabao!

Hivi hapa anaweza kuwa sahihi? Yaani makocha wa timu zote 18 hawafundishi kufunga mabao? Kama ni kweli kuna tatizo kubwa. Lakini alipata muda wa kuhudhuria session za timu zote na kugundua kuwa huwa hazina ratiba ya mbinu nyingine zaidi ya open space?

Kwa hiyo haya mabao ambayo Azam FC, KMC na klabu nyingine zinafunga yanatokana na bahati na si mipango ya timu?

Ni dhahiri kuwa kwa hili Ndayiragije anastahili kurekebisha kauli yake na ikiwezekana kuwataka radhi wataalamu wenzake kuwa midomo iliteleza kwa kuwa si rahisi kwa kocha aliyepata mafunzo, asijue kuna somo la kufundisha ufungaji.

Inawezekana alivutiwa na mazoezi ya Simba ya ufungaji au alienda siku ambayo ratiba ya Simba ilikuwa inahusu ufungaji, lakini alipoenda timu nyingine akakuta ratiba tofauti.

Rai yangu hapo ni kwamba ni lazima makocha wawe na heshima kwa wachezaji na wataaamu wenzao inapotokea wanazungumzia uzuri au udhaifu wa timu au mchezaji.

Kila la heri kocha wetu.