SIMBA MORRISON, YANGA SENZO; NANI ANAMFOKEA MWENZAKE?

Muktasari:

  • BERNAD MORRISON - Mshambuliaji huyu kabla ya kutua Yanga, aliwahi kukipiga Ashanti Gold, AS Vita Club, Odisha FC na Orlando Pirates F.C
  • SENZO MAZINGISA - Wakati mjadala juu ya kuondoka Simba ukiendelea, mtendaji huyu pia aliwahi kufanya kazi hiyo Orlando Pirates na Platinum Stars

SIMBA walianza kuichokonoa Yanga. Wakamtwaa fundi mtukutu, Bernard Morrison. Yanga wakajibu, wamembeba Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Senzo Masingiza. Basi, Kijiweni Luqman Maloto na Dk Levy wanazua zogo.

LUQMAN: Yanga ndio wamefikia hapa? Kipindi cha usajili wa wachezaji, wao wanasajili wakurugenzi. Wakifungwa tena 4 walie.

DK LEVY: Una uhakika gani kuwa wamemsajili? Au umekuwa mtabiri Au unaishi kwa stori za mitandaoni kama wapuuzi wengineo?

LUQMAN: Tangu lini ulianza kutoamini ninachosema?

DK LEVY: Nikuamini kwani umekuwa nabii? Halafu unabii unatimia kwa timu iliyoongozwa na kuongozwa na asilimia kubwa ya watuhumiwa wa mambo mbalimbali ya kijelajela?

LUQMAN: Acha kupaniki wewe. Yanga wapo makini na soka kweli? Simba wamsajili Morrison, mchezaji mwenye ufundi wa ki-intaneshno. Yanga eti wanamsajili Senzo, CEO. Yaani mkurugenzi tu wa klabu. Sasa yule Senzo atacheza soka? Badala kuimarisha timu, wao wanajenga fitina za uwanjani.

DK LEVY: Mlichofanya kama Simba mmesajili laini bila alama za vidole. Kitakachotokea ni kile kile cha Gadriel Michael, Ajibu na Niyonzima. Sisi ndo watalaam. Ulisikia waaaapi mchezaji toka Yanga akafanikiwa Simba? Ulisikia waaaapi? Ulisikia waaaapi? Ulisikia waaaapi? Morrison hatobooooiiii? Atageuka sanamu kama ya Askari pale katikati ya jiji. Mmeliwa pesa kibwege.

LUQMAN: Tulia uone kazi wewe. Morrison atawakalisha mpaka mtaomba poo. Hata kitendo cha Yanga kwenda kumvamia Senzo, ni uthibitisho kuwa wamepanic. Waambie Yanga wamerelaaaax.

DK LEVY: Morrison ni kituko. Tumeamua kuwaachia enyi Wagalilaya kutoka mto Jordan, ambao Wakolintho ma Waefeso waliwatenga kwa tabia zenu za Kirumi kutaka kuhodhi mamlaka zote Katika uso wa dunia. Enyi Wayahudi wa Mtaa wa Msimbazi, ni lini mtatosheka na watumwa wetu mlionao kwa pesa za mwanaume mmoja? Mimi nasimama na Mzee Hamis Kilomoni. Je, anachofanya Mo Dewji ndo thamani ya Simba kweli? Au mnaleta shobo dundo kwa kitu ambacho hakistahili? Kengepori nyie.

LUQMAN: Sasa matusi ya nini? HuweI kujenga hoja za kutetea timu yako? Yaani Morrison kakufilisi busara aisee.

DK LEVY: Nasimama na Kilomoni, Simba siyo ya kulegezwa na billioni ishirini ambayo kimsingi Kwanza haipo. Mo hajaweka pesa kwenye akaunti ya Simba. Bado ipo kwenye akaunti zake. Kwanza mkiamua kukagua akaunti ya Mo huwezi kukuta hata billioni moja. Kwa sababu utajiri wake ni kwa pesa ya MSHUA wake na siyo yeye. Yeye kama yeye anazidiwa mbali sana na Konde Boy. Je Diamond Platinumz atamgusia wapi?

LUQMAN: Sasa hayo maneno yote yanakupunguziaje machungu ya Morrison kwenda Simba?

DK LEVY: Unamfahamu mtu aliyepiga ngoma kumi. Ambazo zinaendelea kutumika mpaka leo kama kiashiria cha taarifa ya habari pale TBC Taifa?

LUQMAN: Kwani story ya Nyunyusa inakupunguziaje machungu ya Morrison kuikacha Yanga na kujiunga na timu ya kijanja, Simba.

DK LEVY: Naona unakwepa jina lake la mwanzo. Ene wei huyo huyo thamani yake ni kubwa sana. Lakini matumizi ya thamani yake hapa Bongo hayaendani na uzito anaostahili. Hilo linaweza kuwa kwa Yanga au Simba. Kwamba thamani ya Simba na anachofanya Mo Dewji hayaendani na thamani ya kilabu chenu. Simba ni kubwa sana huwezi kuiweka katika thamani ya billioni 20. Mbumbumbu Fc kawaida yenu kuingizwa mkenge.

LUQMAN: Kwa nini haya yote unayaleta kipindi hiki taifa la Tanzania linafurahia uamuzi wa busara wa Simba kumsajili Morrison?

DK LEVY: Kwa sababu Yanga imefanya mapinduzi iliyofanya Chelsea. Lakini kwa kuwa nyie ni vilaza hamuwezi kuelewa. Ashley Cole aliondoka pamoja na mkurugenzi wa ufundi wa Arsenal kwenda Chelsea. Unamfahamu huyo boss mwenyewe?

LUQMAN: Unadhani kuna nafuu yoyote Yanga wataipata kwa kujua jina la huyo mkurugenzi wako? Umeshapata picha jinsi Morrison atakavyowanyanyasa Yanga ndani ya uwanja!

DK LEVY: Kwa hiyo Morrison atacheza ma Yanga ligi nzima? Ujue we jamaa si ajabu umeshakuwa fyatu, ila itikadi yetu ya ujamaa ikawa inakisaidia sisi kushindwa kujua kuwa umeshakuwa mwehu... Unahitaji kwenda kwa mwalimu wa saikolojia. Hauko sawa sawa kichwani. Wewe ni ‘empte hedi paseee’.

LUQMAN: Kwani ukinitukana ndio Morrisona atarudi Yanga? Kweli Yanga mpya inatisha. Hivi huyo Senzo anakwenda kucheza namba ngapi pale Yanga?

DK LEVY: Kinachoniumiza naamini kuwa najadiliana na mtu timamu. Ila maongezi yanavyoendelea naona kama najadiliana na hayawani flan hivi amazing mwenye uzumbukuku na uzuzu wenye umbumbumbu ndani yake. Siku ukiwa na akili timamu utaelewa kuwa mafanikio ya Simba msimu uliopita yalitokea wapi.

LUQMAN: Simba chama kubwa. Sorry, taifa kubwa. MO aliweka mkwanja wa kutosha. Wacheza mali walanunuliwa. Tukawa na kocha mzuri. Mishahara kwa wachezaji na makocha ikalipwa kwa wakati. Kambi za maandalizi Afrika Kusini. Wachezaji wazuri, wanalala pazuri, wanakula pazuri. Ulitegemeaje?

DK LEVY: Siyo kwa Mapenzi yangu.Ila ukweli ni kwamba kuna wakati mtu hujui usinamie ukweli au uongo. Hebu kwenye hili nisimamie ukweli au uongo. Maana nimeandika nimefuta zaidi ya mara 58.

LUQMAN: Yaani nikikupa jibu ndio itakupunguzia sononeko la Simba kumchukua Morrison? Sikia, Yanga wamemsajili Senzo akacheze soka au akawape siri za fedha za MO zinavyotumika kusajili wachezaji mali pale Simba?