SHIKAMKONO : Kigogo huyu wa Yanga ni Simba wa kutupwa

Monday February 11 2019

 

LEO Jumatatu tunaendelea na makala haya kati ya mwandishi wetu na Jabir Ally Shikamkono yaliyofanyika wiki iliyopita kijijini Gomero, Kisaki mkoani Morogoro.

Shikamkono aliyekuwa mfadhali, mdhamini na mratibu wa Simba mwishoni mwa miaka ya 80, anakiri kufilisika kutokana na kutumia fedha zake zaidi ya Dola 100,000 alizotokanazo Uarabuni kuihudumia klabu hiyo katika kulipa mishahara, posho za wachezaji na kufanya usajili. Mbali na hayo pia, Shikamkono alihakikisha timu hiyo inakwenda kucheza Ligi Daraja la Kwanza (sasa Ligi Kuu) katika kila mkoa.

Shikamkono alihakikisha timu inakaa kambini, kula na kufanya kila kitu kama anavyofanya Mohammed Dewji ‘MO’ hivi sasa.

Katika mfululizo wa makala haya, Shikamkono anamtaja kiongozi mmoja ambaye amepata umaarufu mkubwa akiwa na Yanga kuwa ni Simba wa kutupwa lakini watu hawajui.

“Nilishangaa kumuona yule bwana akiwa kiongozi wa Yanga,” anaanza kusema tajiri huyo wa zamani wa Simba.

“Alitufuata na kutuomba tumsaidie kuweza kuidhamini na kuifadhili Simba au hata aweze kupata uongozi kwenye klabu yetu,” anafichukua na kumtaja jina mhusika huyo (Mwanaspoti linahifadhi jina lake).

“Wakati anakuja tayari Azim Dewji alishachukua majukumu ya kuidhamini na kuifadhili Simba, ikawa vigumu kwake kuweza kupata nafasi hiyo.

“Tulichomwambia labda aende kutafuta kitu kingine cha kukidhamini lakini sio Simba Sports. Akaenda kwenye mambo mengine kisha akaibukia Yanga, hilo lilinishangaza sana.”

Kama vile haitoshi, Shika mkono anasema mtu huyo pamoja na kuwa Simba, alipoenda Yanga amebadilika sana na ameitetendea vibaya sana Simba katika uongozi wake mbalimbali.

“Sijui huwa wanapewa nini kule Yanga, kila Simba ambaye unayemjua wewe akienda Yanga anabadilika na kuwa Yanga lakini kila Yanga anayekuja kwenye timu yetu na kujifanya Simba, huwa anatuumiza.”

Hapa Shikamkono anatoa mifano ya watu wengi ambao wameisadia Yanga wakiwa ndani ya Simba lakini kutokana na maadili ya habari hatuwezi kuwaanika gazetini.

DEWJI AWAKATAA DUA, SHABAAN

Aidha Shikamkono anafichua kitu kingine ambacho kilimpa wakati mgumu chini ya aliyekuwa mdhamini wa Simba, Azim Dewji aliyechukuwa timu kuanzia mwaka 1990.

“Dewji hakuwataka wachezaji wawili, Shabaan Ramadhani na Dua Said wasajiliwe na Simba. Nilipata tabu sana kwa hawa ambao Dewji aliwakataa kabisa.

Shikamkono anafichua, Shabaan Ramadhani alisema hatiki pesa kwa kuwa yeye anaipenda Simba hakutaka kulipwa pesa za usajili.

“Azim alinihoji, mchezaji gani hataki pesa wakati dunia ya sasa imebadilika kila mtu anataka pesa? Tena alikuwa na wasiwasi na afya yake kwa kuwa alikuwa anaonekana amedhoofu,” anasema.

“Nilimsisitiza sana Azim akubali kwa kuwa ilikuwa ni siku ya mwisho ya usajili hadi saa 6 na dakika 20 ndipo alipokubali kuwasajili wachezaji hao. Ninachoshukuru walicheza kwa mafanikio makubwa ndani ya klabu.

ANYANG’ANYWA GARI NA DEWJI

Kama vile haitoshi, Shikamkono anafichua kilichoifanya Simba imsajili kipa Steven Nemes kutoka Yanga.

“Unajua kipa namba moja wa Simba wakati ule alikuwa ni Mohammed Mwameja. Sasa kuna mechi tulicheza na Yanga tukafungwa bao 1-0. Bao la Mkapa (Keneth Pius) Aprili 12, 1992.

“Bao lile lilimvuruga sana Dewji, alihisi labda Mwameja amefungisha kwa makusudi. Pia, alihisi kipa huyo amekuwa tegemeo sana kwa timu hivyo alifanya anavyotaka, hivyo akataka apatikane mbadala wake.

“Nilimkatalia kuhusu Mwameja kufungisha. Na nikamtaka asichukue uamuzi wowote mbaya kuhusu kipa huyo. Ila nilimkubalia kumchukua Nemes. Kuna wakati tulifikia kutoelewana kabisa na Dewji.

“Siku moja (Dewji) alikuja nyumbani kwangu kwa hasira. Na kugonga geti kwa nguvu. Haikuwa tabia yake nilipomuona nilishangaa sana kufanya vile. Ishu ilikuwa hiyohiyo ya Mwameja, tulienda kuizungumza lakini hatukuelewana. Aliamua kuninyang’anya gari lake….Nikampatia funguo.

“Siku zote mimi na Dewji tulikuwa tunataniana yeye alikuwa akisema watu wafupi hawana akili na mimi nilimwambia watu warefu akili wameziacha chini.

“Nilikodi teksi nikarudi nyumbani, nikamwambia mke wangu kilichotokea. Basi jioni Dewji akaenda kwenye msikiti wao, walikuwa wakimwita rais, akawaambia wenzake kilichotokea. Hawakufurahi wakamwambia amekosea.

“Usiku uleule Dewji alikuja nyumbani tena. Safari hii akapiga honi kiustaarabu. Nikaenda kumsikiliza. Aliniambia kumbe wakati mwingine watu wafupi wanakuwa na akili. Tukacheka yakaisha. Akanipa funguo za gari.

NEMES AMKUBALI MWAMEJA

Hata hivyo, Shikamkono anasema kuna wakati alizungumza na Nemes mazoezini kuhusu Mwameja akakiri hamuwezi kipa huyo.

“Nemes aliniambia yule jamaa (Mwameja) ni kama mnyama anapofanya mazoezi yake, hataki masihala kabisa,” anasema Shikamkono.Kitu gani kiliiponza Simba kufungwa na Stella Abjan 1993? Usikose kesho Jumanne.

Advertisement