SHARO WA KIHAYA: Amwangusha JPM kwa kicheko

Saturday November 24 2018

 

By Saddam Sadick

Jana Ijumaa tulianza kumsikia Sharo wa Kihaya akielezea maisha yake hadi kuingia kwenye sanaa na jinsi alivyokimbiwa na mpenzi wake kisa sanaa ya vichekesho ambayo kwa sasa imempaisha na kuweza kupata mafanikio.
Leo tunaendelea na sehemu nyingine na Sharo anaelezea mafanikio na changamoto alizopitia kabla na baada ya kuingia kwenye sanaa na mambo mengine yaliyomfanya azidi kuja juu japokuwa anasema kuna ushindani mkubwa. Pia anaweka wazi juu ya matarajio yake na jinsi familia yake ilivyomsapoti. Endelea naye...

Mafanikio yake
Kweyamba anasema pamoja na kuwa bado hajafikia kiwango anachohitaji lakini hawezi kukufuru kwani hadi sasa amefanikiwa kuwa na mtaji wa watu na familia ya mke na mtoto mmoja.
Anasema kuwa mbali na hivyo,pia anaendelea na ujenzi,huku mtoto wake Prochea Privatus akiwa anaendelea vyema shuleni na kwamba kwa sasa anaendelea kufanya mipango kusaka wadau ili kufika mbali zaidi.
“Mafanikio yapo japo si makubwa,ila najivunia kujulikana kwa watu lakini nimepata familia ya mke na mtoto mmoja ambaye anasoma shule.Pia nimeanza kujenga nyumba yangu na ninafanya mchakato wa kutafuta wadau wenye kunipa sapoti ili nifike mbali zaidi,” anasema Kweyamba.

Familia kumbe inamuelewa sana
Mkali huyu kwenye uchekeshaji anasema kuwa kinachompa nguvu zaidi kwenye kazi hiyo ni jinsi familia yake na majirani zake wanavyomkubali katika ubinifu wake.
Anasema kuwa anapokuwa nyumbani amepumzika na familia huku wakiangalia kazi yake kwenye TV huwa wanavutiwa sana na muda mwingine mke wake humshauri jinsi ya kuongeza ‘manjonjo’ ili kuwavutia wengine zaidi.
Anaeleza hata majirani zake nao hawana taabu kwani kazi yake wanaipenda na mara kadhaa hufuatilia anachofanya na kuongeza kuwa jambo hilo humuongezea nguvu katika kubuni mambo mapya.
“Familia yangu hata majirani hawana noma kabisa,kuna muda mke wangu hunishauri kuongeza ujuzi zaidi ili kuendelea kuwavutia wengi kwa hiyo kupitia hapo Napata nguvu,” anasema mchekeshaji huyo.

Changamoto
Staa huyu anasema kuwa moja ya changamoto katika tasnia ya Sanaa ni masilahi duni kutokana na kazi ngumu wanayofanya na mwisho kulipwa pesa ndogo na kuishia kula,kunywa na kulala.
Anasema tatizo jingine ni kukosa ufadhili kwa wadau, taasisi na kampuni ambazo muda mwingi hupenda mafanikio ya haraka bila kufikiria mzunguko wa kazi yenyewe.
“Kutokana na maslahi kuwa madogo husababisha hata kazi zenyewe kuwa na mapungufu,lakini mimi napambana ili mashabiki wangu wandelee kupata kilichobora zaidi,ufadhiri unakuwa mgumu wengi hutaka mafanikio ya haraka”anasema.
Hatosahau matukio haya
Kweyamba anasema kuwa katika maisha yake kwanza hataweza kusahau tukio la masikitiko la kufiwa na msanii mwenzake,Karume Kenge aliyefia mikononi mwake hivi karibuni.
Anasema kuwa kwa kipindi chote marehemu huyo wakati anaumwa alikuwa naye karibu na siku ya kifo chake alikuwa naye tukio ambalo hataweza kulisahau.
Anasema kuwa katika uhai wa Kenge, alikuwa na upendo kwenye kundi la Futuhi lakini hata jamii kwa ujumla hivyo atamkumbuka milele kutokana na mwenendo mzuri aliokuwa nao.
“Tukio ambalo sitakaa kusahau ni kufiwa kwa msanii mwenzangu,Kenge ambaye alifia mikononi mwangu wakati nikumuhudumia,kwa ujumla niliumia na sitasahau,” anasema.
Anaongeza, tukio lingine ambalo hawezi kusahau ni wakati wa kampeni za Uchaguzi mwaka 2015 wakati wakiwa kwenye ziara na Rais John Magufuli na moja ya shoo waliyoifanya Kiongozi huyo alicheka hadi kuanguka akiwa jukwaani.
Anasema kuwa kipindi hicho walikuwa wilayani Musoma mkoani Mara, mamia waliokuwa wamefurika uwanjani hapo kusikiliza sera Rais huyo walifanya igizo moja matata ambalo Magufuli alishindwa kuhimili na kujikuta akicheka hadi kuanguka.
“Tukio la kufurahisha ambalo nalikumbuka ni mwaka 2015 wakati wa kampeni za uchaguzi Mkuu,ambapo siku hiyo tukiwa na Rais Magufuli mkoani Mara tulifanya shoo moja ambayo ilimfanya kiongozi huyo acheke hadi kuanguka,” anasema huku akicheka na yeye.

Ushindani kwenye Sanaa
Mchekeshaji huyu anakiri kuwa ushindani kwa sasa kwenye tasnia ya filamu ni mkubwa na hilo linamfanya kuwa na mbinu binafsi ya kuweza kuwazidi wapinzani.
Anasema kuwa katika kundi la Futuhi wakiongozwa na Brother K,wamekuwa na ubinifu mkubwa ili kuweza kuwazidi makundi mengine kutokana na hali ya sasa ya utandawazi.
“Ushindani upo sana na hii inatufanya sisi kundi la Futuhi kuwa na mambo mapya kila siku ili kutofautiana na makundi mengine, ukizingatia soko na utandawazi lazima tuwe na mbinu tofauti zenye ushawishi,” anasema Shalo.

Kuhusu mavazi yake
Kama ambavyo huonekana katika filamu na mavazi ya uchekeshaji,Kweyamba anafafanua kuwa mavazi hayo wala hayana bei yoyote na hayapatikani mbali.
Anasema yeye huingia masokoni na kuchagua ambayo yanaendana na kipindi chake na bei yake huwa ni kuanzia Sh4,000,5,000 hadi 10,000.
“Nguo zangu mbona za kawaida tu,hata bei nikikwambia unacheka.Mara nyingi nanunua kwenye masoko ya hapa Mwanza haswa kule Mlango Mmoja na Soko Kuu na bei huwa haizidi Sh 10,000,” anasema msanii huyo.

Joti na Brother K wamkuna
Moja ya wasanii kwenye uchekeshaji aliowataja Shalobaro kuwa wanamvutia katika kazi hiyo ni Lucas Lazaro ‘Joti’ na Andrew Ngonyani ‘Brother K’ na kwamba wawili hao ni funga kazi.
Anasema kuwa anapokuwa na Brother K kwenye muvi yoyote hujisi furaha kwani huamini kuwa kazi yao itaenda vizuri kutokana na ubora wa msanii huyo katika uchekeshaji.
Anasema kuwa hadi sasa licha ya kwamba amepiga hatua katika masuala ya Filamu,lakini bado hajafikia kiwango anachotaka na ndoto zake ni kumfikia Joti.
“Kwa Wasanii wa Filamu nawapenda Joti na Brother K na tunapokuwa kazini huwa najisikia vizuri,lakini bado sijafikia kiwango nachotaka kwa sababu nina ndoto za kumfikia Joti,” anasema Shalobaro.

Awaahidi makubwa mashabiki
Mvunjambavu huyo anasema kuwa mwakani anatarajia kuangusha moja ya filamu ambayo mashabiki wake wataikubali na kwamba huenda akamshirikisha Joti.
Anasema kuwa kutokana na mipango yake anatarajia kutengeneza kitu ambacho kitaacha historia kwenye maisha yake na kuzitoa hofu Kampuni na wadau wanaotaka kutangaza na yeye kuwa milango ipo wazi.
Anasema licha ya kwamba hajafikiria kustaafu kwenye kazi yake hiyo, lakini muda wowote akiona mambo hayaendi vizuri anaweza kupumzika na kuendelea na mishe nyingine.
“Mwakani natarajia kutoa kitu kipya ambacho kitakuwa na wahusika wengi wenye uwezo kama Joti na wengine, suala la kustaafu ni muda wowote, pia niwatoe hofu wenye nia ya kutangaza na mimi nawakaribisha,” anasema Shalobaro wa Kihaya.

Advertisement