SANCHO NGOMA BADO MBICHI

MANCHESTER, ENGLAND. MANCHESTER United mpo? Zile kelele zote za kuhusu Jadon Sancho zimegoma kutimia baada ya siku ya mwisho iliyopangwa na Borussia Dortmund kumaliza dili la mchezaji huyo kufikia na miamba hiyo ya Old Trafford kushindwa kutoa mkwanja wa kumaliza biashara.

Staa Sancho amejumuishwa kwenye kikosi cha Borussia Dortmund kitakachokwenda Uswisi kwenye mechi za kujiandaa na msimu mpya. Miamba hiyo ya Bundesliga huko nyuma iliripotiwa kuwaambia Man United kwamba wafanye kila wanaloweza kuhakikisha wanamaliza dili la kumsajili Sancho hadi kufikia Agosti 10, ambayo ni jana Jumatatu.

Lakini, miamba hiyo ya Old Trafford bado imegoma kukubaliana juu ya ada ya Pauni 108 milioni inayotaka kulipwa Dortmund.

Hata hivyo, hadi kufikia jana Jumatatu asubuhi hakuna dili lolote lililothibitishwa na hivyo, Dortmund ilimtangaza winga huyo kwenye kikosi chao kitakachokwenda Uswisi kwenye mechi za kujiandaa na msimu ujao. Kikosi hicho cha kocha Lucien Favre kitakakwenda kuweka kambi katika mji wa Bad Ragaz.

Na Sancho alipigwa picha akiwa na wachezaji wenzake walipokuwa uwanja wa ndege wakijiandaa na safari hiyo ya kwenda Uswisi jana Jumatatu asubuhi. Man United, ambao jana usiku walikuwa na shughuli ya kuwakabili Copenhagen kwenye robo fainali ya Europa League, wala hawajali maneno hayo ya Dortmund kwa sababu wanachojua wao ni kwamba dirisha la usajili lipo wazi hadi Oktoba 5.

Taarifa zilizopatikana Jumamosi iliyopita ni kwamba Man United haitaki kukubali kirahisi kulipa pesa ndefu kiasi hicho kunasa huduma ya Sancho pekee yake, wakati wanahitaji wachezaji wengine kibao kwenye dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi.

Lakini, kwa taarifa za kutoka Ujerumani zinadai kwamba Dortmund wamempa ofa Sancho ya kumwongeza mshahara na kwamba wanamlipa Pauni 173,000 kwa wiki kama atabaki kwenye kikosi. Huko Man United aliripotiwa kupewa ofa ya mkataba wa miaka mitano wenye thamani ya Pauni 340,000 kwa wiki.

Dortmund walisema kwamba wala hawana shida na ishu ya Sancho kushiriki kwenye pati huko Uingereza, huku ripoti nyingine ikidai kwamba winga huyo Mwingereza amejiunga kwenye grupu la WhatsApp la wachezaji wa Man United.