SAMATTA AANZA KULA BENCHI

YULE straika mpya wa Aston Villa, Ollie Watkins ameanza kwa kutupia katika mchezo wa kujiandaa na msimu mpya wa Ligi Kuu England dhidi ya Manchester United huku nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta akicheza kwa dakika 25.

Usiku wa Jumamosi, Aston Villa wakiwa nyumbani kwenye uwanja wao wa Villa Park waliikaribisha Manchester United, ikiwa ni sehemu kwa timu zote mbili kujiandaa na msimu huu wa Ligi Kuu England ambao tayari umeanza kutimua vumbi.

Katika mchezo huo, Manchester United wamekumbana na kipigo cha bao 1-0 walilofungwa katika dakika ya 38 na Ollie Watkins ambaye alianza kwenye safu ya ushambuliaji ya Aston Villa.

Straika huyo mpya wa Kiingereza, alicheza kwa dakika 65 na kutolewa huku nafasi yake akaingia Samatta ambaye ana mtihani mkubwa mbele yake kama ataendelea kuichezea klabu hiyo.

Kwa namna ambavyo alimwona Samatta katika dakika 25 alizocheza kwenye mchezo dhidi ya Manchester United, kocha Hafidhi Badru ambaye amekuwa akifundisha vijana kwenye akademi mbalimbali nchini humo, amemchambua nahodha huyo wa Taifa Stars.

“Samatta aliangushwa na ugeni hakuwa anaijua vizuri ilivyo Ligi Kuu England, alicheza vizuri na pengine kama angepewa muda zaidi alikuwa na uwezo wa kuifunga Manchester, ubora wake bado upo juu.

“Anapaswa kuwa na moyo mgumu kwa sababu presha kwake ni kubwa na ukizingatia alishapewa nafasi ya kutosha lakini mambo yakawa tofauti, nadhani wakati macho ya wengi yakiwa kwa Ollie naiona nafasi ndogo kwake ambayo anaweza kuitumia kuwaaminisha watu,” alisema,

Badru alisema kwa namna ambavyo ameongea na rafiki yake anayeishi Birmingham, Samatta anaweza kusalia kwenye klabu hiyo kwa msimu mwingine tena licha ya kuhusishwa kuwa anaweza kusepa Aston Villa baada ya kusajiliwa kwa Ollie.

“Wanaweza kucheza pamoja kule mbele kama Samatta ataonyesha kwa sababu namjua kuwa ni namba 10 mzuri,” alisema kocha huyo.

VIKOSI VILIVYOCHEZA

Aston Villa Villa: Steer; Cash, Konsa, Mings, Targett; Hourihane, Luiz, McGinn, Trezeguet, Watkins, Grealish.

Akiba: Nyland, Sinisalo, Taylor, Elmohamedy, Lansbury, Nkamba, El Ghazi, Guilbert, Hause, Jota, Ramsey, Samatta, Davis.

Manchester United: Henderson; Dalot, Fosu-Mensah, Maguire, Shaw; McTominay, van de Beek; Lingard, Rashford, James; Ighalo.

Akiba: Grant, Mengi, Williams, Galbraith, Garner, Elanga.

KAMPENI KUANZIA HAPA

Baada ya mchezo wao wa kwanza wa msimu wa Ligi Kuu England dhidi ya Manchester City kuahirishwa, Aston Villa watauanza rasmi msimu huu Septemba 15 kwa kucheza dhidi ya Burton katika Kombe la Ligi (EFL).

Septemba 21 watakuwa nyumbani baada ya kucheza dhidi ya Burton wakiwa ugenini, wakiikaribisha Sheffield Utd, utakuwa mchezo wao wa kwanza katika Ligi Kuu England (EPL).

MZEE ATOA BARAKA

Baba wa staa huyo, Ali Pazi amesema atapambana kubaki Villa.