SABABU TANO ZA KUMUONDOA SAMATTA ASTON VILLA

MARA baada ya Aston Villa inayoshiriki Ligi Kuu ya England, kukamilisha usajili wa straika, Ollie Watkins kutokea Brentford FC, inayoshiriki Ligi Daraja La Kwanza nchini humo zilivuma taarifa za Mtanzania Mbwana Samatta kuonyeshwa mlango wa kutokea.

Baada ya kuvuma kwa taarifa hizo kutoka katika mitandao mbalimbali ya kijamii, miamba ya soka la Uturuki, Besiktas wametajwa kuongoza mbio za kuiwania saini ya Samatta.

Anayeongoza mchakato wa kutaka kumvuta Samatta kutoka huko Villa Park, ambako inaonekana nafasi yake ya kucheza msimu ujao ni finyu, ametajwa kuwa ni Emre Kocadag ambaye ni miongoni mwa watu ambao wapo kwenye bodi ya Besiktas.

Mwanaspoti inakuletea sababu tano ambazo zinaweza kuchangia Samataa kung’oka katika viunga hivyo vya Villa Park na kwenda katika timu nyingine.

MFUMO

Kocha wa Aston Villa, Dean Smith msimu uliopita alikuwa anapenda kutumia straika mmoja katika mechi nyingi hadi timu hiyo inaponea kubaki katika ligi dakika za jioni.

Smith huenda alikuwa anatumia straika mmoja kutokana na timu yake kutokuwa na uwezo wa kufunga mabao mengi lakini inaruhusu kufungwa, jambo lililomsukuma kuongeza kiungo mwingine.

Awali, nafasi hiyo ya straika alikuwa anaanza, Mbrazil Wesley Moraes kabla ya kuumia na nafasi hiyo alikuja kupewa Samatta aliyejiunga na timu hiyo katika dirisha dogo.

Smith kama atarudi msimu huu na mfumo huo wa kutumia straika mmoja ni wazi chaguo la kwanza atakuwa, Watkins aliyesajiliwa kwa dau la Euro 30.8 milioni lililoweka rekodi kwa klabu hiyo wakati Samatta na wenzake watakuwa mbadala.

Samatta atakuwa anapata dakika chache kucheza tofauti na alivyomaliza msimu na kama ataweza kufunga mabao katika muda huo mfupi ndio itakuwa salama yake lakini kama ikiwa tofauti na hivyo katika dirisha dogo msimu ujao lolote linaweza kutokea.

KUSHINDWA KUFUNGA

Samatta ambaye usajili wake Aston Villa ulikuwa furaha kwa Watanzania wengi waliokuwa wakifatilia timu hiyo, ameitumikia katika mechi 16 za michuano yote na kuifungia mabao mawili - moja kwenye mechi 14 za EPL na jingine alifunga katika fainali ya Kombe la Ligi kwenye Uwanja wa Wembley dhidi ya Manchester City.

Nahodha huyo wa timu ya taifa ya Tanzania, alionekana kukosa hali ya kujiamini na muda mwingine hata kukosa nafasi za wazi na kuogopa hata kupiga mashuti au kucheza kama alipokuwa KRC Genk.

Uwezo na kasi ya kufunga mabao huenda ndio sababu iliyowavutia Aston Villa kumsajili Samatta ambaye alitisha hadi katika Ligi ya Mabingwa Ulaya akiwafunga bao tamu la kichwa Liverpool kwenye Uwanja wa Anfield ambako walikuwa na sifa ya kutoruhusu mabao wakati huo akiwa na Genk.

Hata hivyo, ugeni wa ligi, kutozoea mazingira, kukutana na wachezaji wapya, ushindani na vinginevyo huenda vilikuwa vikwazo kwa Samatta kushindwa kuonyesha makali yake katika miezi nane aliyoishi klabuni Aston Villa.

UBORA WA MASTRAIKA

Ukiachana na viungo kama nahodha wa timu, Jack Grealish ambao muda mwingine hutumika kama washambuliaji, kwa sasa Villa ina mastraika watano.

Mastraika hao ni Wesley ambaye bado ni majeruhi ambaye aliifungia Villa mabao matano katika mechi 21, mwingine, Muingereza Keinan Davis aliyefunga mabao mawili katika mechi 55.

Wengine ni Mbulgaria Indiana Vassilev aliyojiunga na timu hiyo, 2020 amecheza mechi nne hajafunga bao lolote, Samatta aliyecheza mechi 16 akifunga mabao mawili na Watkins, ambaye kutokana na usajili wake kuvunja rekodi anazamwa kuwa kama chaguo la kwanza. Watkins amecheza mechi mbili akiwa na Villa na amefunga mabao mawili - moja mechi ya kirafiki akiizamisha Manchester United 1-0 na jingine dhidi ya Burton Albion ya Ligi Daraja la Pili waliyoshinda 3-1 na kusonga mbele katika Kombe la Carabao. Katika mechi hiyo ya Jumanne, straika Davis aliingia ‘sub’ na kufunga bao la tatu, huku jingine likifungwa na Grealish.

Samatta ili aweze kubaki anatakiwa kuwa bora zaidi ya mastraika hao wote kwa maana kufunga mabao mengi kadri atakavyopata nafasi ya kucheza.

STAA MPYA

Ni wazi baada ya kusajiliwa kwa pesa nyingi, Watkins ndio atakuwa chaguo la kwanza lakini kama haitoshi straika huyo aliwahi kufanya kazi na kocha wa Villa, Smith walipokuwa wote Brentford.

Uwezo wa kufunga mabao 45, katika mechi 132 za timu hiyo ya Ligi Daraja la Kwanza ambayo ameitumikia tangu mwaka, 2017–2020 ni kati ya sababu nyingine anazamwa kuwa chaguo la kwanza na hivyo kupunguza muda wa kucheza kwa Samatta.

Ili Smith amuache nje Watkins au straika mwingine na kumpa nafasi Samatta anatakiwa kuuwasha moto wa kufunga mabao kama ilivyokuwa wakati yupo KRC Genk au TP Mazembe.

MKWANJA

Sababu nyingine ambayo inaweza kumuondoa Samatta katika viunga vya Villa Park kama uongozi wa timu hiyo utapata pesa nzuri ya kumuuza nyota huyo wa Tanzania kutoka katika timu nyingine.

Tayari kuna timu kama Besiktas zimeonyesha nia ya kumtaka Samatta kama watatoa mkwanja wa maana utakaokaribia ule Euro 10.5 milioni waliotumia kumsajili Aston Villa wanaweza kuuchukua.

MSIKIE KUMWEMBE

Mchambuzi wa masuala ya soka nchini, Edo Kumwembe amesema hadhani kama Samatta anaweza kuondoka Aston Villa kutokana na rekodi bora alizonazo dhidi ya mastraika wote anaowania nao namba.

Kumwembe anasema Samatta ambaye alifunga mabao 76 na kutoa asisti 20 katika mechi 191 alizoitumikia Genk ya Ubelgiji na kufunga mabao matatu katika mechi sita za Ligi ya Mabingwa Ulaya, ni rekodi bora ambazo hamna kati ya wapinzani wake wa namba pale Villa anayezifikia.

“Atarejea makali tu,” aliseam Edo.