Rwakatare, Mashaga watoswa rasmi OBFT

Muktasari:

Pamoja na kwamba hadi Novemba 14, ni mdau mmoja pekee alikuwa amejitokeza kuchukua fomu, vigogo hao hawana sifa za kurejea kutetea nafasi zao kwa mujibu wa Katiba.

Mbali na Lwakatare na Mashaga, aliyekuwa makamu wa rais, Lukelo Wililo pia amekosa sifa za kurejea kugombea tena.

Dar es Salaam. Aliyekuwa rais wa Shirikisho la ngumi za ridhaa, sasa ngumi za wazi (OBFT), Mutta Lwakatare na Katibu mkuu, Makore Mashaga 'wamepigwa pini' kurejea kutetea nafasi zao kwenye Uchaguzi mkuu utakaofanyika Desemba Mosi.

Pamoja na kwamba hadi Novemba 14, ni mdau mmoja pekee alikuwa amejitokeza kuchukua fomu, vigogo hao hawana sifa za kurejea kutetea nafasi zao kwa mujibu wa Katiba.

Mbali na Lwakatare na Mashaga, aliyekuwa makamu wa rais, Lukelo Wililo pia amekosa sifa za kurejea kugombea tena.

Ofisa Habari wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Najaha Bakari alisema viongozi walioongoza kwa misimu miwili ndani ya Shirikisho hilo hawaruhusiwi kugombea tena.

"Katiba ya OBFT hairuhusu kuongoza kwa misimu mitatu," alisema Najaha.

Vigogo hao walijitosa kugombea kwa mara nyingine Februari mwaka huu ambapo walibadilishaba, Mashaga safari hiyo  akiwania Umakamu wa rais huku Lukelo yeye akiwania ukatibu mkuu.

Lwakatare akitetea nafasi yake ya urais, lakini BMT ilizuia Uchaguzi huo siku ya mwisho ikidai wagombea wanaotetea nafasi zao hawana sifa za kugombea.