Roy Keane kumwita Becks bosi

Muktasari:

Keane anatajwa kama mtu mwenye misimamo na ubabe pindi mambo yanapokwenda tofauti hivyo, watu wanasubiri kwa hamu kuona akikabidhiwa Salford.

 

Manchester, England. HAYA ndio maisha buana. Mabosi wa klabu ya Salford ambayo inamilikiwa na kundi la wachezaji wa zamani wa Manchester United ambao ni marafiki maarufu kama Class of 92, wanajiandaa kumpa kazi nahodha wao Roy Keane.

Klabu ya Salford inamilikiwa kwa pamoja na Gary Neville, Phil Neville, Ryan Giggs, David Beckham, Paul Scholes na Nicky Butt na inashiriki Ligi Daraja la Pili.

Mabosi hao wamemfuta kazi kocha Graham Alexander jana Jumatatu ya Oktoba 12, 2020 na wanafikiria kumpa kazi ya kukinoa kikosi hicho Keane.

Hata hivyo, wakati mchakato wa kumpa Keane kibarua hicho ukianza, kwa sasa Scholes atakuwa kocha wa muda kuendeleza jahazi la kuwania nafasi ya kupanda hadi Championship msimu ujao.

Kwa sasa Salford iko nafasi ya tano kwenye msimamo ikishinda mechi tatu na kutoka sare mara mbili katika mechi tano ilizocheza mpaka sasa.

Keane akiwa ameongozana na Neville na Scholes alikuwepo kutazama mchezo wa Salford dhidi ya Tranmere ulioisha kwa sare ya mabao 2-2 ukiwa ndio wa mwisho kwa Alexander akiwa kocha kabla ya kufutwa kazi.

Kwa mujibu wa The Mirror, Keane anajiandaa kurejea kwenye kazi ya ukocha tangu alipoamua kujiweka kando mwaka 2018 wakati huo akiwa kocha msaidizi kwenye timu ya Taifa ya Ireland chini ya Martin O'Neill.

Kwa sasa Keane ni mchambuzi wa Sky Sports akiwa amepata kuzinoa Sunderland, Ipswich, Aston Villa na Nottingham Forest.

Alishinda tuzo ya Kocha wa Mwaka wakati alipoipandisha Sunderland mwaka 2007 kabla ya kujiuzulu mwaka 2008.