Ronaldo wa mwisho kulikubali benchi

Muktasari:

Ronaldo anajiamini. Anapenda mazoezi mpaka amepitiliza. Unaweza kumuita katika benchi kama amefunga au amepika mabao, au ameumia. Unaweza kumuita katika benchi kama timu yake inaongoza kwa tofauti ya mabao matatu.

MARA mbili ndani ya mechi tatu zilizopita pale Italia benchi limemuita Cristiano Ronaldo. Kocha wake, Maurizio Sarri amechukua maamuzi magumu ya kumwita benchi Ronaldo na nafasi yake kuchukuliwa na watu wengine wanaokwenda kuokoa jahazi.

Bahati nzuri wote walioingia walikwenda kuisaidia timu. Mechi ya wikiendi iliyopita Ronaldo alikasirika na kutimkia katika vyumba vya kubadilishia nguo na kisha akaondoka zake uwanjani mapema kabla ya mechi haijamalizika.

Sasa hatima ya Ronaldo ipo hewani pale Turin. Sarri ni kocha mwenye kiburi na maamuzi magumu. Nadhani ataendelea kufanya anachofanya. Upande wa pili simuoni Ronaldo akikubali benchi kwa urahisi pale Turin.

Ronaldo anajiamini. Anapenda mazoezi mpaka amepitiliza. Unaweza kumuita katika benchi kama amefunga au amepika mabao, au ameumia. Unaweza kumuita katika benchi kama timu yake inaongoza kwa tofauti ya mabao matatu.

Vinginevyo hawezi kujiona akitolewa uwanjani kwa ajili ya kumpisha mchezaji ambaye kocha anaamini kwamba atakwenda kufanya mambo makubwa kuliko Ronaldo. Kwa tunaomtazama kwa nje tunaweza kuona kwamba labda Ronaldo amepwaya lakini Ronaldo mwenyewe kwa hulka zake hawezi kujiona amepwaya. Ndivyo alivyo. Ni mshindani.

Lakini zaidi ni hata akina Muhammad Ali na Mike Tyson wakati ubora wao ukiondoka hawakuweza kukiri moja kwa moja kwamba nyakati zimewapita.

Waliendelea kupambana na nyakati. Wakati fulani wakapokea vipigo vya aibu. Ndivyo itakapokuwa kwa Ronaldo.

Sio Ronaldo tu. Hata Lionel Messi. Kwa sasa anakubali kwenda katika benchi kama timu yake inaongoza kwa tofauti ya mabao. Siamini kama anaweza kukubali kwamba kuna mchezaji anayeweza kutoka katika benchi na kuisaidia timu kupata matokeo kuliko yeye aliye uwanjani.

Vita ya Sarri inaweza kumuondoa Ronaldo Juventus. Sioni kama anaweza kwenda katika kioo chake na kujinong’oneza kwamba amekwisha. Kila siku ataamini kwamba yeye ndiye mwokozi wa timu yake.

Hata kama Sarri alipatia katika mabadiliko yake ya kumtoa Ronaldo na kumuingiza mtu mwingine mwenye uwezo zaidi bado sioni kama Ronaldo atakubali janga hili kwa muda mrefu.

Kuna wachezaji wachache sana washindani zaidi ya Ronaldo. Amejitengeneza kuwa alivyo kwa sababu ni mshindani.