Ronaldo ndo nani ? mpango mzima huu

Muktasari:

  • Nakumbuka mwaka jana, yeye na Real Madrid walivyowakatili Juventus ambao walikuwa na kiu kubwa ya kuingia fainali na kutwaa kombe, mwenye kiu zaidi akiwa golikipa na nahodha wao, Gianluigi Buffon, aliyekuwa akimaliza msimu ili ang’atuke, lakini tamaa yake ya mwisho ilikuwa kutwaa kombe hilo, maana ubingwa wa nchi kwa Juve ni kitu cha kawaida.

WIKI iliyopita tulishuhudia matokeo ya ajabu kiasi kwenye soka. Aliyetarajiwa kusonga mbele katika Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL) alitupwa nje na aliyeonekana kuwa msindikizaji akigeuka kuwa msafiri.

Achana na yale ya Tottenham Hotspur kuwatoa Manchester City waliokuwa wakitarajiwa kurekebisha makosa ya mchezo wa kwanza hapa London ambapo walifungwa 1-0, wakitarajiwa wange shinda nyumbani kwao Etihad kwa tofauti ya kutosha ya mabao, lakini aikuwa, wakalingana mabao, na Spurs wakasonga kwa faida ya mabao mengi zaidi ya ugenini.

Nataka tutazame yale ya ‘underdogs’ Ajax kutoka Uholanzi kuwavimbia Juventus waliokuwa nyumbani kwao Torino. Ilikuwa kama moja ya maajabu ya soka, kwa sababu Ajax walishinda 2-1 na kuwafurusha Juve kwenye mashi ndano hayo makubwa.

Na kwenye mashi ndano haya, mtu ambaye amekuwa kama alama yake kubwa katika miaka ya karibuni ni Cristiano Ronaldo – mtaalamu wa kucheka na nyavu, mkongwe wa kupiga mabao matatu kwa mechi moja, mtu makini katika kusaidia kubadili mchezo kwa mbinu zake.

Na kwa miaka mitatu mfululizo, amelinyanyua kombe hilo akiwa na Real Madrid ya kocha Zinedine Zidane, ikimaanisha alikuwa uwanjani kwa karibu mechi zote za UCL tangu hatua za makundi hadi mitoano yote, na kwa hakika alionekana kuwa na mchango mkubwa.

Nakumbuka mwaka jana, yeye na Real Madrid walivyowakatili Juventus ambao walikuwa na kiu kubwa ya kuingia fainali na kutwaa kombe, mwenye kiu zaidi akiwa golikipa na nahodha wao, Gianluigi Buffon, aliyekuwa akimaliza msimu ili ang’atuke, lakini tamaa yake ya mwisho ilikuwa kutwaa kombe hilo, maana ubingwa wa nchi kwa Juve ni kitu cha kawaida.

Sasa ikaja kuwa jambo la kubadilishana vile, ghafla mwishoni mwa msimu, Ronaldo akaamua kuondoka Real Madrid akajiunga na Juventus huku Buffon akiwa ameshang’atuka na kuagana na wenzake kwenye Allianz Stadium hapo Torino.

Kweli Juventus wakavuka makundi na kuingia robo fainali ya kwanza iliyofanyika jijini Amsterdam, wakatoka sare ya 1-1, wakijiamini kwamba wangeenda kuua gemu nyumbani Allianz Stadium, uwanja ambao mara nyingi hapo Italia huurejea tu kwa jina la ‘Stadium’.

Mashabiki waliamini wanaenda kushinda, wachezaji hawakuwa na wasiwasi na benchi la ufundi chini ya kocha mahiri Massimiliano Allegri walijua kabisa ni zamu yao, kama Tanzania walivyokuwa wakiimba kwamba vijana wa Serengeti Boys mwaka huu ni zamu yao hadi Brazil lakini wapi.

Juve kwa kweli waligeuzwa kama watu wa kufundishwa soka na vijana hao wa Ajax ambao huku Ulaya kurejewa kama Academy. Ni vijana wadogo tu, wasio na uzoefu mkubwa wala maumbo au misuli ya kutishia wakongwe.

Ajax ndiko timu nyingi kubwa huenda kuchungulia na kununua makinda.

Sasa vijana hao hao wadogo wakawaonesha Juventus kwamba soka inabaki kuwa soka tu bila kujali wanaye Ronaldo ndani au la. Nigusie kidogo tu kwamba Real Madrid ambao hawakuwa na Ronaldo msimu huu tayari wametupwa nje; kwa maana nyingine wameshavuliwa ubingwa wa dunia waliokuwa wanataka wautetee kwa mara ya nne.

Kila mtu alikuwa akimwangalia Ronaldo na jezi yake ile ya Jeep, wakimsubiri afanye mambo. Badala ya kuwa msaada, inaelekea Ronaldo au CR 7 kama anavyojiita na akiwa na chapa hiyo kwenye biashara zake, zikiwamo za mavazi, alionekana kutengeneza tatizo maana kuna wachezaji waliamini kwamba madhali yumo uwanjani, basi wao wangeweza kulegalega tu naye hatimaye angewashindia gemu kirahisi tu.

Nilishuhudia Juventus wakipunguza jitihada kidogo kidogo – wakidhani ingetosha tu na kwamba ushindi ulikuwa wao wala halikuwa suala la ‘jasho na damu’.

Walikuja kuhamaki na kuanza kupiga mpira walipomaizi kwamba walikuwa wakihitaji mabao mawili ili wabaki ndani ya UCL.

Wakaanza kupigwa mshangao, kuchanganyikiwa huku Emre Can na BlaiseMatuidi wakihaha kuudhibiti mpira bila mafanikio ya kutosha. Akili yangu ikarudi nyuma miaka minne iliyopita, nikaanza kulinganisha kikosi cha Juve kisichokuwa na uwiano na kile cha Allegri kilichopoteza 3-1 kwa Barcelona pale Berlin, Ujerumani katika fainali.

Kikosi kile kilikuwa na wachezaji matata kama Andrea Pirlo, Paul Pogba, Arturo Vidal, Carlos Tevez na Alvaro Morata.

Lakini miaka minne baadaye, Allegri amepoteza nguvu ile kubwa iliyoiunganisha timu, kikosi kikijawa ubinafsi zaidi, na Ronaldo kwa asili ni mbinafsi; hapendi mshindani ndani ya timu, anataka afunge yeye tu mabao na akifunga mwingine anaweza si tu kutoshangilia bali pia kukunja ndita na kukimbia mbali na mfungaji ili asimpongeze.

Ronaldo wa fainali za Kombe la UCL sasa amekuwa wa kuishia robo fainali; aliyedhaniwa alikuwa akihamisha kombe kutoka Santiago Bernabeu ya Real Madrid kupeleka Torino kwa Juve amekosa kote. Ili kuimarisha timu, Juve wakatoa pauni milioni 88 kumnunua mbinafsi mkuu wa soka, na sasa imewagharimu; watoto wa mjini husema imekula kwao.

Kimsingi pauni milioni 88 walizotumia Juve kumnunua Ronaldo zimeleta tofauti kidogo katika mwonekano mzima kama pauni milioni 75 walizomnunulia Gonzalo Higuain 2016.

Wamejiamulia kwamba njia bora zaidi ya kutwaa UCL ni kununua mtu mmoja mkubwa aliyepo na kusahau umoja wao, uendelevu na maendeleo kama timu. Unapokuwa na alama 17 juu ya wenzako kwenye Ligi Kuu ya nchi yako – kama walivyokuwa hawa kwenye Serie A (na sasa wametwaa ubingwa tayari wa Italia) basi unaweza kudhani umeweka sawa kila kitu.

Hata hivyo, walipoenda mapumziko wakiwa na sare ya 1-1, walijua kwamba kulikuwapo hatari, lakini wakajipa matumaini kwamba wao ni wakubwa nawangewanyamazisha Ajax madhali Ronaldo alikuwapo. Hadi hapo matokeo yauwiano yakawa 2-2, kila mmoja akiwa na bao moja la ugenini, ngoma ilikuwa mbichi.

Kama utani vile, na kama Daudi alivyomuua Goliati, Ajax wakawadunga Juventus bao la pili zikiwa zimesalia dakika 23 mechi kumalizika. Daudi alimuua Goliati mara moja tu, lakini Ajax alikuwa ametoka kuwapiga Real Madrid 4-1 kule Santiago Bernabeu mwezi uliopita na sasa walikuwa mbele kwa mabao mawili Allianz.

Juventus wakaanza kupoteana, mpira ukawa haukai miguuni pao, macho sijui yalikuwa hayaoni vyema tena na Ronaldo akawa si yule wa uokoajiambaye aliwaokoa Juve mbele ya Atletico kwa kutundika hat-trick.

Hakuna kitu kinachochosha kama kusubiri; Ronaldo akasubiriwa awavushe, dakika zikaanza kuhesabiwa na ujue hapo walikuwa anahitaji mabao mawili haikuwa hivyo.

Hapakuwapo na cha mleta kombe la UCL Juventus wala cha ‘game changer’safari hii. Juve walitakiwa kucheza kitimu tangu awali, kupunguza kujiamini na Ronaldo apunguze ubinafsi uliokithiri anaouonesha zaidi kwa kujigonga kifua.